Sh1.61 trilioni kutekeleza vipaumbele 10 wizara ya afya Tanzania
- Wizara kuendeleza utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ngazi zote.
- Pamoja na kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.
Dar es Salaam. Wizara ya Afya imeomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh1.61 trilioni kwa mwaka 2025/26 kutekeleza vipaumbele 10 ikiwemo kufufua kiwanda kitakachozalisha dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi (ARV).
Katika mwaka huo wa fedha unaoanza Julai mwaka huu, Serikali imepanga kufufua kiwanda cha Tanzania Pharmaceutical Industries (TPI) kilichopo Arusha kwa lengo la kuanza uzalishaji wa ARVs ambazo ni muhimu katika kukabiliana na athari za Ukimwi.
Hatua hiyo ya Serikali huenda ikaisaidia Serikali kukabiliana na athari za uamuzi wa Marekani wa kusitisha misaada mwishoni mwa Januari ikiwemo ile ya Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa kukabiliana na Ukimwi (PEPFAR) inayohusu uimarishaji mapambano dhidi ya Ukimwi.
Bajeti ya mwaka 2025/26 imeongezeka kwa Sh306.35 bilioni sawa na asilimia 23.35 ukilinganisha na kiwango cha Sh1.31 trilioni kilichopitishwa na Bunge kwa mwaka 2024/25.

61% kugharamia miradi ya maendeleo
Waziri wa Afya, Jenista Mhagama, aliyekuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2025/26 bungeni Dodoma leo June 2, 2025 amesema asilimia 61 ya fedha hizo zitatumika kwenye miradi ya maendeleo.
“Mheshimiwa Spika, Wizara imepanga kutumia Sh991.75 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo sawa na asilimia 61 ya bajeti iliyotengwa,” amesema Waziri Mhagama.
Matumizi ya kawaida yanatarajiwa kuwa Sh626.43 bilioni sawa na asilimia 39 ya bajeti iliyotengwa ikiwa imepungua kwa asilimia 9 ukilinganisha na Sh632.2 bilioni za mwaka uliopita.
Katika bajeti ya matumizi ya kawaida, mishahara ya watumishi wa wizara na taasisi zilizo chini yake itanatarajiwa kuwa Sh475.41 bilioni wakati Sh151.01 bilioni zikitumika kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Wizara hiyo inatarajia kuwa kati ya fedha za maendeleo zilizopangwa mwaka huu, fedha za ndani ni Sh564.45 bilioni na kiasi cha Sh427.29 bilioni kinatarajiwa kutoka kwenye vyanzo vya nje.
Wizara hiyo inatarajia kukusanya mapato ya jumla ya Sh756 bilioni kutoka taasisi na hospitali zilizo chini yake, ikiwa ni ongezeko la asilimia 12 kutoka makusanyo ya mwaka uliopita.
Vipaumbele vingine vitakavyotekeleza katika mwaka huo wa fedha ni kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa ya kuambukiza yakiwemo magonjwa ya milipuko, magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, magonjwa yasiyoambukiza na huduma za lishe
Serikali hiyo ya Rais Samia Suluhu Hassan inatarajia kuimarisha upatikanaji na ubora wa huduma za afya zinazotolewa katika ngazi zote kuanzia zahanati hadi Taifa na kuimarisha mifumo ya ugharamiaji wa huduma za afya nchini ikiwa ni pamoja na kuendelea na utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote.
“Kuendelea kufanya tafiti na kuhimiza matumizi ya matokeo ya tafiti hizo kwa maeneo ya kimkakati pamoja na kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na watoto wachanga,” amesema Mhagama.
Vipaumbele vingine vinavyoangaziwa na Serikali ni kuimarisha upatikanaji na uendelezaji wa wataalam katika sekta ya afya kwa fani za kati, ubingwa na ubingwa bobezi na kuimarisha huduma za matibabu ya ubingwa na ubingwa bobezi pamoja na kuimarisha tiba utalii nchini.
Serikali kuendeleza tiba asilia
Mhagama ameeleza katika hotuba yake kuwa wizara itaendeleza na kusimamia afua za tiba asili na tiba mbadala na kuimarisha huduma za afya ya akili, huduma za utengamao hususan kwa watoto, wazee na watu wenye ulemavu.
Pamoja na mipango hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya Ukimwi, Elibariki Kingu ameeleza kuwa mwenendo wa upatikanaji wa fedha kwa miradi ya maendeleo ya wizara hiyo sio ya kuridhisha licha ya mwaka wa fedha kufikia ukingoni.
Kingu ameongeza kuwa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka 2024/2025 haujazingatia utoaji wa fedha zote zilizoidhinishwa, jambo linalokwamisha kukamilika kwa miradi ya maendeleo ya afya ambayo ni ya muhimu kwa ustawi wa jamii.
Latest



