Majaliwa anusa harufu ya wizi wa mali mradi wa nyumba Kigamboni

November 16, 2018 11:45 am · Daniel
Share
Tweet
Copy Link

Baadhi ya majengo yaliyopo katika eneo la Dege Beach. Picha| yusufbadi.blogspot.com


  • Ni wa nyumba 7,460 katika eneo la Dege Beach  zilizojengwa kwa ubia kati shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kampuni ya Azimio Housing Estate Limited (AHEL).
  • Asikitishwa na uharibifu na wizi wa mali unaoendelea katika mradi huo.
  • Aagiza TRA na NSSF kukutana ili kudhibiti wizi na kuimarisha ulinzi.

Dar es salaam. Waziri Mkuu, Kassimu Majaliwa anusa harufu ya wizi wa mali katika mradi wa nyumba 7,460 katika eneo la Dege Beach katika Halmashauri ya Wilaya ya Kigamboni na kusikitishwa na uharibifu unaoendelea.

Nyumba hizo  zilizojengwa kwa ubia kati shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na kampuni ya Azimio Housing Estate Limited (AHEL) ulisainiwa mwaka 2012 na kuanzisha kampuni ya hodhi ya “Hifadhi Builders”.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu Novemba 13, 2018, katika kampuni hiyo, AHEL ilikuwa inamiliki hisa za asilimia 55 na NSSF asilimia 45. Katika asilimia 55 za AHEL, asilimia 20 ni ardhi iliyotoa kwenye mradi na asilimia 35 angetakiwa kuweka fedha taslimu .

Kutokana na matukio hayo amewaagiza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio na Mkurugenzi wa Mkuu kampuni ya Azimio Housing Estate Limited, Mohammed Iqbal  wakutane na Kamishna Mkuu wa  Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere ili wajadiliane namna ya kudhibiti wizi na kuimarisha ulinzi.

“Kuna mpango gani wa ulinzi wa mali hapa, mali zinaendelea kuibiwa, tutakuja kuanza ujenzi hapa na kukuta hakuna mali hata moja. Ulinzi lazima uimarishwe pande zote mbili za mradi huu eneo la ujenzi na eneo la kuhifadhia vifaa vya ujenzi,” amesema Majaliwa.


Zinazohusiana: Majaliwa atoa neno korosho kukosa wanunuzi


Mradi huo umegharimu Dola za Marekani 653.43 milioni ambazo kati yake ujenzi ungegharimu Dola 544.53 wakati gharama za ardhi zingekuwa Dola 108. 90 milioni sawa na Sh1.5 trilioni.

Kutoka na hali hiyo  Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Erio amemuahidi Waziri Mkuu kutekeleza maagizo hayo ya kukutana na pande zote zinazohusika na utekelezaji wa mradi  ili kujadiliana na namna ya kuimarisha ulinzi na kutatua changamoto ya wizi wa mali unaoendelea katika eneo hilo.

Taarifa hiyo inabainisha kuwa hadi  kufikia Juni 2018 NSSF walishailipa kampuni ya Hifadhi Builders Dola za Marekani 133.8 milioni kama mchango wake kwenye ujenzi wa mradi huo ambazo ni sawa na Sh305.8 bilioni wakati kampuni ya Azimio ilitoa Sh12.6 bilioni tu.

Enable Notifications OK No thanks