Serikali: ARV zipo za kutosha
- Yawataka wananchi kupuuzia taarifa potofu za uhaba wa dawa hizo zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii.
- Wananchi watakiwa kuendelea kutumia dawa kama inavyoshauriwa na wataalamu wa afya.
Arusha. Serikali ya Tanzania imesema dawa za kufubaza Virusi Vya Ukimwi (ARV) zipo za kutosha nchini na wagonjwa hawatahitaji kununua dawa hizo kama taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii.
Taarifa ya Wizara ya Afya iliyotolewa leo Februari 8, 2024 imewahakikishia watumiaji wa dawa hizo kuwa zipo za kutosha na hazitatolewa kwa malipo kama baadhi ya taarifa potofu zinavyosema.
“Serikali kupitia Wizara ya Afya, inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI Haziuzwi na kwamba zipo za Kutosha…
…Watumiaji wa dawa hizi, hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu upatikanaji wa dawa hizi. Serikali kupitia Wizara inaendelea kuweka mikakati thabiti na stahiki ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida.” imesema taarifa ya Wizara ya Afya.
Ufafanuzi huo wa Wizara ya Afya unakuja ikiwa zimepita wiki mbili tangu Januari 20, 2025,Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) lilitangaze kusitisha msaada wake wa kimataifa kwa siku 90 ili kupitia na kuhakiki programu zake.
Kusitishwa kwa msaada hiyo kunagusa utendaji kazi wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR) anaohusika kufadhili huduma za matibabu ya ugonjwa wa Ukimwi ikiwemo utoaji wa ARV kwa waathirika.
Tangu kutolewa tangazo la kusitishwa kwa mfuko huo baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wamekuwa wakisambaza taarifa potofu kuwa huenda dawa hizo zitaanza kutolewa kwa malipo tofauti na ilivyokuwa awali.
Hata hivyo, siku chache zilizpita Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kuingizwa kwa PEPFAR katika orodha ya huduma za msaada wa kibinadamu zilizopata msamaha.
Tangazo hilo linaiweka Tanzania na nchi nyingine zinazotegemea ufadhili wa mfuko kwenye ahueni ikijihakikishia uhakika wa dawa licha ya Serikali kujidhatiti kukabiliana na uhaba wa dawa hizo kabla haujatokea.
“Dawa haziuzwi, tunazo za kutosha na zikipungua tutanunua zingine. Wananchi msiwe na hofu,” amesema Gerson Msigwa, Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Aidha, Wizara ya Afya imetoa rai kwa wananchi kupuuza taarifa hizi na kuendelea kutumia dawa kwa usahihi kama wanavyoelekezwa na wataalam wa afya ili kuzuia usugu wa vimelea vya magonjwa haya dhidi ya dawa.