Bajeti ya Wizara ya Ulinzi yapaa kwa mara ya pili mfululizo

May 6, 2020 3:46 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imekuwa ikiongezeka mfululizo tangu mwaka 2018/2019.
  • Mwaka 2020/21 itatumia Sh2.14 trilioni, kikiwa ni kiwango cha juu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
  • Serikali yatakiwa kutoa fedha kwa wakati ili wizara itekeleze majukumu yake. 

Dar es Salaam. Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inakusudia kutumia bajeti ya Sh2.14 trilioni katika mwaka wa fedha 2020/21 ikiongezeka kutoka Sh1.85 trilioni iliyopitishwa mwaka 2019/20 huku Serikali ikitakiwa kutoa fedha kwa wakati ili kufanikisha mipango ya wizara hiyo.

Bajeti hiyo inaongezeka kwa mara ya pili mfululizo tangu ilivyoanza kuongezeka katika mwaka huu wa fedha unaoishia Juni 2020 kutoka Sh1.67 trilioni ya mwaka 2018/19.

Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama amewasilisha hotuba ya bajeti kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Hussein Mwinyi. 

Mhagama aliyeomba kuidhinishiwa fedha hizo leo (Mei 6, 2020) Bungeni jijini Dodoma amesema kati ya fedha hizo, Sh1.9 trilioni sawa na asilimia 92.4 ya bajeti yote zitaelekezwa katika matumizi ya kawaida.

Kiasi kilichobaki ambacho hakizidi asilimia nane ya bajeti yote ndiyo kitatumika kutekeleza shughuli za maendeleo za wizara hiyo nyeti nchini Tanzania. 

Wizara hiyo ni miongoni mwa wizara zilizovuka bajeti ya Sh1 trilioni ikiwemo ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. 

Bajeti hiyo ya mwaka ujao wa 2020/2021 ndiyo bajeti ya kiwango cha juu  kabisa kwa wizara hiyo ndani ya miaka minne iliyopita. 

Tayari Bunge limeshaidhinisha bajeti hiyo baada ya kuijadili tangu ilipowasilishwa mchana wa leo. 


Soma zaidi: 


Vipaumbe vya 2020/2021

Waziri Mhagama amesema mwelekeo wa kazi zinazokusudiwa kufanywa na wizara hiyo mwaka 2020/21 utazingatia maeneo ya kipaumbele ya kuliimarisha jeshi kwa zana na vifaa vya kisasa, mawasiliano pamoja na rasilimali watu.

“Tutaendelea kuweka mazingira mazuri ya utendaji kazi kwa Wanajeshi ikiwemo mafunzo, matunzo ya zana na miundombinu, maslahi, huduma bora za afya, ofisi na makazi,” amesema Mhagama.

Amesema Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) litaongezewa uwezo kwa kuboresha miundombinu ili liweze kuchukua vijana wengi zaidi na kutoa mafunzo ya uzalendo, ukakamavu, umoja wa kitaifa na stadi za kazi kwa vijana wa Kitanzania.

Wizara hiyo pia itaendeleza tafiti na uhawilishaji wa teknolojia kwa ajili ya kuzalisha bidhaa na huduma kwa matumizi ya kijeshi na kiraia na kuimarisha na kuratibu Jeshi la Akiba.Aidha, amesema wataendelea kutumia rasilimali walizonazo zikiwemo hospitali na kulinda mipaka ya nchini ili kupambana na COVID-19.

 “Wizara inaendelea kutoa elimu kwa Watumishi kuhusu ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya corona (COVID-19) na namna ya kujikinga,” amesema Waziri Mhagama.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama katika mapendekezo yake kuhusu bajeti hiyo imeishauri Serikali kutoa fedha zilizoidhinishwa kwa wakati kwa wizara hiyo ili shughuli zilizopangwa zifanyike kwa wakati.

“Pamoja na kuongezeka kwa bajeti ya wizara hii ya 2020/21, Serikali itoe kipaumbele kwa wizara hii wakati wa kutoa fedha hizo kwa mafungu husika,” amesema Mbunge wa Uyuwi Almasi Maige wakati akiwasilisha  mapendekezo ya kamati hiyo.

Amesema Serikali iyapatie fedha za kutosha mashirika ya utafiti ya Nyumbu na Mzinga ya wizara hiyo  ili yaweze kuendeleza tafiti zake zinazoendelea zenye tija kwa nchi yetu ikiwemo utengenezaji wa magari.

Enable Notifications OK No thanks