Rais Samia: Vyombo habari mlivyovifungia, vifungulieni
- Ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa.
- Avitaka vyombo vya habari kuhakikisha vinafuata sheria na kanuni zilizowekwa na Serikali.
Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuvifungulia vyombo vya habari vilivyofungiwa, na kuhakikisha vinafuata sheria na kanuni zilizowekwa ili isionekane Serikali inaminya uhuru wa vyombo vya habari.
Rais Samia, aliyekuwa akizungumza leo Aprili 6, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kuwaapisha makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu, amesema licha ya kufunguliwa kwa vyombo hivyo vihakikishe vinafuata sheria za Serikali.
“Nasikia kuna viji vyombo vya habari huko mlivifungia si vijiTV vya mkononi vile vifungulieni lakini wafuate sheria na miongozo ya Serikali. Tusiwape mdomo wa kusema tunaminya uhuru wa vyombo vya habari,” amesema Rais Samia.
Aidha, ameagiza sheria, kanuni na adhabu ziwe wazi, makosa na adhabu zake zifahamike lakini siyo kuvifungia vyombo kwa ubabe bila kufuata taratibu zilizowekwa.
“…Lakini muhakikishe kila mliyempa ruhusa ya kuendesha chombo cha habari anafuata sheria za Serikali na kanuni ziwe wazi, kosa hili adhabu yake ni hii na mnakwenda kwa adhabu mlizoziweka kwenye kanuni tusifungie tu kibabe,” amesisitiza Mama Samia.
Zinazohusiana:
- LHRC yazungumzia adhabu ya vituo vitatu vya televisheni mtandaoni.
- TCRA yakusudia kusimamisha leseni za DSTV na Zuku.
- CCM yazidi kuongeza umiliki wa vyombo vya habari Tanzania
Huenda tamko hilo la Rais wa sita wa Tanzania, Mama Samia likafungua ukurasa mpya kwa utendaji wa vyombo vya habari na kuongeza wigo wa upashanaji habari nchini.
Kwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita baadhi ya vyombo mbalimbali vya habari yakiwemo magazeti na televisheni za mtandaoni vilisitishiwa leseni za uchapaji na usambazaji kabisa na kwa muda na vingine kutakiwa kuomba upya leseni kwa kile kilichodaiwa kukiuka sheria za Serikali.
Miongoni mwa vyombo vya habari vilivyofungiwa miezi ya hivi karibuni ni gazeti la Tanzania Daima na televisheni ya mtandaoni ya Kwanza TV.
Latest