TCRA yakifungia kipindi cha Polepole, akijibu mapigo
- Imekifungia kipindi chake cha televisheni ya mtandaoni kwa miezi sita.
- Adaiwa kwa uchochezi dhidi ya Uviko-19, deni la Taifa na wamachinga.
- Apokea hukumu, kutoa tamka.
Dar es Salaam. Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imekisimamisha kwa muda kipindi cha mtandaoni cha Mbunge wa kuteuliwa (CCM), Humphrey Polepole kutokana na kukiuka misingi, sheria na kanuni za huduma ya utangazaji ikiwemo kutoa maudhui ya upotoshaji kuhusu Corona (Uviko-19).
Kipindi hicho cha Shule ya Uongozi kinachorushwa katika mtandao wa YouTube kinajulikana kinatumia chaneli ya Humphrey Polepole Online Television.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui wa TCRA, Hans Gunze ametangaza uamuzi huo leo (Desemba 17, 2021) na kueleza kuwa Polepole anatuhumiwa kurusha maudhui yenye kupotosha umma na yanayoweza kuchochea wananchi wa Tanzania kugomea na kudhoofisha kampeni ya kitaifa ya kujikinga na virusi vya Corona kwa madai kuwa virusi hivyo vimetengenezwa maabara.
Pia Polepole anatuhumiwa katika kipindi hicho kwa nyakati tofauti alipotosha kuhusu zoezi la Serikali la kuwapanga wafanyabiashara wadogo (wamachinga) kuwa wakuu wa mikoa hakufuata utaratibu na deni la Taifa bila kufuata sheria, misingi na kanuni za huduma ya utangazaji.
Kamati hiyo imesema maudhui hayo yanakiuka Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta za mwaka 2018.
Gunze amesema pia waendeshaji wa kipindi hicho hawana taaluma ya uandishi wa habari hivyo kupunguza ufanisi na kutozalisha maudhui yenye tija kwenye jamii.
“Kipindi cha Shule ya Uongozi cha Humphrey Polepole Online Tv kinaamriwa kusimamishwa kwa muda hadi mmiliki atakapohakikisha anakuwa na wafanyakazi wenye taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji ili kuleta ufanisi na tija katika vipindi vyake,
“Pili kuhakikisha vipindi vyake vyote vinazingatia sheria, kanuni, misingi na maadili ya uandishi na utangazaji wa habari na leseni yake,” amesema Gunze.
Zinazohusiana:
- LHRC yazungumzia adhabu ya vituo vitatu vya televisheni mtandaoni.
- TCRA yakusudia kusimamisha leseni za DSTV na Zuku.
- CCM yazidi kuongeza umiliki wa vyombo vya habari Tanzania
Baada ya kutekeleza maelezo hayo kipindi cha Humphrey Polepole Online kitatakiwa kutoa taarifa TCRA kuwa maelekezo yote yamezingatiwa na kuwa kipindi kitarejea chini ya uangalizi wa TCRA kwa miezi sita na kutoa onyo kali kwa kituo husika kwa aina ya maudhui ambayo kimeyatoa.
Hata hivyo, Polepole ana haki ya kukata rufaa ndani ya siku 21 iwapo hajaridhika na uamuzi huo.
Kipindi cha Polepole kinakuwa miongoni mwa radio na televisheni mbalimbali zilizofungiwa mwaka huu ikiwemo Wasafi TV iliyofungiwa miezi sita Januari 2021 kwa kukiuka kanuni za utangazaji.
Polepole ajibu mapigo
Muda mfupi baada ya kufungiwa kipindi chake, Polepole amesema anaishukuru Kamati ya Maudhui ya TCRA kwa kukamilisha zoezi hilo kwa sababu alipata nafasi ya kusikilizwa na leo hukumu imetolewa.
“Kazi ya kusema kweli ina safari, ina safari kidogo na ninadhani kwa mimi ambaye ni mwanachama wa CCM kwa imani, ninayeamini katika kusema kweli daima bila kuweka chembe ya fitina.
“Mimi ninayeamini katika ahadi nyingine ya CCM, nitatumia elimu yangu kwa faida ya wote, kwangu mimi hii ni mitihani midogo, nitakaa na wasaidizi wangu, tutatafakari kisha nitawajulisha.
Amesema kazi ya kusema kweli bado ina safari na hatakata tamaa, maadamu anachokifanya kinalinda maslahi mapana ya nchi na chama chake.
Latest
