Bashungwa: Sijapewa fedha za maendeleo wizara ya viwanda, biashara 2019-2020

Mwandishi Wetu 1316Hrs   Mei 05, 2020 Biashara

Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara yake ya mwaka 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo. Picha|Wizara ya Viwanda na Biashara.


  • Hadi mwezi Machi 2020 wizara hiyo haikupata fedha zozote kwa ajili ya shughuli za maendeleo zilizotengwa katika bajeti ya 2019/2020.
  • Pia yashindwa kukusanya kabisa mapato iliyoidhinishiwa mwaka huu.
  • Bajeti yake ya 2020/2021 yashuka kwa Sh19.1 bilioni  hadi Sh81.4 bilioni.

Dar es Salaam. Waziri wa Viwanda na Biashara Innocent Bashungwa amesema hadi kufikia mwezi Machi 2020 wizara yake haikupata fedha zozote kwa ajili ya shughuli za maendeleo zilizotengwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2019/2020 , jambo ambalo kamati ya Bunge imesema linarudisha nyuma juhudi za kujenga uchumi wa viwanda. 

Katika mwaka 2019/2020, Wizara ya Viwanda na Biashara katika fungu 44 na 60 iliidhinishiwa na Bunge la Tanzania  matumizi ya jumla ya Sh100.4 bilioni.

Kati ya hizo, Sh 51.5 bilioni zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo na kiasi hicho kilichobaki kilielekezwa katika matumizi ya kawaida ya wizara ikiwemo kulipa mishahara. 

Waziri huyo amesema licha ya wizara yake kuidhinishiwa kiasi hicho cha fedha kwa ajili ya matumizi ya maendeleo lakini hadi Machi mwaka huu haikuwa imepata hata senti moja. 

“Wizara haikupata fedha kwa ajili ya matumizi ya maendeleo,” amesema Bashungwa leo (Machi 5, 2020) bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2020/2021.  

Hata hivyo, wizara hiyo ilipokea Sh33.8 bilioni sawa na asilimia 69.2 ya fedha zote zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida. 

Aidha, Bashungwa ameliambia Bunge kuwa katika mwaka huu, wizara yake iliidhinishiwa kukusanya jumla ya Sh14.3 milioni (inayojumuisha fungu 44 Sh5.3 milioni na fungu 60 Sh9 milioni) kutokana na uuzaji wa nyaraka za zabuni na marejesho ya mishahara endapo mtumishi ataacha kazi. 

Lakini hadi kufikia Machi 31 mwaka huu,  wizara haikufanikiwa kukusanya kiasi chochote kutoka vyanzo hivyo.

Waziri huyo hajasema ni kwanini wizara yake haijapata fedha za maendeleo na haijakusanya fedha ilizoidhinishiwa mwaka huu. 

Pamoja na changamoto hizo za mapato na matumizi, Bashungwa amesema wamefanikiwa kutekeleza malengo ya bajeti hiyo ikiwemo miradi ya uwekezaji mipya 303 iliyosajiliwa na kulinda viwanda vya ndani kwa kuhakikisha vinapata malighafi ya kutosha kufanikisha uzalishaji.

“Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kufanya marejeo ya Sera ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ya mwaka 2003,” amesema.


Soma zaidi: 



Utekelezaji wa bajeti ya 2020/2021

Wizara hiyo imeomba kuidhinishiwa bajeti ya Sh81.4 bilioni kwa ajili ya mwaka ujao wa 2020/2021 huku ikisema katika mwaka huo inakadiria kuwa itakusanya Sh15 milioni. 

Hata hivyo, bajeti hiyo ya mwaka ujao imeshuka kidogo kwa Sh19.1 bilioni ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2019/2020 ambayo ilikuwa Sh100.4 bilioni Kati ya fedha hizo zitakazotumika 2020/2021, Sh29.6 bilioni zitakuwa za matumizi ya maendeleo sawa na asilimia 36.4 ya bajeti yote ya wizara hiyo na zilizosalia zitatumika katika matumizi ya kawaida.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge wa Viwanda, Biashara na Mazingira Suleiman Masoud Nchambi amesema kwa mwenendo usioridhisha wa utoaji wa fedha kwa Wizara ya Viwanda na Biashara, miradi mingi iliyopanga haitatekelezwa kwa wakati, jambo litakalorudisha nyuma juhudi za kujenga uchumi wa viwanda.

“Kamati inaishauri Serikali kuhakikisha fedha zinazoidhinishwa na Bunge zinapelekwa kwa wakati ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu yote yaliyokusudiwa,” amesema Kanali mstaafu Nchambi. 

Amesema kamati yake inapendekeza kuongeza kasi ya utekelezaji wa  malengo ya wizara  ili kufikia malengo iliyojiwekea ikiwemo ujenzi wa viwanda na kuboresha mazingira ya biashara nchini. 

Related Post