Kasi ya mfumuko wa bei yashuka kwa mara ya tatu Tanzania
- Tangu Februari mwaka huu, mfumuko wa bei umekuwa ukishuka mfululizo.
- Umefikia asilimia 4.3 kwa mwaka unaoishia Aprili 2023.
Dar es Salaam. Huenda Watanzania wakaanza kupata ahueni ya ukali wa gharama za maisha baada ya kasi ya mfumuko wa bei kushuka hadi asilimia 4.3 kwa mwaka unaoishia Aprili 2023.
Mfumuko wa bei wa Taifa hupima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) katika taarifa yake ya Mei 8, 2023 imeeleza kuwa mfumuko wa bei kwa Aprili 2023 umeshuka kutoka asilimia 4.7 iliyorekodiwa mwaka unaoishia Machi 2023.
Tangu Februari mwaka huu, mfumuko wa bei umekuwa ukishuka mfululizo, jambo linaloashiria kuwa bei za bidhaa mbalimbali zimeanza kushuka ikilinganishwa na robo ya nne ya mwaka 2022.

“Hii inamaanisha kuwa, kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili 2023 imepungua ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2023,” imeeleza taarifa ya NBS.
Kupungua kwa mfumuko wa bei wa Taifa kumechangiwa na kupungua kwa mfumuko wa bei kwa baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi cha mwaka ulioishia Aprili, 2023 ikilinganishwa na kipindi cha mwaka ulioishia Machi, 2023.
Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei ni pamoja na mchele kutoka asilimia 32 hadi asilimia 31.2, mahindi (kutoka asilimia 50.9 hadi asilimia 44.8) na unga wa ngano kutoka asilimia 16.1 hadi asilimia 7.5).
Mfumuko wa bei ya unga wa mtama umeshuka kutoka asilimia 5.6 hadi asilimia 5.3), unga wa mahindi (kutoka asilimia 48.9 hadi asilimia 48.0), spageti/tambi (kutoka asilimia 2.1 hadi asilimia 1.3) na nyama ya ng’ombe (kutoka asilimia -4.7 hadi asilimia -6.0) na nyama ya kuku kutoka asilimia 4.6 hadi asilimia 4.5.
Bidhaa nyingine ambazo mfumuko wa bei umeshuka ni mafuta ya kupikia chakula kutoka asilimia -6.3 hadi asilimia -14.4, matunda (kutoka asilimia 7.4 hadi asilimia 6.7), karanga mbichi (kutoka asilimia 15.6 hadi asilimia 13.4), viazi vitamu (kutoka asilimia 7.8 hadi asilimia 2.0), maharagwe (kutoka asilimia 30.5 hadi asilimia 29.9), choroko kavu (kutoka asilimia 5.2 hadi asilimia 1.0) na vinywaji visivyo na kilevi kama soda na maji kutoka asilimia 7.5 hadi asilimia 4.4.
Baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoonesha kupungua kwa mfumuko wa bei ni vitambaa vya nguo kutoka asilimia 0.9 hadi asilimia -0.1, kitenge (kutoka asilimia 2.6 hadi asilimia 2.2), viatu vya watoto (kutoka asilimia 2.6 hadi asilimia 2.5) na bidhaa kwa ajili ya ukarabati wa nyumba mf. mabati na saruji kutoka asilimia 4 hadi asilimia 3.4.
Mfumuko wa bei ya gesi umeshuka kutoka asilimia 9 hadi asilimia 8.3, mafuta ya taa (kutoka asilimia 36.6 hadi asilimia 12.3), mkaa (kutoka asilimia -8.3 hadi asilimia -8.9), dizeli (kutoka asilimia 23.2 hadi asilimia 1.4) na petroli kutoka asilimia 7.6 hadi asilimia -9.3.
“Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Aorili 2023 umepungua hadi asilimia 9.1 kutoka asilimia 9.7 kwa mwaka ulioishia mwezi Machi, 2023,” imeeleza NBS.
Hali ya Afrika Mashariki
Nchini Uganda, mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Aprili 2023 umepungua hadi asilimia 8 kutoka asilimia 9 kwa mwaka ulioishia Machi, 2023. Kwa Kenya, mfumuko wa bei umepungua hadi asilimia 7.9 kutoka asilimia 9.2.
Latest