Maagizo ya Majaliwa kwa wakuu wa mikoa, wilaya ukusanyaji mapato
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikata utepe, wakati akizindua huduma ya afya ya kijiji, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kusini, Kizimkazi Dimbani, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku tatu Zanzibar. Januari 17, 2020. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.
- Amewataka watumishi wa umma wajiimarishe katika ukusanyaji wa mapato na yaingizwe kwenye mfuko wa Serikali.
- Amesema haitowavumilia watumishi ambao ni wezi, wabadhilifu, wavivu na haitosita kuwachukulia hatua.
- Pia amewataka kusimamia vizuri uwajibikaji na utowaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo yao.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma Tanzania wajiimarishe katika ukusanyaji wa mapato na wahakikishe fedha zote zinazopatikana zinaingizwa kwenye mfuko wa Serikali ili zitumike kuwahudumia wananchi.
Majaliwa ambaye yuko Zanzibar kwa ziara ya kikazi, amesema ni muhimu kwa watumishi kushirikiana katika ukusanyaji wa mapato ili Serikali iweze kupata fedha za kugharamia miradi ya maendeleo.
“Mkuu wa Mkoa usiogope chukua hatua kwa mtumishi yeyote atakayebainika kula fedha za mapato ambazo zinatolewa na wananchi kwa njia ya kodi. Mtumishi wa aina hiyo hafai kuwa mtumishi wa umma,” amesema Majaliwa leo (Januari 17, 2020) wakati akizungumza na watumishi na viongozi wa mkoa wa Kusini Unguja.
Katika taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, kila mtumishi wa umma ametakiwa kuwajibika katika kufanya kazi kwa bidii na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano haitowavumilia watumishi ambao ni wezi, wabadhilifu, wavivu na haitosita kuwachukulia hatua.
Zinazohusiana:
- Majaliwa atoa neno korosho kukosa wanunuzi
- Majaliwa anusa harufu ya wizi wa mali mradi wa nyumba Kigamboni
Sambamba na hilo, amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wanasimamia vizuri uwajibikaji na utowaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo yao.
Amesema huduma za jamii kama za afya, maji lazima ziimarishwe nchini na viongozi wa halmashauri wahakikishe zinapatikana ipasavyo.
“Huduma zikiwa zinatolewa vizuri wananchi hawatolalamika,” amesema Majaliwa.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub amesema halmashauri za wilaya zimeendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato na kutoa huduma kwa jamiii kwa mfano, Halmashauri ya Wilaya ya Kusini ukusanyaji wa mapato umeongezeka kutoka Sh241 milioni kwa mwaka wa fedha 2017/2018 hadi Sh524.51 milioni kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Latest