Ni laana: Shinikizo lazidi kuwasaka waliombaka binti videoni

August 5, 2024 6:09 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Siku moja baada ya kusambaa video zinazoonyesha tukio la ubakaji dhidi ya binti mmoja anayedai kuwa ni mkazi wa Dar es Salaam, viongozi na watumiaji wa mitandao ya kijamii wamelaani vikali kitendo hicho wakitaka jeshi la polisi liwachukulie hatua kali waliohusika kukomesha vitendo hivyo. 

Tofauti na matukio mengine zinaposambaa picha au video za ngono mtandaoni, safari hii sehemu kubwa ya watumiaji wa mitandao ya kijamii wameonyesha kuchukizwa na kitendo hicho kilichofanywa na kundi la wanaume wasiopungua wanne wanaodaiwa kuwa ni askari. 

Jeshi la Polisi jana lilieleza kuwa limeanza kuwasaka wanaume hao huku wakionya watumiaji wa mitandao kusitisha kusambaza video hizo kwa kuwa ni kinyume cha sheria na zinaendelea kumdhalilisha na kumuumiza kisaikolojia binti huyo. 

Katika moja ya video hizo, binti huyo anajitambulisha kuwa anatokea Yombo Dovya shuleni jijini Dar es Salaam huku mmoja ya watuhumiwa hao akiuliza iwapo mwenzake ameanza kurekodi video. 

Video nyingine inaonyesha vijana wanne huku wawili kati yao wakifanya nae vitendo vya ngono. Mwingine wa tatu akimuamrisha binti huyo kutii wito wanaomuambia na wanne akishabikia kinachoendelea “akisubiria zamu” yake. Mtu wa tano aliyerekodi tukio hilo haonekani kwenye video. 

Pia wanaume hao wamesikika wakieleza kuwa wametekeleza kitendo hicho kwa maagizo ya kiongozi wao wakidai kuwa binti huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mume wa kiongozi wao.

‘Hatuwezi kuwa na taifa la wahalifu’

Tangu kuenea kwa video hizo kwenye mitandao ya kijamii, hususan X (zamani Twitter) na Instagram kumekuwa na shinikizo kubwa kwa viongozi wa juu wa nchi na vyombo vya ulinzi na usalama kufanya uchunguzi wa haraka na kuwakamata watuhumiwa hao.

Wakili mashuhuri nchini Peter Madeleka kupitia mtandao wa X amemtaka Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwapeleka mahakamani watuhumiwa hao ndani ya saa 24 na iwapo itashindikana kwa kisingizio chochote atajitolea kwa fedha zake kushughulikia kesi hiyo.

“Hatuwezi kuwa na taifa la kulinda wahalifu,” amesema Madeleka ambaye hivi karibuni alishinda tuzo ya wakili bora wa mwaka 2023-2024 aliyehudumia jamii.

Ni ukatili dhidi ya wanawake

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza kuwa kimehuzunishwa na ukatili huo na wanataka wahusika wote watano na aliyewatuma kulingana na maelezo wanakamatwa na kufikishwa mbele ya mkono wa sheria.

“Tunamuomba Rais wa Tanzania akiwa kama mama na amiri jeshi mkuu kutoka hadharani na kuonyesha kuchukizwa na jambo hili la udhalilishaji na ukatili juu ya mtoto wa kike akiwa kama mama mzazi na kiongozi mwenye dhamana ya kulinda raia wa Tanzania”. Amesema Anna Henga.

“Tukifumbia macho mambo haya yatazidi kujitokeza katika jamii yetu kwa mwamvuli wa watu kutumia nafasi zao kuumiza na kudhalilisha watu wengine,”  Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Anna Henga amewaambia wanahabari leo Agosti 5.

Tukio hili limeendelea kuonesha ukubwa wa tatizo la ukatili wa kijinsia na kuporomoka kwa maadili nchini ikiwemo matumizi mabaya ya Tehama. 

Baadhi ya watumiaji wa mtandao wameonekana kuchukizwa vikali kuendelea kusambazwa kwa video hizo ikiwa ni tofauti na miaka ya nyuma pale ambapo video hizo zilipokuwa zikisimbaa wengi walikuwa wakizitaka kama “connection”. 

‘Unayesambaza halijakukuta’

“Watu wapo ‘busy’ wanaomba video. Siku zaja utatumiwa ya mtu wako wa damu, mama, baba, kaka, dada, mtoto, mke, mume ndo utajua sio kila kitu lazima uone. Katili habishi hodi. Tujifunze kukataa kupokea na kutuma video, picha za udhalishaji,” amesema mtumiaji wa Instagram anayejulikana @Vickymic94_dagaanono. 

Kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya 2015 watumiaji wanapaswa kuepuka kusambaza picha ama video za utupu ama zisizo na maadili kwa jamii kupitia mitandao mbalimbali kama WhatsApp, Facebook, Youtube, Instagram ama X zamani ‘Twitter’. 

Adhabu ya uchapishaji wa ponograa ni faini isiyopungua milioni 20 au kifungo kisichopungua miaka 7 au vyote kwa pamoja. Ponograa chafu au ya kiasherati ni faini isiyopungua milioni 30 au kifungo kisichopungua miaka 10 au vyote kwa pamoja.

“Wakati tunaendelea kuwatafuta na kuwakamata waliofanya kitendo hicho cha kikatili kisichovumilika tutawakamata pia wataokiuka agizo hili na kuendelea kusambaza picha hizo” imeeleza taarifa kwa umma iliyotolewa na Jeshi la Polisi Agosti 4 mwaka huu.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk Dorothy Gwajima ameeleza kuwa tayari jeshi la polisi wanashughulikia kesi hiyo na kwamba njia nzuri ya kumjali msichana huyo ni kutoendelea kusambaza video hizo. 

One comment

Comments are closed.

Enable Notifications OK No thanks