Ifahamu mikoa mitano yenye ATM chache zaidi Tanzania 

July 30, 2026 12:03 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni Simiyu, Songwe, Rukwa, Pemba na Katavi. 
  • Idadi ya matawi na mawakala wa benki inaongezeka.
  • Watalamu wa uchumi wasema kupungua kwa ATM si habari mbaya.

Dar es Salaam. Miaka mitano iliyopita, benki kuwa na mashine za kutolea pesa (ATM) ilikuwa kama alama ya maendeleo kwaa sekta ya fedha nchini.

Kadiri benki zilivyopanua matawi yake, ndivyo zilivyoongeza ATM ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Lakini picha hiyo inaanza kubadilika.

Ndani ya miaka mitano iliyopita, kwa mujibu wa Ripoti ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha mwaka 2025 iliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), idadi ya ATM imepungua huku idadi ya matawi, mawakala wa benki na simu pesa ikiongezeka. 

Ripoti hiyo inabainisha kuwa idadi ya ATM ilipungua kutoka 2,174 mwaka 2024 hadi 1,981 mwaka 2025. Hiyo ni sawa na upungufu wa mashine 193 au asilimia 8.9 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja.

Kupungua kwa ATM, huenda kunaashiria jambo jipya katika sekta ya benki, ikizingatiwa kuwa mashine hizo zimekuwa zikiongezeka mfululizo tangu mwaka 2021 kabla hazijanza kupungua 2023. 

Ripoti ya BoT inaonyesha kuwa mwaka 2021 kulikuwa na ATM 1,410 ambapo ziliongezeka hadi 1,911 mwaka uliofuata. Na mwaka 2023 zilifikia 2,209 kabla hazijaanza kushuka mwaka 2024 na 2025. 

Ripoti hiyo inaonesha kuwa Pemba ndiyo eneo lenye idadi ndogo zaidi ya ATM Tanzania ikiwa na ATM nane pekee hadi mwaka 2025, ikilinganishwa na 10 za 2021.

Kwa baadhi ya wakazi wa Pemba, changamoto si uwepo wa ATM pekee bali gharama ya kuzifikia. 

Mkazi wa Kisiwa cha Pemba kilichopo Zanzibar, Khaulat Rashid anasema kufuata huduma ya ATM humgharimu kati ya Sh1,000 na Sh1,600 kwa usafiri wa gari, hali inayomfanya kuona huduma za kidijitali kama njia rahisi na yenye gharama nafuu zaidi ya kufanya miamala ya kifedha. 

Mikoa mingine iliyokuwa na ATM chache 2025 ni pamoja na Katavi yenye ATM 11, ikifuatiwa na Simiyu na Songwe (ATM 14 kila mmoja), huku Rukwa ikiwa na ATM 16.

Licha ya Katavi kuwa miongoni mwa mikoa 10 yenye ATM chache zaidi, ina mafanikio kwa sababu zimekuwa zikiongezeka. Mwaka 2021 ilikuwa na ATM sita tu lakini mwaka jana zimeongezeka hadi 11 sawa na ongezeko la asilimia 83.3 ndani ya kipindi cha miaka mitano. 

Dar bado kinara wa ATM

Wakati Pemba ikiwa na ATM nane pekee, Dar es Salaam inaendelea kuwa kitovu cha huduma za ATM nchini.

Mkoa huo wenye idadi kubwa ya watu ulikuwa na ATM 650 hadi 2025, ikiwa ni karibu theluthi moja ya ATM zote zilizopo Tanzania na mara 81 ya ATM zilizokuwepo Pemba.

Wakati ATM zikipungua, mawakala na matawi ya benki yanaongezeka, jambo linaloashiria ukuaji wa huduma za benki kwa njia simu za mkononi hasa zilizounganishwa na intaneti. 

BoT inaeleza kuwa mawakala wa benki 187,692 walisajiliwa nchini 2025 kutoka mawakala 145,450 mwaka 2024. Hilo ni ongezeko la asilimia 29.1 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja. 

Mikoa iliyokuwa mawakala wengi wa benki ni pamoja na Dar es Salaam kwa asilimia 30, Mwanza (asilimia 7.3), Arusha (asilimia 7.0), Dodoma (asilimia 5.1), huku Mbeya ikiwa na asilimia 4.9. 

Hata hivyo, kufikia Desemba 2025, idadi ya matawi ya benki iliongezeka kufikia matawi 1,049 kutoka matawi 1,028 yaliyorekodiwa mwaka uliotangulia. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hadi kufikia Desemba 2025, Tanzania ilikuwa na benki 42 zikipungua kutoka 46 za 2021.  

Kupungua kwa ATM ni habari mbaya?

Licha ya takwimu kuonyesha kupungua kwa ATM mwaka mmoja uliopita, wachambuzi wa masuala ya fedha wanaeleza kuwa hali hiyo ni sehemu ya mageuzi katika sekta ya benki hasa matumizi ya huduma za kidijitali kwa njia ya simu.  

Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) Prof Abel Kinyondo anasema Tanzania imefikia hatua ambayo mawakala wa benki na huduma za fedha kwa njia ya simu zinaweza kutoa karibu huduma zote zilizokuwa zikifanywa na ATM.

“Kwa muktadha wa Tanzania, kupungua kwa ATM si tatizo kwa sababu tuna mfumo mpana wa mawakala wa benki na huduma za kidijitali. Kwa mteja ni rahisi zaidi kwenda kwa wakala aliyepo karibu kuliko kusafiri hadi ilipo ATM,” anasema Prof Kinyondo.

Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, benki pia zinaokoa gharama kubwa kwa kutumia mawakala kuliko kuwekeza kwenye ATM ambazo zinahitaji matengenezo, ulinzi na usimamizi wa karibu.

“Wakala anafanya kazi ile ile inayofanywa na ATM lakini kwa gharama ndogo zaidi kwa benki na kwa urahisi mkubwa zaidi kwa mteja,” ameongeza Prof Kinyondo.

Anasema mawakala pia hunachochea ajira kwa kuwa kila wakala ni fursa mpya ya biashara na kipato kwa wananchi.

Mtaalam huyo anaonya kuwa mjadala haupaswi kujikita katika idadi ya ATM pekee bali gharama za huduma za kifedha zinazotozwa na benki wakati watu wakifanya miamala kwa njia ya kidijitali.

“Changamoto kubwa si ATM. Changamoto ni gharama za huduma za kifedha. Hapo ndipo Benki Kuu na Serikali wanapaswa kuelekeza nguvu ili wananchi wengi zaidi waweze kutumia huduma rasmi za fedha kwa gharama nafuu,” anafafanua Prof Kinyondo.

Ripoti ya Ujumuishi wa Fedha ya BoT ya mwaka 2023 pamoja na ripoti ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya BoT ya mwaka 2024, zinaeleza kuwa ukuaji wa huduma za kidijitali, ongezeko la matumizi ya malipo ya kielektroniki na upanuzi wa mitandao ya mawakala ni njia muhimu wa benki kuwafikia wananchi wengi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Masoko & Zaidi
Loading…
No recent matches
No upcoming matches
/
No matches found for this filter
30 Jul, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
30 Jul, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
30 Jul, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
Vodacom Tanzania yapendekeza gawio la Sh23.91 kwa hisa 2026

Vodacom Tanzania yapendekeza gawio la Sh23.91 kwa hisa 2026

Nukta TV

Fursa kwa wakulima, uhitaji mazao ya chakula ukiongezeka Kenya, Uganda

Fursa kwa wakulima, uhitaji mazao ya chakula ukiongezeka Kenya, Uganda

Nukta TV

Jinsi afya ya akili inavyowatesa wanawake makazini

Jinsi afya ya akili inavyowatesa wanawake makazini

Nukta TV