Fahamu historia ya USAID Tanzania
- Ilianzishwa mwaka 1961 chini ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo John Kennedy.
- Tanzania ni miongoni mwa nchi za mwanzoni kupata msaada huo.
Arusha. Huenda umewahi kusikia kuhusu Shirika la Msaada wa Kimataifa ya Marekani (USAID) na jinsi linavyotoa misaada katika sekta mbalimbali nchini ikiwemo za afya.
Shirika hili limejizolea umaarufu tangu kuanzishwa kwake mwaka 1961 likizisaidia nchi za changa za Afrika zilizokuwa zimepata uhuru wakati huo kukuza uchumi.
Chini ya uongozi wa aliyekuwa Rais wa Marekani wakati huo John Kennedy USAID ilianza utekelezaji wa miradi yake mara moja ikianzia nchini Tanganyika (sasa Tanzania) na baadae kujitanua katika mataifa mengine ya Afrika ikiwemo Zambia, Malawi na Nigeria.
Kwa mujibu wa USAID msaada huo katika miaka ya mwanzo ya uhuru wa Tanganyika ililenga kuimarisha sekta ya elimu kwa kuanzisha vyuo kama Chuo cha Kilimo Morogoro (Sasa SUA), Chuo cha Utawala wa Umma, na vyuo vya mafunzo ya walimu Iringa na Dar es Salaam.
Mwaka 1964, baada ya Tanganyika kuungana na Zanzibar, miradi ilipanuka kujumuisha maendeleo ya jamii, uhifadhi wa mazingira, na miundombinu, ikiwemo barabara ya Tanzania-Zambia iliyokamilika 1973.
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/sxsss.png?resize=787%2C523&ssl=1)
‘Jifunze uelewe’ ni miongoni mwa miradi ya USAID nchini Tanzania uliowasaidia watoto zaidi ya milioni 1.4 katika shule za msingi 3,288 mwaka 2024 kuboresha ujuzi wao wa kusoma na kuhesabu.Picha|USAID/Instagram.
Kadri miaka ilivyoendelea, USAID ilipanua misaada yake kwa kujikita kwenye kilimo, afya, na miundombinu katika nchi nyingine za Afrika ikiwemo Kenya, Nigeria, na Ethiopia.
Miongoni mwa miradi ambayo USAID ilisaidia katika nchi hizo ni pamoja na kilimo inayolenga kuongeza uzalishaji wa chakula na kupunguza umaskini kupitia mpango wa Feed the Future.
Katika sekta ya afya, USAID ilihusika katika mapambano dhidi ya magonjwa kama UKIMWI, malaria, na kifua kikuu.
Kupitia Mfuko wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI (PEPFAR), USAID ilitoa misaada ya dawa, matibabu, na kampeni za kinga katika nchi nyingi za Afrika.
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/WhatsApp-Image-2025-02-04-at-18.36.11-Copy.webp?resize=1024%2C896&ssl=1)
Kusitishwa kwa USAID na kuanzishwa kwa mpango wa PEPFAR
Katika miaka ya 1980 na 1990, USAID ilisitisha msaada katika nchi za Afrika kwa muda, lakini ilirejea kwa nguvu mpya kwa kuimarisha afya vijijini, kupambana na UKIMWI,kupitia mpango wa dharura wa Rais wa Marekani wa kupambana na UKIMWI (PEPFAR) ulioanzishwa mwaka 2003.
Tangu kuanzishwa kwa mfuko huo Serikali ya Marekani imewekeza zaidi ya dola bilioni 100 katika juhudi za kimataifa za kupambana na VVU/UKIMWI, na hivyo kuokoa zaidi ya maisha ya watu milioni 25 duniani kote, kuzuia maambukizi mapya na kusaidia nchi kadhaa kudhibiti janga hilo huku ikichangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha usalama wa afya na uchumi wa dunia.
Miaka iliyofuatia USAID iliendelea kufadhili miradi mingine ya afya na maendeleo ikiwemo mpango wa kupambana na malaria ulioanza mwaka 2005, sekta ya kilimo kupitia mpango wa ‘Feed the Future’ uliosaidia wakulima 450,000 kupata mafunzo na masoko, miradi wa ‘Power Africa’, Let Girls Learn na mingine mingi.
Ripoti ya mpya AidData kwa kushirikiana na REPOA ya mwaka 2024 inabainisha kuwa mchango wa Marekani kupitia USD ni wastani wa Sh 1 bilioni lakini kuanzia mwaka 2012 hadi mwaka 2022 shirika hilo lilifadhili miradi yenye wastani wa Dola za Marekani bilioni 2.8 (sawa na Sh7.9 trillioni).
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/01.jpg?resize=1024%2C682&ssl=1)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (wa poli kulia) akizindua kampeni ya Afya yangu (2021-2026) inayofadhiliwa na USAID yenye lengo lakusaidia Serikali ya Tanzania kutoa huduma bora na jumuishi za kinga, matibabu, na huduma za utunzaji wa VVU na Kifua Kikuu (TB) ihususan kwa vijana na watoto.Picha|T-Mark Tnazania.
Ndani ya miaka hiyo sekta ya kilimo ilipata ufadhili wa Dola za Marekani 546 milioni), miundombinu (579 milioni), afya hususani katika mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI (3.8 bilioni) na malaria (533 milioni).
Hata hivyo, Januari 20, mwaka huu USAID lilitangaza kusitisha msaada wake wa kimataifa kwa siku 90 ili kupitia na kuhakiki programu zake.
Kusitishwa kwa msaada hiyo kunagusa mfuko wa PEPFAR anaohusika kufadhili huduma za matibabu ya ugonjwa wa Ukimwi ikiwemo utoaji wa ARV kwa waathirika.
Pamoja na sitisho hilo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Februari 3 mwaka huu ilitangaza kuingizwa kwa PEPFAR katika orodha ya huduma za msaada wa kibinadamu zilizopata msamaha.
Miongoni mwa shughuli zilizoruhusiwa ni pamoja na utunzaji wa watu wenye VVU kwa lengo la kuokoa maisha, upimaji ushauri, kuzuia na matibabu ya maambukizi ya kifua kikuu huduma za maabara, ununuzi na usambazaji wa bidhaa za afya na dawa.
PEPFAR imeruhusiwa kutoa huduma nyingine ikiwemo ya kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto na nyinginezo katika sekta ya afya.
Latest
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/VFLt5vHV7aCoLrLGjP9Qwm.jpg?fit=300%2C169&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/71f29364436954e34871d65ac6f43839-scaled.jpg?fit=300%2C200&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/images-96.jpeg?fit=300%2C157&ssl=1)
![](https://i0.wp.com/nukta.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/Gi21YlZXgAAxQ2l.jpg?fit=300%2C200&ssl=1)