Chaneli mpya ya utalii Tanzania yapata leseni kuonyeshwa bila malipo

January 16, 2019 8:14 pm · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza na wajumbe wa Kamati Maalum iliyoundwa na serikali ya kusimamia uboreshaji wa Channel ya Utalii ya  TBC ya Tanzania Safari Channel jijini Dodoma Januari 16, 2019. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Imepatikana baada ya kukamilisha usajili na itaanza kuonekana kwenye kisimbusi cha AZAM namba 109.
  • Chaneli hiyo itakuwa kiungo muhimu katika kutangaza utalii wa Tanzania ambao haupewi hadhi inayohitajika.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amepokea leseni ya usajili wa chaneli ya utalii ya Tanzania Safari ambayo itaiwezesha kuonyeshwa kwa umma bila ya malipo(a must-carry channel) na wamiliki wa visimbusi nchini.

Majaliwa amekabidhiwa leseni hiyo leo (Januari 16, 2019) kwenye kikao alichokiitisha ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma ambapo alitaka apewe mrejesho kutoka kwa wajumbe wa Kamati Maalum ya kusimamia uboreshaji wa Chaneli hiyo ya utalii Tanzania. 

Akikabidhi leseni hiyo kwa Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Habari Tanzania (TBC), Dk Ayoub Rioba amesema kukamilika kwa usajili huo kumeiwezesha chaneli hiyo ianze kuonekana kwenye kisimbusi cha AZAM namba 109.

Kwa mujibu wa taarifa illiyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Rioba amesema kamati hiyo iliundwa Desemba 21, mwaka jana na inajumuisha wajumbe kutoka taasisi ambata za maliasili na utalii za Tanzania bara na Zanzibar.

 “Baada ya kupata leseni, sasa hivi tunaonekana kwenye kisimbusi cha AZAM chaneli namba 109 na pia kwenye Intelsat ambako tutaweza kuonekana kwenye nchi zote barani Afrika, sehemu kubwa ya bara la Ulaya na Uarabuni,” amesema.


Zinazohusiana: 


Chaneli hiyo itakuwa kiungo muhimu katika kutangaza utalii wa Tanzania ambao haupewi hadhi inayohitajika, jambo linalotoa mwanya kwa baadhi ya watu kufaidika na vivutio vilivyomo nchini isivyo halali.

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (TAWA), Meja Jenerali Mstaafu Hamisi Semfuko amesema chaneli hiyo inaweza kunufaika kwa kupata matangazo kutoka kwa wamiliki wa mahoteli, makampuni ya kutoa huduma za utalii na wenye magari ya utalii.

Tanzania sio nchi ya kwanza kuanzisha chaneli hiyo, zipo nchi mbalimbali ikiwemo Kenya zilizoanza kutumia fursa hiyo muda mrefu kuutangaza utalii katika nchi zao ambapo itakuwa ni muda muafaka kwa Tanzania kufaidika kiuchumi na chaneli hiyo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Dk Allan Kijazi amesema chaneli ya Tanzania Safari imekuja katika wakati muafaka kwa kuwa itaongeza juhudi za taasisi zao kutangaza vivutio vilivyopo nchini na hivyo kuongeza idadi ya watalii wa ndani na wa nje.

 “Uwepo wa chaneli hii utasaidia kuondoa upotoshaji wa makusudi uliokuwa ukifanywa na baadhi ya nchi kuwa vivutio fulani viko kwenye maeneo yao wakati siyo kweli,” amwsema.

Enable Notifications OK No thanks