Ifahamu mikoa 5 yenye visimbuzi vichache Tanzania

November 5, 2022 10:23 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Songwe, Katavi, Simiyu, Njombe na Simiyu.
  • Dar es Salaam kinara kwa kuwa na visumbuzi vingi.

Dar es Salaam.  Licha ya televisheni kuwa chombo muhimu cha kupashana habari za maendeleo, baadhi ya watu bado hawapati huduma hiyo kutokana na kushindwa kupata huduma ya visimbuzi katika mikoa yao.

Kisimbuzi ni kifaa kinachotumika kupokea matangazo yanayorushwa kwa mfumo wa digitali ili yaonekane na kusikika hata kwenye televesheni.

Huduma ya visimbuzi  iliidhinishwa rasmi nchini mwaka 2011 na kuwa  nyenzo muhimu ya wananchi kupata taarifa mbalimbali za runinga kidigitali.

Ripoti mpya ya Takwimu za Mawasiliano ya robo ya tatu ya mwaka 2022 ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha kuwa  idadi ya visimbuzi nchini imeongezeka kwa asimia 4.9 kutoka visimbuzi milioni 3.1 vilivyokuwepo Juni na kufikia  milioni 3.3 mwezi Septemba mwaka huu.

“Kati ya hivyo, milioni 1.65 ni vya dijitali kwa mfumo wa televisheni wa utangazaji wa mitambo ya ardhini (DTT) ikilinganishwa na milioni 1.67 kwa mfumo wa televisheni kwa satelaiti,” imeeleza ripoti hiyo.

Hata hivyo,  kwa baadhi ya mikoa wakazi wake hawajawahi au wanaomiliki kifaa hicho cha dijitali ni wachache, jambo linaweza kuchangia kuwakosesha taarifa muhimu kuhusu maisha yao na maendeleo.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Songwe ndiyo mkoa wenye simbuzi vichache zaidi Tanzania Bara. Hadi kufikia Septemba mwaka huu ulikuwa na visimbuzi 1,568 tu. 

Kwa mujibu wa Takwimu za Msingi za mwaka 2021 zinazotolewa na  Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mkoa huo wenye Wilaya nne unakadiriwa kuwa na watu milioni 1.7. 

Ukigawanya idadi hiyo kwa kaya zenye angalau wanafamilia watano ni sawa na kusema kaya 313 tu mkoani humo ndiyo zenye vingamuzi majumbani mwao kati ya kaya 343,521 zilizopo mkoani humo. 

Visimbuzi  hivyo vilivyopo mkoani Songwe ni pungufu mara 810 zaidi ya vile vilivyopo kwenye jiji la Dar es Salaam.

Ripoti hiyo ya robo ya tatu ya mwaka 2022 inaonyesha mikoa mingine iliyoshika mkia kwenye idadi ya visimbuzi ni pamoja na Simiyu wenye visimbuzi 11,849 ikifuatiwa na Katavi ikiwa na visimbuzi 16,990.

Mikoa mingine ni Njombe visimbuzi 17,778 na Mkoa wa Rukwa ambao ulikuwa na visimbuzi 18,509 ilipofika Septemba mwaka huu.

 Dar es Salaam Kinara wa visimbuzi Tanzania

Takwimu  hizo zinaonyesha kuwa Mkoa wa Dar es Salaam unaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya  visimbuzi ambapo hadi kufikia mwezi Septemba ilikuwa na jumla ya visimbuzi milioni 1.3.

Visimbuzi  hivyo vilivyopo jijini humo ni zaidi ya nusu ya visimbuzi vyote vilivyopo nchini.

Dar es Salaam imefuatiwa kwa mbali na  Arusha yenye visimbuzi  272,702, Mwanza (261,237) na Mbeya visimbuzi 218,007.

Kampuni ya Startimes ndiyo inashikilia sehemu kubwa ya soko la ving’amuzi nchini ambapo kwa mujibu wa TCRA, hadi Septemba ilikuwa na watumiaji wa visimbuzi milioni 2.08.

Hiyo ni sawa na kusema asilimia 63.6 au kwa kila vsimbuzi 10 vilivyopo nchini sita ni vya Startimes ambayo inachuana vikali na Azam ambayo ina visimbuzi 887,959 huku kampuni ya Agape ndiyo yenye vichache zaidi (4,001).

Ipi sababu ya ukosefu wa  visimbuzi kwenye mikoa hiyo

Mtaalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) Emmanuel  Sabali anasema chanzo kikuu cha ukosefu wa huduma ya visimbuzi katika baadhi ya mikoa ni uchumi mdogo uliopo kwenye kaya na maeneo husika.

Licha ya kuwepo kwa chaneli za bure kwenye baadhi ya visimbuzi itakulazimu kulipia baadhi ya chaneli ili uweze kuhabarika zaidi kwa habari au burudani nyingine zinzopatikana kwenye visimbuzi hivyo.

Malipo ya kila mwezi ya visimbuzi hivyo  husababisha baadhi ya watu kukimbia kabisa huduma hiyo kwa kushindwa kumudu gharama za vifurushi.

“Unakuta kima cha chini cha kulipia kisimbuzi kwa mwezi ni Sh9,000 au 10,000 alafu mtu akilipie kila mwezi inakuwa ni changamoto,” anasema Sabali.


Zinazohusiana:


Naye Danford Kija mshauri na mtengenezaji wa mifumo ya kompyuta  anasema sababu nyingine ya baadhi ya kaya au mikoa kukosa huduma hiyo ni vipaumbele walivyojiwekea.

“Miji ambayo ni ya kilimo unakuta vipaumbele vyao ni mashamba na kilimo kuliko ununuzi wa visimbuzi,” anasema Kija huku akibainisha kuwa uelewa mdogo wa masuala ya teknolojia nao unachangia. 

Suala hilo linaweza kuchangia kuwakosesha taarifa muhimu vijana na watoto hasa zile zinazohusu maendeleo ya teknolojia.

“Watoto na vijana ndio waathirika wakubwa wa ukosefu wa huduma hiyo, kuna aarifa nyingi za muhimu ambazo ni lazima uzitazame kwenye televisheni ndipo zieleweke,” anasema Kija.

Hata hivyo mtengenezaji huyo wa mifumo ya kompyuta anasema ni vyema kuangalia pia tawimu za matumizi ya redio au vifaa vingine vya upashanaji habari, kwa sababu kila mtu ana njia yake anayoamini katika kupata habari.

Mtaalamu huyo ameongeza kuwa mtu akiwa na vyanzo vyote vya taarifa ikiwemo televisheni redio na vifaa janja  anakuwa na faida zaidi kulinganisha mwenye kifaa kimoja au wasiokuwa navyo kabisa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW