Tamnoa yazungumzia Serikali kupunguza tozo miamala ya simu
- Yasema itarejesha wateja walioacha kutumia huduma hizo.
- Baadhi ya wananchi waomba zifutwe kabisa.
- Serikali yasisitiza kutozifuta na zitaendelea kutozwa.
Dar es Salaam. Wakati kukiwa na maoni mchanganyiko kuhusu uamuzi wa Serikali wa kupunguza tozo za miamala ya simu kwa asilimia 30, watoa huduma za mawasiliano ya simu Tanzania wamesema uamuzi huo utarejesha wateja wao walioacha kutumia huduma hizo.
Serikali ilishusha viwango hivyo vya tozo baada ya Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kutia saini marekebisho ya Kanuni za Tozo za Miamala ya Kieletroniki za Kutuma na Kutoa Fedha za Mwaka 2021 mnamo Agosti 31, 2021
Pia watoa huduma za simu waliridhia kupunguza viwango vya tozo wanazotoza katika miamala ya kutuma na kutoa fedha kati ya mtandao na mtandao mwingine kwa asilimia 10.
Viwango vilivyopunguzwa vilitangazwa rasmi kwa tangazo la Serikali Septemba Mosi mwaka huu.
Wakati baadhi ya watu wakisema tozo hizo zifutwe au zipunguzwe zaidi, Chama Cha Watoa Huduma za Mawasiliano ya Simu Tanzania (Tamnoa) kimesema uamuzi wa Serikali ni wa busara kwa sababu utachangia kuongeza kasi ya miamala ya fedha inayofanyika kwa njia simu.
Mwenyekiti wa chama hicho, Hisham Hendi amesema tangu utekelezaji wa tozo hizo ulipoanza Julai mwaka huu, watu wanaotumia huduma za kifedha kwa njia simu walianza kupungua bila kutaja kwa kiwango halisi.
“Tunaipongeza Serikali kwa kupunguza asilimia 30 na kutoweka miamala ya bei ya chini katika utekelezaji wa agizo hili. Tunatumai hii pamoja na upunguzaji wa asilimia 10 ya ada za miamala kwenye miamala inayofanyika baina ya wateja wa makampuni tofauti zitarudisha wateja ambao waliacha kufanya miamala tangu kuanza kwa utekelezaji wa agizo hili,” amesema Hendi katika taarifa yake iliyotolewa leo Septemba 2, 2021.
Hendi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Vodacom Tanzania anayemaliza muda wake amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa tozo hizo ili ziwe na manufaa kwa Watanzania.
Amesema pia watashirikiana katika kutafuta njia bora zaidi za jinsi ya kupata majukwaa ya kidijitali yatakayowezesha ukusanyaji wa kodi kwa ukaribu na mamlaka husika na wadau wengine ili kuhakikisha kunakuwa na usawa katika kutimiza matazamio ya jamii.
“Katika enzi hii ya mapinduzi ya nne ya viwanda, sekta inayostawi ya mawasiliano ina jukumu muhimu la kuwezesha sekta zingine kama teknolojia ya kilimo (Agritech), huduma ya matibabu kwa video (telemedicine) na malipo ya Serikali na huduma ili kuendelea kuchangia ukuaji wa Taifa,” amesema mwenyekiti huo wa Tamnoa.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Lameck Nchemba akisaini marekebisho ya Kanuni za Tozo za Miamala ya Kielektroniki za Kutuma na Kutoa Fedha kwa Mwaka 2021, marekebisho hayo yamepunguza viwango vya tozo za miamala hiyo kwa asilimia 30, Agosti 31, 2021 jijini Dodoma. Picha| Wizara ya Fedha na Mipango.
Kupunguzwa kwa tozo hizo kunatokana na kuwepo kwa malalamiko lukuki kwa watumiaji wa huduma za simu Tanzania ambazo wengi wamesema zinawaumiza kwa kuongeza gharama za maisha.
Baadhi ya wananchi walioongea na Nukta Habari (www.nukta.co.tz) wamesema Serikali imefanya jambo jema kupunguza tozo hizo lakini ifikirie kuzifuta kabisa maana zinawaumiza.
“Ni hatua nzuri maana wengi tuliacha kutuma hela kwa simu. Itasaidia turudi tena lakini kama Serikali inaweza waziondoe kabisa tozo hizo,” amesema Eliud Mwakipembe, mkazi wa kata ya Mabatini mkoani Mbeya.
‘Tozo ziko palepale’
Wakati baadhi ya watu wakishauri tozo zifutwe kabisa, Rais Samia Suluhu Hassan amesema haina mpango wa kuzifuta, zitaendelea kuwepo kwa sababu zinasaidia utekelezaji wa miradi mbalimbali huku akibainisha kuwa miezi miwili tangu Serikali kuanza kukata kodi hiyo imekusanya Sh60 bilioni zitakazojenga vituo vya afya 220.
“Fedha zitakazokusanywa kama tozo katika miamala ya simu mwezi Septemba na Oktoba zitakwenda kujenga madarasa zaidi ya 500 Tanzania nzima,” amesema Rais Samia leo wakati akizungumza na wananchi katika kata ya Tegeta akiwa njiani kuelekea Bagamoyo mkoani Pwani.
Latest