Ripoti: 46% ya wanawake Tanzania wakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi
- Sababu zikiwa ni kujikita zaidi katika shughuli zenye tija ndogo na upatikanaji mdogo wa mitaji.
Dar es Salaam. Serikali na wadau wa maendeleo huenda wakatakiwa kuongeza nguvu katika kuwawezesha wanawake kiuchumi, baada ya ripoti mpya kubaini bado wanakabiliwa na vikwazo vinavyopunguza tija ya shughuli zao.
Ripoti mpya ya hali ya uchumi Tanzania ya Septemba 2026 inayottolewa na Benki ya Dunia (WB) inabainisha kuwa karibu nusu ya kundi hilo bado llinakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi.
“Mwenendo kama huo unaonekana pia katika biashara ndogo zinazoongozwa na wanawake, ambazo zina uzalishaji kwa wastani ulio chini kwa asilimia 46 ikilinganishwa na biashara zinazoendeshwa na wanaume,” inaeleza ripoti ya Benki ya Dunia.

Ripoti inaeleza kuwa pengo hilo linahusishwa na sababu mbalimbali, ikiwemo wanawake kujikita zaidi katika shughuli zenye tija ndogo, upatikanaji mdogo wa mitaji na mapato madogo yatokanayo na mali.
Pamoja sababu hizo Benki ya Dunia pia imeutaja mzigo wa malezi kuwa mingon mwa sababu nyingine zinazozuia ukuaji wkaiuchumi wa wanawake.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wanawake hutumia takribani asilimia 14 ya muda wao katika kazi za nyumbani na malezi yasiyolipwa, zaidi ya mara tatu ya asilimia nne inayotumiwa na wanaume.
Hali hiyo inachangia kile Benki ya Dunia inachokiita umaskini wa muda ‘timely poverty’ ambapo majukumu mengi ya kifamilia huwaacha wanawake na muda mchache wa kushiriki katika shughuli zinazoweza kuongeza kipato na tija.
Wachambuzi waeleza suluhu
Nukta Habari imezungumza na wachambuzi wa masuala ya uchumi ili kujua hatua zinazopaswa kuchukuliwa kuwaondoa wanawake katika vikwazo vya kiuchumi vinavyowakabili.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Paul Chegula, anasema ili kuwaondoa wanawake katika vikwazo hivyo, ni muhimu kukabiliana na tamaduni zisizofaa, ikiwemo mfumo dume, huku Serikali ikiweka mazingira yenye fursa sawa katika maeneo mbalimbali.
“Kuweka fursa sawa upande wa Serikali katika maeneo mbalimbali, maeneo ya ajira, maeneo ya elimu na kadhalika. Kwamba hata kwenye upande wa ajira usiwe na vigezo, tuweke fursa sawa ili nao wakiweza kuingia kwenye soko la ajira wanaweza waka-boost uchumi wao,” amesema Paul.
Chegula ameongeza kuwa uwezeshaji wa wanawake hauwezi kutenganishwa na elimu, akisisitiza umuhimu wa familia kuwapa watoto wa kike fursa sawa za elimu kama watoto wa kiume.
“Kwenye eneo la elimu, wazazi, familia, mambo ya kusomesha mtoto wa kiume pekee zimeshapita. Tukiwawekea nguvu hawa wamama wana uwezo mkubwa sana wa kuweza kubadilisha jamii na hali za kiuchumi zao zitabadilika kabisa,” amesema.
Kwa upande wake, Dk Lenny Kasoga, mtaalamu wa uchumi kutoka Mwanza, akizungumzia namna majukumu ya malezi yanavyoweza kuwabana wanawake kiuchumi na kijamii, amesisitiza umuhimu wa kuanzisha mijadala ya kijamii kuhusu changamoto hizo.
“Kama jamii tuanze kuweka midahalo ambayo watu watapata kujadili, kwa sababu watu wengine sasa hivi hawana muda wa kujadili. Wanawake wanahangaika sana, maanake mwanamke hawezi kukataa kuwa mwanamke, maana anazaa, akishazaa lazima alee. Kitu ambacho kinabidi kiwekewe mkazo ili kijadiliwe na watu,” amesema.
Kasoga anasema mijadala hiyo inaweza kusaidia jamii kutafakari namna ya kupunguza mzigo wa majukumu ya malezi kwa wanawake na kuweka mazingira yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.