Ahueni: Mfumuko wa bei washuka Tanzania
- Umeshuka hadi kufikia asilimia 4 kwa mwaka ulioishia Januari 2022 kutoka asilimia 4.2 iliyorekodiwa Desemba mwaka jana.
- Umechagizwa zaidi na kupungua kwa gharama za bidhaa zisizo za vyakula.
Dar es Salaam. Kasi ya mfumuko wa bei za bidhaa na huduma nchini Tanzania imeshuka hadi kufikia asilimia 4 kwa mwaka ulioishia Januari 2022 kutoka asilimia 4.2 iliyorekodiwa Desemba mwaka jana, ikichagizwa zaidi na kupungua kwa gharama za bidhaa zisizo za vyakula.
Kushuka kwa mfumuko wa bei kumekuja baada ya kupanda mfululizo tangu Septemba mwaka 2021.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Taarifa ya mfumuko wa bei ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) iliyotolewa leo (Februari 8, 2022) imesema hali hiyo imechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei wa baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Januari mwaka huu ikilinganishwa na kipindi cha mwaka ulioishia mwezi Desemba, 2021.
Mfumuko wa Bei ambao haujumuishi bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwezi Januari 2022 umepungua hadi asilimia 3.1 kutoka asilimia 3.9 ilivyokuwa kwa mwaka ulioshia mwezi Desemba, 2021.
Zinazohusiana: Mfumuko wa bei wang’ang’ania kiwango cha Januari
NBS imesema mfumuko wa bei ambao haujumuishi vyakula visivyochakatwa, nishati na bili za maji (Core inflation) umepungua pia hadi asilimia 3.3 kutoka asilimia 4.6 ilivyokuwa mwezi DESEMBA mwaka jana.
“Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kushuka kwa mfumuko wa bei ni mavazi kutoka asilimia 4.5 hadi asilimia 2.8, viatu (kutoka asilimia 4.6 hadi asilimia 4.4); na kodi ya pango kutoka asilimia 4.4 hadi asilimia 1.2.
Bidhaa nyingine ni magodoro kutoka asilimia 12.3 hadi asilimia 7.3, majokofu (kutoka asilimia 4.2 hadi asilimia 1.5); cherehani (kutoka asilimia 9.1 hadi asilimia 5.0); simu janja (kutoka asilimia 3.5 hadi asilimia 3.3); vyombo vya nyumbani kama sahani (kutoka asilimia 16.7 hadi asilimia 3.6); luninga (kutoka asilimia 3.5 hadi asilimia 1.2) na malazi kwenye hoteli na nyumba za kulala wageni kutoka asilimia 6.6 hadi asilimia 2.9.

Mfumuko wa bei Afrika Mashariki
Nchini Uganda. mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Januari 2022 umepungua hadi asilimia 2.7 kutoka asilimia 2.9 kwa mwaka ulioishia Desemba, 2021.
Kwa upande wa Kenya, mfumuko wa bei umepungua had asilimia 5.4 kutoka asilimia 5.7.
Latest
