Wanne mahakamani kwa ubakaji, ulawiti binti wa Yombo
- Watuhumiwa wanne kusomewa mashtaka leo mahakamani.
- RPC Dodoma atenguliwa kwa kauli tata kuhusu mwenendo wa kesi.
Dar es Salaam. Watuhumiwa wanne kati ya sita waliokamatwa na Jeshi la Polisi kwa kuhusika na tukio la ukatili wa kijinsia dhidi ya binti baada ya video zilizosambaa mitandaoni na kuibua shinikizo kubwa kutoka kwa wananchi, watafikishwa mahakamani leo Agosti 19 ili kusomewa mashtaka.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na Jeshi la Polisi leo Agosti 19, 2024 imesema kuwa “tungependa kujulisha kuwa watuhumiwa wa kesi hiyo watafikishwa mahakamani kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.”
Hatua hii imefikiwa na Jeshi la Polisi baada ya kufanya uchunguzi wa kina kwa zaidi ya wiki mbili ambao hadi sasa umefanikisha kuwakamata watuhumiwa wanne pekee wanaofikishwa mahakamani huku wengine wawili wanaotajwa kuhusishwa na tukio hilo taarifa zao kutowekwa wazi.
Watuhumiwa wanaofikishwa mahakamani leo hii ni Clinton Honest Damas maarufu kama Nyundo, Praygod Edwin Mushi, Amini Lord Lema na Nickson Idala Jackson waliokamatwa Agosti 9, 2024 kwenye mikoa ya Dodoma na Pwani.
Hata hivyo, taarifa ya kufikishwa mahakamani kwa watuhumiwa hao imetolewa ikiambatana na kukanushwa kwa habari iliyochapishwa na gezeti la Mwananchi Agosti 18, 2024 yenye kichwa “RPC: ANAEDAIWA KUBAKWA NA KULAWITIWA ALIKUWA KAMA ANAJIUZA” na kuwaelezea watuhumiwa wa kesi hiyo kama walevi na wavuta bangi.
Habari hiyo imeibua mwitikio wa makundi tofauti yakionesha kutoridhishwa na majibu ya aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Dodoma RPC Theopista Mallya ambae taarifa ya Jeshi la Polisi inabainisha kuwa amehamishiwa makao makuu ya polisi Dodoma na nafasi yake kuchukuliwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) George Katabazi.
Wananchi kuweni na subira
Doroth Gwajima, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) amekiri kupokea maoni na maswali kuhusu hatima ya mwenendo wa shauri la kesi hiyo na kuwasihi wananchi kuwa na subira wakiamini haki itaonekana na itatendeka kwa mujibu wa sheria.
Kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Jinai, toleo la 2022, kifungu cha 131A. (1) kosa la ubakaji linapofanywa na kikundi cha watu, kila atakaekutwa na hatia atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha, bila kujali jukumu lake halisi kwenye ubakaji.
Pia kifungu cha 154 (1) kinabainisha kuwa mtuhumiwa akibainika kutenda makosa ya kinyume cha maumbile atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha na wakati mwingine kifungo kisichopungua miaka thelathini.
Latest