Umemejua unavyookoa maisha ya wajawazito Iringa
- Idadi ya wanawake kujifungua, watoto kupata chanjo yaongezeka.
- Wasaidia kuboresha huduma za uzazi Lupembe Lwa Senga.
Dar es Salaam. Baada ya kubanwa na uchungu mkali wa mwanawe wa kwanza, Sara Majolino (30) alilazimika kwenda zahanati iliyopo kijijini kwao akiwa na taa ya chemli ambayo ingesaidia kutoa nishati ya mwanga wakati wa kujifungua.
Kabla ya uamuzi wa kwenda zahanati, Sara, mkazi wa Kijiji cha Lupembe Lwa Senga kilichopo mkoani Iringa, alilazimika kuvumilia uchungu wa ujauzito wake kwa saa tatu ili kupisha kwanza giza lipite, akikusudia kuepuka madhara ambayo yangejitokeza iwapo angezalishwa gizani.
Hata hivyo, maumivu ya uchungu hayakuwa tayari kusubiri zaidi kiasi cha kumlazimu kwenda zahanati ya Lupembe Lwa Senga hivyo hivyo na giza.
“Ilikuwa mwaka 2013 uchungu ulinishika saa 8 usiku ila nilijikaza kwa sababu ilikuwa giza na mazingira ya zahanati hayaruhusu, kulikuwa hakuna umeme,” anasema Sara.
Sara amebaki na kumbukumbu isiyofutika maishani mwake juu alivyohatarisha maisha yake na mwanaye kutokana na zahanati yao kukosa umeme wakati huo.
Ukosefu wa nishati ya umeme ni miongoni mwa mambo yanayoathiri upatikanaji wa huduma za uzazi kwa wanawake wajawazito kijijini hapo na baadhi ya maeneo mengi nchini.
“Nilifika hapa mida ya saa 11 alfajiri, hata hivyo tulikuja na taa ya mafuta, ikabidi shangazi yangu aingie ndani wawe wanasaidiana na nesi wakati najifungua,” anabainisha Sara.
Zinazohusiana:Begi la umemejua: Mkombozi wa elimu Tanzania
Kwa mujibu wa Sara, ndugu wa mzazi anayejifungua huingia katika chumba cha uzazi kwa ajili ya kushika taa za chemli ili kuongeza mwanga utaowezesha shughuli ya uzazi kufanyika kwa ufasaha.
Sara ni sehemu ya watu bilioni moja wanaohudumiwa katika vituo vya afya visivyo na nishati ya kuaminika ya mwanga duniani, ambao ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) na Wakala wa Kimataifa wa Nishati Jadidifu (IRENA) inawataja kuwa wapo hatarini kupoteza maisha.
Tanzania ni miongoni mwa mataifa ambayo bado idadi ya vifo vya uzazi ni kubwa, hususan kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano ambapo Ripoti mpya ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania (THDS-MIS) kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa mwaka 2022 inaonesha kuna vifo 43 vya uzazi katika kila vizazi hai 1,000.
Hii ina maana katika kila watoto 100,000 wanaozaliwa 430 wanafariki wakiwa chini ya umri wa miaka mitano sawa na asilimia 4.3.
Hata hivyo, ripoti kama hiyo ya mwaka 2015/16 ilibainisha kuwa idadi ya vifo vya uzazi ni 556 katika kila vizazi hai 100,000.
Miongoni mwa sababu zinazochochea idadi hiyo ya vifo ni pamoja na ukosefu wa huduma bora za uzazi, ukosefu wa huduma za dharura ya uzazi, na sababu zitokanazo na uzazi kama vile kutokwa na damu baada ya kujifungua.
Ni historia isiyosahaulika
Kutokuwepo kwa nishati ya uhakika ya mwanga kijijini Lupembe Lwa Senga haukuwa mtihani kwa wanawake wajawazito pekee bali hata kwa wauguzi na wakunga wa zahanati ya kijiji hicho, kilichopo umbali wa zaidi ya kilomita 80 kutoka Iringa mjini.
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Lupembe Lwa Senga, Dk. Evelyn Kadeghe anakumbuka jinsi alivyokuwa anazalisha akiwa kwenye mwanga hafifu wa tochi ya simu au taa ya chemli jambo lililokuwa linamzuia kufanya kazi yake kwa ufanisi.
“Unakuta simu yenyewe umebana mdomoni, mikononi umevaa glavu, kweli ilikuwa inachosha, hii ni changamoto ambayo huwezi kumsimulia mtu…
…saa nyingine mama ‘anableed’ (anavuja damu), unashindwa kumjali mtoto unakimbilia mama, mtoto naye anatakiwa afunikwe, kutolewa hewa, bila mwanga mambo hayaendi hasa chumba cha leba (uzazi),” amesema Dk Kadeghe.
Hata mara baada ya umeme unaosambazwa na Wakala wa Umeme Vijijini Rea) kuwasili kijijini hapo, bado haukuwa mkombozi wa kutosha kwa kuwa hukatika kwa saa 12 hadi siku mbili.
Hali hii huathiri shughuli za uzazi kwa kuwa kwa kawaida mzazi aliyejifungua anatakiwa kuwa chini ya uangalizi kwa saa 24 ambapo uwepo wa mwanga husaidia kugundua changamoto yoyote kwa mzazi au mtoto.
Umemejua suluhu ya kudumu
Kutokana na zahanati hiyo kukosa nishati ya uhakika ya mwanga na kwa ajili ya kutunzia vifaa tiba, mwaka 2020 wadau wa nishati wakiongozwa na Shirika lisilo la kiserikali la Elico Foundation walijitosa kuhakikisha huduma hiyo inapatikana ili wazazi na watoto wanaozaliwa wawe salama.
Elico Foundation hujihusisha na usambazaji wa nishati ya umeme vijijini ambapo kwa kushirikiana na wadau wengine kama Mott Foundation, walifanikiwa kufunga miundombinu ya umemejua inayosaidia kuendesha shughuli mbalimbali katika zahanati hiyo ikiwemo za uzazi kwa saa 24.
Uhakika wa nishati ya umeme ulimfanya Sara Majolino kurejea tena kujifungua mtoto wa tatu katika kituo kile kile cha afya mara baada ya miaka 10 kupita, safari hii akiwa hana wasiwasi na bila kubeba taa ya chemli.
“Mwaka huu uchungu ulianza kama saa 11 jioni, nashukuru Mungu nilijifungua salama lakini tofauti na mwanzo sasa hivi nilivyojifungua nililala hospitali kwa saa 24 kutokana na uwepo wa mwanga,” anasema Sara.
Simulizi ya Sara haitofautiani sana na ya Editha Mhaluka (33) mama wa watoto watano. Watoto wawili wa Editha kati yao amejifungulia katika kituo hicho cha afya, akikiri uwepo wa mabadiliko makubwa ya huduma ambapo kwa sasa wanahudumiwa haraka na kwa urahisi tofauti na awali.
“Sasa hivi tukifika kweupe, wahudumu wanatuhudia kirahisi kwa kweli tunanufaika nao sana huu umeme” anasema Editha.
Kutokana na uwepo wa nishati ya uhakika ya mwanga unaotokana na umemejua idadi ya wazazi wanaojifungua katika kituo hicho imeongezeka tofauti na awali kabla ya kufungwa kwa mitambo ya umemejua.
Dk.Evelyn anasema kwa sasa zahanati hiyo inaweza kuzalisha wanawake nane mpaka 12 kutoka idadi ya wanawake wawili hadi wanne kwa mwezi pamoja na kuhudumia wagonjwa 50 hadi 70 kutoka ndani na nje ya kijiji cha Lupembe Lwa Senga.
Nishati ya umemejua inasaidia kuendesha vifaa vya umeme ikiwemo jokofu linalotumika kuhifadhi chanjo na daw ambalimbali zinazotakiwa kuhifadhiwa kwenye ubaridi. Pichal Esau Ng’umbi/Nukta
Huduma za chanjo kwa watoto zaimarika
Mbali na huduma za mama na mtoto kuimarika, uwepo wa nishati ya uhakika ya umeme umechochea kuimarika kwa huduma za utoaji chanjo kwa watoto ambazo awali zilikuwa zinasuasua kutokana na kutokuwepo kwa miundombinu ya kuhifadhi.
Kawaida chanjo za binadamu na mifugo huhifadhiwa katika sehemu yenye ubaridi kuanzia nyuzi joto 2 hadi 8 ili kutunza uwezo wake wa kufanya kazi.
Dk. Evelyn ameiambia Nukta Habari kuwa awali zahanati hiyo ilikuwa na jokofu ambalo lilitumika kuhifadhi chanjo lakini kutokana na umeme wa Rea kukatika mara kwa mara walilazimika kusafiri umbali mrefu ili kuhifadhi chanjo hizo.
“Mwanzoni ilikuwa inatugharimu muda na pesa, kufuata chanjo mjini na kuzirudisha siku tayari imeisha na hapo lazima utumie zaidi ya Sh6,000 kama utapanda basi hii ilikuwa inasababisha baadhi ya watoto wasimalize chanjo,” anasema Dk. Madeghe.
Soma zaidi:Ugonjwa wa kipindupindu waripotiwa Kagera, wanne wafariki
Tangu wafungiwe umemejua katika zahanati hiyo sasa wanaweza kuhifadhi chanjo na kuwachanja watoto zaidi ya 140 kwa mwezi kwa kuwa zinapatikana muda wowote zinapohitajika kutoka watoto chini ya 120 kwa mwezi hapo awali.
Wadau wanasema upatikanaji wa nishati ya uhakika katika maeneo ya huduma za jamii kama hospitali utasaidia kuchagiza maendeleo nchini hususan katika maeneo ya pembezoni.
Mkurugenzi wa Elico, Sisty Basil anasema malengo ya shirika hilo ni kushirikiana na Serikali kusambaza huduma ya nishati jadidifu katika maeneo ya vijijini na kwa sasa wanatekeleza miradi katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Arusha, Singida na Morogoro.