Kuna nini mawakala wa benki kupungua baadhi ya mikoa Tanzania?
- Mikoa hiyo ni Rukwa, Shinyanga, Tabora, Ruvuma na Singida.
- Dar es Salaam yaongoza kuwa na mawakala wengi.
- Wachumi wasema hatua za haraka zichukuliwe kuimarisha huduma za kibenki nchini.
Dar es Salaam. Huenda ujumuishaji kifedha kwa wananchi wa baadhi ya mikoa nchini ukiwemo Rukwa ukachukua muda mrefu baada ya huduma za mawakala wa benki kupungua katika maeneo hayo.
Tangu kuanzishwa kwa huduma za mawakala wa benki nchini, kumepunguza changamoto ya watu kupanga foleni na kutumia muda mrefu kupata huduma za kifedha.
Hata hivyo, huenda hali hiyo ikajirudia kwa baadhi ya wananchi ambao katika maeneo yao huduma za kuweka na kutoa fedha kwa mawakala wa benki siyo za uhakika.
Ripoti ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha ya mwaka 2021 ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) iliyotolewa Septemba 13, 2022, inaonyesha kuongezeka idadi ya mawakala nchini kwa mwaka 2021 ambapo idadi hiyo imefikia 48,923 sawa na ongezeko la asilimia 21 ikilinganishwa na mwaka juzi.
Idadi hiyo ya mawakala imekuwa ikiongezeka tangu mwaka 2017, hali inayoonyesha matumaini mapya ya kupatikana kwa huduma hiyo nchini.
Huduma ya mwakala wa benki zinarahisisha kutuma na kutoa pesa kwa wananchi walio mbali na mashine za ATM au matawi ya benki. Picha | Daudi Mbapani.
Mawakala wapo wapi?
Licha ya idadi ya mawakala wa benki kuongezeka Tanzania mwaka mmoja uliopita, iko baadhi ya mikoa idadi hiyo imekuwa ikishuka, jambo linaloibua maswali mengi. Mikoa hiyo ni Rukwa, Shinyanga, Tabora, Ruvuma na Singida.
Ripoti hiyo ya BoT inaeleza kuwa Mkoa wa Rukwa ndiyo umeshuhudia kupungua kwa kasi kwa mawakala wa benki kuliko mikoa mingine ambayo imepata changamoto hiyo.
Mwaka jana mkoa huo ulikuwa na mawakala wa benki 180 ambapo idadi hiyo imeshuka kutoka mawakala 421 waliokuwepo mwaka 2020.
Hiyo ni sawa na upungufu wa mawakala 241 au sawa na asilimia 57.2 ya mawakala waliokuwepo mwaka juzi.
Anguko hilo la zaidi ya nusu ya mawakala ndani ya mwaka mmoja linaweza kuwa la ghafla kwa sababu miaka iliyotangulia, mawakala wa benki walikuwa wakiongezeka mfululizo mkoani humo.
Mathalan, BoT inaeleza katika ripoti hiyo kuwa kuanzia mwaka 2017 mpaka mwaka 2020 idadi ya mawakala mkoani humo ilikuwa ikiongezeka.

ATM nazo bado bado sana
Wakati Rukwa ikishuhudia kupungua kwa mawakala wa benki, pia haifanyi vizuri katika mashine za kutolea pesa (ATM) ambapo hadi 2021 mkoa huo ulikuwa na ATM 15 tu ambazo hazijaongezeka tangu mwaka 2020.
Mbali na Rukwa, mikoa mingine ambayo idadi ya mawakala imepungua mwaka mmoja uliopita ni pamoja na mkoa wa Tabora kwa asilimia 32.7 na kufikia mawakala 583, Ruvuma (asilimia 23) hadi mawakala 485.
Singida, mawakala wa benki walipungua kwa asilimia 18.7 kutoka mawakala 503 Mwaka juzi hadi kufikia mawakala 409 Mwaka 2021 huku Mkoa wa Shinyanga wakipungua kutoka mawakala 1026 .hadi mawakala 888.
Mikoa mingine ni kicheko
Wakati idadi ya mawakala ikipungua katika mikoa hiyo mitano, baadhi ya mikoa imeshuhudia kuongezeka kwa idadi ya mawakala kwa zaidi ya asilimia 50 kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Pemba yenye mikoa miwili ndiyo ilikuwa na kasi kubwa ya ongezeko la mawakala wa benki mwaka 2021 ambalo waliongezeka kwa asilimia 890 hadi kufikia mawakala 1,080 kutoka mwakala 100 waliokuwepo mwaka 2020.
Mkoa wa Simiyu nao mawakala wake waliongezeka hadi 1,202 kutoka mawakala 336 waliokuwepo mwaka 2020, ikifuatiwa na Katavi iliyokuwa na mawakala 204 kutoka mawakala 136 waliokuwepo mwaka juzi.
Hata wakati mikoa hiyo ikiongoza kwa kasi kubwa ya ongezeko la mawakala kwa mwaka 2021, Dar es Salaam ndiyo mkoa unaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya mawakala wa benki ambao walifikia 16,059 mwaka jana ikifuatiwa na Mkoa wa Arusha uliokuwa na mawakala 3,944.
Soma zaidi:
-
Mikoa mitano yenye ATM chache zaidi Tanzania
-
Benki Kuu yatoa maagizo kwa watoa huduma ndogo za fedha
Hii ina maanisha nini?
Dk Issack Safari Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) anasema kupungua kwa mawakala wa benki kwa baadhi ya mikoa nchini kunamaanisha bado baadhi ya mikoa haina uelewa juu ya faida za kutumia benki pia inaashiria maendeleo hafifu ya uchumi wa kipesa.
“Kuna baadhi ya wananchi hawaamini masuala ya kibenki wanaona kama wakiweka fedha zao benki baadhi ya kodi zitamaliza fedha zake, wengine wanahisi wakiweka fedha zao benki zinaweza kupotea” anasema Dk Safari.
Kuendelea kupungua kwa mawakala hawa pia kunamaanisha nguvu ndogo ya mabenki kuwashawishi wananchi kutumia huduma zao hali inayosababisha baadhi ya mawakala kukosa wateja na kufunga huduma.
“Kazi kubwa ya maagent (mawakala) ni kushawishi wananchi kutumia huduma za uwakala kama kutoa au kuweka pamoja na matumizi mengine, kama wameshindwa kufanya hii kazi hata benki wanaona hakuna haja ya kufanya nao kazi tena,” anasema Dk Safari.

Matokeo ya upungufu huu ni yapi?
Ikiwa huduma za mawakala wa kibenki zikiendelea kupungua mabenki yatakosa fedha za kujiendesha na kuwawezesha wananchi kwenye miradi mbalimbali kwa njia ya mikopo.
“Kama benki ikikosa fedha za kutosha kujiendesha ina maana itafunga lile tawi na kama benki ikifungwa italeta majanga makubwa ikiwemo wananchi kukosa mikopo,” anasema mtaalam huyo wa uchumi.
Ili kunusuru hali hiyo inayotishia ukuaji wa sekta ya benki nchini, Dk Safari ameshauri benki kuchukua hatua za haraka kuongeza elimu na ushawishi kwa wananchi watumie huduma za kibenki.
Latest