Azam yapata leseni ya kuonyesha chaneli za bure, DSTV, Zuku wanafuata
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye mesema kuruhusu chaneli za ndani kuonyeshwa kwa kutumia leseni za kimataifa kutazifanya chaneli za ndani kuwa za kulipia badala ya kuonekana bure. Picha|Mtandao.
- Serikali imesema tayari kampuni ya Azam imepata leseni hiyo jana huku DSTV na Zuku nazo zimewasilisha maombi ambayo yanafanyiwa kazi na TCRA.
- Agosti 2018, visimbuzi vya DSTV, Zuku na Azam vilizuiwa kuonyesha chaneli za bure kwa sababu zilikiuka masharti ya leseni zao.
- Kutolewa kwa leseni hizo kutatanua wigo wa kupata habari kwa wananchi.
Dar es Salaam. Wigo wa wananchi kupata hanari mbalimbali nchini huenda ukaongezeka baada ya kampuni ya Azam inayomiliki kituo cha runinga cha Azam TV kupata leseni kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya kurusha chaneli zisizo za kulipia.
Agosti 2018, visimbuzi vya kampuni za Multichoice Tanzania (DStv), Simbanet Tanzania (Zuku) na Azam vilizuiwa kuonyesha chaneli za zisizo za kulipia za ndani ya nchi kutokana na masharti ya leseni zao kukidhi mfumo wa soko la kimataifa na maudhui yake huwa ni ya kulipia.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye amesema Azam walikuwa miongoni mwa makampuni yaliyoomba leseni hiyo ambapo wamekabidhiwa tayari kwa ajili ya kuendelea na mchakato wa ujenzi wa miundombinu itakayowezesha chaneli za bure kuonekana katika kisimbuzi chake.
“Kati ya watu walio apply (omba) leseni za kuonyesha chaneli zisizo za kulipia, Azam wapo na ni jana wamepokea hiyo leseni na wametuhakikishia kwamba ndani ya miezi saba watakuwa wamejenga DDT (miundombinu) katika maeneo yote ya nchi yetu kwa ajili ya kurusha chaneli hizo za bure,” amesema Nditiye wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi mapema leo (Mei 14, 2019) bungeni.
Hatua hiyo ya Azam kupata leseni inaongeza idadi ya kampuni zinazotoa huduma ya kuonyesha chaneli zisizo za kulipia na kufikia nne ukiachilia mbali kampuni ya Basic Transmission Ltd inayomiliki visimbuzi vya Continental na Digitek; Star Media (Startimes); na Agape Associates (Ting).
Chaneli za ndani zisizo za kulipia hujumuisha TBC 1, ITV, Star TV, Channel TEN, East Africa TV, Safari Chennel na Clouds TV.
Hata hivyo, Nditiye amesema DSTV na Zuku na wamewasilisha maombi ya kupata leseni za kuonyesha chaneli zisizo za kulipia na maombi yao yanafanyia kazi na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Maombi hayo yamepokelewa na hatua iliyopo sasa ni TCRA kuyapitia na kutoa ushauri kuhusu utoaji wa leseni hizo kwa makampuni husika.
“Kwa sasa TCRA inashughulikia maombi yaliyopokelewa ili iweze kushauri utoaji wa leseni stahiki,” amesema Nditiye.
Zinazohusiana:
- Mwakyembe aingilia kati sakata la TCRA na kampuni za visimbuzi.
- TCRA yakusudia kusimamisha leseni za DSTV na Zuku.
Awali akijibu maswali mawili ya Mbunge wa jimbo la Nyamagana, Stanslous Mabula aliyetaka kujua ni lini Serikali itatoa muafaka wa upatikanaji wa chaneli za bure kwenye visimbuzi vya DSTV, Zuku na Azam ikizingatiwa kuwa wananchi wanakosa fursa ya kufahamu mambo yanayoendelea nchini kutokana na visimbuzi hivyo kutokuonyesha chaneli za ndani.
“Serikali kupitia TCRA imefanya jitihada ikiwa ni pamoja na kukaribisha maombi ya leseni ya kubeba maudhui ya chaneli za ndani yaani multiplex operators kutoka kwa wanaohitaji yakiwemo makampuni ya Azam, DSTV na Zuku ili yaweze kupata leseni stahiki na kuweza kubeba au kutoa huduma za maudhui ya ndani kupitia visimbuzi vyao,” amesema Mhandisi Nditiye.
Amesema Serikali inafahamu umuhimu wa wananchi kujua mambo yanayoendelea kwenye Taifa kwa misingi hiyo imetoa leseni zenye masharti tofauti ikiwemo ya utangazaji wa umma ambapo matangazo huruhusiwa kurushwa kwa watoa huduma wenye ‘must carry’ katika runinga za TBC 1 na TBC 3 maarufu kama Safari Channel,
Amebainisha kuwa makampuni yanayomiliki visimbuzi vya DSTV, Zuku na Azam hayakustahili kubeba chaneli za ndani zisizolipiwa (free to air local channels) kutokana na masharti ya leseni zao.
Masharti ya leseni hizo na mfumo wa mzima wa miundombinu ya utangazaji husika yamelenga soko la kimataifa na hutofautiana na masharti ya leseni za watoa huduma za ndani ya nchi.
Amesema kuruhusu chaneli za ndani kuonyeshwa kwa kutumia leseni za kimataifa kutazifanya chaneli za ndani kuwa za kulipia badala ya kuonekana bure.
Latest
