Bei mpya za mafuta Juni hizi hapa, dizeli yapaa kwa Sh85
- Lita moja ya dizeli kwa mwezi Juni itanunuliwa kwa Sh4,333 huku petroli ikinunuliwa kwa Sh4,086.
Arusha. Unaweza kusema ni maumivu juu ya maumivu kwa watumiaji wa vyombo vya moto vinavyotumia mafuta ya dizeli baada ya bei ya nishati hiyo kwa mwezi Juni kupaa kwa Sh85.
Ongezeko hilo litawafanya watumiaji wa nishati hiyo kupitia Bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi Juni kununua lita moja kwa Sh4,333 kutoka Sh4,248 iliyokuwa ikitumika mwezi Mei.
Maumivu hayo yatawafikia hata wale wanaotumia mafuta hayo kupitia Bandari ya Tanga ambao watanunua lita moja ya dizeli kwa Sh4,404 na Bandari ya Mtwara kwa Sh4,440.
Licha ya ongezeko hilo taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) iliyotolewa usiku wa kuamkia leo Juni 3, 2026 imesema Serikali imeweka ruzuku ya Sh534.91 kwa kila lita ya dizeli ili kupunguza maumivu.
“Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuhakikisha mafuta yanapatikana nchini muda wote na kuendelea kuhakikisha bei zinaendelea kuwa himilivu ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza ikiwemo zile za kiuchumi na kijamii. Miongoni mwa hatua hizo ni utoaji wa ruzuku ya takriban Shilingi 534.91 kwa kila lita moja ya mafuta ya dizeli,” imesema taarifa ya Ewura.
Ruzuku hiyo ya Serikali iliyoanza kutolewa mwezi Mei, imepaa kwa karibu mara mbili ya kiwango kilichopitishwa mwezi uliopita suala linaloleta ahueni kiduchu kwa watumiaji wa nishati hiyo.
Mwezi Mei, Sh259 ya ruzuku ilitengwa kwa kila lita ya dizeli iliyoongezeka kwa asilimia 100.3 ukilinganisha ile iliyotengwa kwa mwezi Juni.
Ruzuku hiyo imewekwa katika nishati hiyo kutokana na umuhimu wake katika shughuli za kiuchumi na kijamii zikiwemo uzalishaji viwandani, usafirishaji wa bidhaa na huduma za usafiri wa umma.
Hivi karibuni Serikali ilitangaza mpango wa kujenga vituo 10 vya Gesi Asilia Iliyoshinikizwa (CNG) kama miongoni mwa mikakati ya kukabiliana na kupaa huko kwa bei ya nishati.
Hata hivyo, wachambuzi wa uchumi walisema mpango huo unaweza usifanikiwe kwa kiasi kikubwa kutokana na utegemezi mkubwa uliopo katika mafuta ya dizeli katika vyombo vya usafiri wa umma na viwanda.
Ahueni kiduchu watumiaji wa petroli
Huenda watumiaji wa petroli wakapata ahueni kiduchu mwezi Juni 2026 baada ya bei ya mafuta hayo kushuka ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Kwa petroli inayopitia Bandari ya Dar es Salaam, mwezi huu inanunuliwa kwa Sh4,086 sawa na punguzo la Sh29 kutoka Sh4,115 iliyokuwa ikitumika mwezi uliopita.
Hata kwa watumiaji wa mafuta hayo kupitia Bandari ya Tanga watanunua mafuta hayo kwa Sh4,157 na Sh4,193 kwa yale yatakayopitiia Bandari ya Mtwara.