Polisi yaanza uchunguzi jaribio la utekaji Dar es Salaam

November 13, 2024 10:37 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Lasema watuhumiwa wa tukio hilo watakamatwa baada ya uchunguzi kukamilika.
  • Watumiaji wa mitandao ya kijamii walitaka jeshi hilo kupambana na matukio hayo yanayofananishwa na utekaji.

Arusha. Jeshi la Polisi limesema linachunguza  video iliyosambaa katika mitandao ya kijamii inayowaonyesha watu wawili wakijaribu kumkamata na kumwingiza kwa nguvu ndani ya gari mfanyabiashara anayejulikana kama Deogratius Tarimo.

Taarifa ya Jeshi la Polisi inakuja ikiwa ni saa chache baada ya picha hizo jongefu kusambaa katika  mitandao ya kijamii ikiwemo X zilimuonesha Tarimo akilazimishwa kuingia kwenye gari huku akipiga kelele za kuomba msaada kutokea katika Hoteli ya Rovenpic iliyopo eneo la Kiluvya Jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Tarimo aliwazidi nguvu watu hao na kufanikiwa kukimbia akiwa kifua wazi na pingu mkononi.

Msemaji wa Jeshi la Polisi David Misime katika taarifa yake iliyotolewa leo Novemba 13, 2024 amesema baada ya tukio hilo Tarimo alitoa taarifa katika kituo cha polisi Magogoni Dar es Salaam Novemba 11 mwaka huu.

“Kulingana na ushahidi uliowasilishwa kituoni hapo na yeye mwenyewe ni kwamba, chanzo cha tukio na kilicho msukuma kufika katika Hoteli ya Rovenpic iliyopo eneo la Kiluvya Jijini Dar es Salaam ni kufanya mazungumzo ya biashara ambayo amekuwa akiwasiliana kuifanya na aliokuwa anawasiliana nao toka Oktoba 25, 2024,”imesema taarifa hiyo

Aidha, Jeshi la Polisi limesema baada ya kukamilika kwa uchunguzi wa tukio litawakamata na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria watu hao waliohusika.

Baada ya kutolewa kwa taarifa hiyo baadhi ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii wamelitaka Jeshi hilo kushughulikia matukio hayo yanayofananishwa na utekaji ili kupunguza hofu kwa wananchi.

“Nina imani sana na jeshi langu la Tanzania, kwani mnatulinda raia na mali zetu, lakini kuna maswala mmekua mkituahidi wahusika watakamatwa lakini katika ili la kutekana mmeliweza kwa asilimia fulani tu hamjaweza kulitatua hofu ipo katikati yetu raia sana,” amesema  mtumiaji wa mtandao wa X anayetambulika kama Shirima Junior

“..Uhai ni zawadi toka kwa Mungu na yeye ndo mwenye haki na uhai wetu Tekelezeni wajibu wenu nasisi tutekeleze wajibu wetu,”amesema Maulid Meddy mtumiaji mwingine wa X .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks