Wabunge waitaka Serikali kugharamia matibabu ya Ukimwi kwa fedha za ndani

February 4, 2025 5:20 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni baada ya kusitishwa kwa misaada kutoka kwa mashirika na taasisi za nje ya nchi ikiwemo PEPFAR.

Dar es Salaam. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Ukimwi imeitaka Serikali ya Tanzania kugharamia huduma stahiki kwa waathirika wa virusi vya Ukimwi, magonjwa ya ngono, na homa ya ini kwa kutumia mapato ya ndani. 

Mapendekezo hayo yametolewa ikiwa zimepita siku nane baada ya Marekani kusitisha misaada iliyokuwa ikitolewa kupitia Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) iliyokuwa ikisaidia Tanzania kugharamia huduma hizo.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk Elibariki Kingu aliyekuwa akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo leo Februari 4, 2025 bungeni, Dodoma amesema kuwa ufinyu wa fedha za ndani zilizotengwa kudhibiti ugonjwa huo unafifisha jitihada za kupamba na ugonjwa huo.

“Bunge lihakikishe kwamba taasisi zake zinatenga fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza mkakati wa kudhibiti maambukizi,” amesema Dk Kingu.

Kwa muda mrefu kiwango kikubwa cha fedha za utekelezaji wa afua za Ukimwi kama tohara za wanaume, kinga tiba, usambazi wa kondomu na elimu kuhusu maambukizi, zimekuwa zikitolewa na wafadhili mbalimbali kutoka nje ya nchi husasan Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na Ukimwi (PEPFAR).

Mathalan mwaka wa fedha 2024/25 Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS) imepanga kutumia Sh12.44 bilioni  fedha za nje zikiwa asilimia 84 huku asilimia 14 pekee zikiwa ni fedha ya ndani.

Dk Kingu amethibitisha kwamba, mchango wa mashirika ya kimataifa na yasiyo ya kiserikali umekuwa na manufaa makubwa kwa jamii na nchi kwa ujumla kama kupunguza maambukizi ya Ukimwi kufikia asilimia nne kwa mujibu wa Tanzania Health Impact Survey 2023 kutoka asilimia 5, 2016/17.

Mbali na kupunguza maambukizi mashirika hayo ya msaada ikiwemo PEPFAR yamesaidia kupunguza vifo vinavyosababishwa na Ukimwi huku zaidi ya watu milioni 1.7 wakipata huduma ya dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi bure.

Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum kutoka Tabora, Jacqueline Kainja (CCM) ameeleza umuhimu wa Serikali kuchukua hatua za haraka na za moja kwa moja kuhakikisha kuwa mpango wa utekelezaji wa kukamilisha afua za Ukimwi kama mfano, kuzuia maambukizi, kutoa matibabu, na kuelimisha jamii unafanywa kwa kutumia rasilimali za ndani ya nchi. 

“Ni wakati sasa wa Serikali kusimamia mpango wa utekelezaji wa kukamilisha afua za Ukimwi uliozindiliwa Disemba 1, 2024 ili kuhakikisha unatumia rasilimali za ndani ya nchi ili kuweza kudhibiti na kupambana na Ukimwi,” amesema Kainja.

Kulingana na Kingu, endapo changamoto zinazoikabili Tume ya Kudhibiti Ukimwi zitatatuliwa kwa ufasaha Tanzania itafikia lengo la kuzuia kabisa maambukizi mapya ya Ukimwi.

“Jitihada madhubuti zinahitajika katika mapambano dhidi ya Ukimwi, zikiwemo kutatua changamoto zilizobainika (utegemezi na ushirikiano dhaifu) wakati wa utekelezaji, utatuzi utaleta matokeo chanya ya moja kwa moja ikiwa ni pamoja na kutokomeza Ukimwi ifikapo 2023,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks