Si kweli: Wizara ya Afya imetangaza bei mpya ya dawa za ARV
- Uchunguzi wa Nukta Fakti wabaini kuendelea kutolewa kwa dawa hizo kupitia mfuko wa PEPFAR.
Dar es Salaam. Wizara ya Afya ya Tanzania imekanusha taarifa inayosambaa mitandaoni kuwa imetangaza bei mpya ya dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV),
Taarifa hiyo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiiga muekano wa machapisho ya Millard Ayo, inasema kuwa dawa hizo kwa sasa zinauzwa Sh7,600, baada ya kusitishwa kwa msaada wa dawa hizo kutoka Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) jambo ambalo si kweli.
Wizara ya Afya kupitia akaunti yake ya Instagram, imethibitisha kuwa taarifa hizo si za kweli.
Ukweli ni huu
Januari 20, 2025,Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) lilitangaza kusitisha msaada wake wa kimataifa kwa siku 90 ili kupitia na kuhakiki programu zake.
Kusitishwa kwa msaada hiyo kunagusa utendaji kazi wa Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR) anaohusika kufadhili huduma za matibabu ya ugonjwa wa Ukimwi ikiwemo utaoaji wa ARV kwa waathirika.
Hata hivyo, siku chache zilizpita Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilitangaza kuingizwa kwa PEPFAR katika orodha ya huduma za msaada wa kibinadamu zilizopata msamaha.
Miongoni mwa shughuli zilizoruhusiwa ni pamoja na utunzaji wa watu wenye VVU kwa lengo la kuokoa maisha, upimaji ushauri, kuzuia na matibabu ya maambukizi ya kifua kikuu huduma za maabara, ununuzi na usambazaji wa bidhaa za afya na dawa.
Pamoja na hayo, PEPFAR imeruhusiwa kutoa huduma nyingine ikiwemo ya kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto hivyo taarifa hiyo ni potoshi.
Mbali na ufafanuzi huo, ukiangalia uandishi wa taarifa hii umekaa kimakosa hususani kwenye matumizi ya lugha za uandishi mfano kuna baadhi ya maneno kama KWASASA yameunganishwa, huku maneno mengine kama IMETTOA ikiwa na herufi zilizobebana.
Sio hivyo tu hata kiunganishi kilichowekwa ili kupata taarifa kamili haina kikoa cha Serikali ambacho hutumika katika taarifa za mara kwa mara.
Nukta Fakti inaendelea kuwasihi watu kuacha kusambaza taarifa zenye lengo la kupotosha jamii ili kuepusha madhara ambayo mtu anaweza kuyapata iwapo hatachunguza ukweli wa taarifa hiyo.