Rais Samia: Wakuu wa mikoa kuweni karibu na wananchi mtatue shida zao

August 26, 2025 3:48 pm · Kelvin Makwinya
Share
Tweet
Copy Link
  • Amtaka Makalla kutumia uzoefu kuhakikisha Arusha inaendelea kuwa kitovu cha utalii na kuchagiza fursa za kiuchumi na kidiplomasia 

Dar es salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wakuu wa mikoa  kuwa karibu na wananchi katika maeneo wanayotumikia  ili wabaini na kutatua changamoto zinazowakabili.

Miongoni mwa changamoto ambazo zimekuwa zikilalamikiwa mara kwa mara ni pamoja na migogoro ya ardhi, na upatikanaji wa haki katika mifumo ya haki jinai. 

Rais Samia aliyekuwa akizungumza mara baada ya hafla ya uapisho wa viongozi wapya wateule leo Agosti 26, 2025 Ikulu, jijini Dodoma amesema wakuu wa mikoa watimize wajibu huo kwa kushirikiana na viongozi wengine wanaofanya nao kazi.

“Wote mlioteuliwa ni mahiri katika maeneo yenu…muende mkawajibike ipasavyo na Mungu awasaidie,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Arusha Amos Makalla kutumia uzoefu wake kuhakikisha Arusha inaendelea kuwa kitovu cha utalii na diplomasia pamoja na kuchagiza fursa za kiuchumi mkoani humo.

“Arusha ni mkoa mkubwa kiuchumi na kitovu cha diplomasia katika nchi yetu, kwa uzoefu wako sina shaka utaweza kusimamia maendeleo ya mkoa huu,” amesisitiza Rais Samia.

Rais Samia amesema kuwa Serikali inamipango mikubwa ya maendeleo katika jiji la Arusha ikiwemo ujenzi wa miundombinu na mazingira bora kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) yanayotarajiwa kufanyika katika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 2027.

“Nisikwambie mengi, CPA Makala wewe ni mwenyeji kwenye nafasi hiyo,” ameagiza Rais Samia.

Makalla ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha  Agosti 23, 2025 akitokea kuwa kwenye nafasi ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza kwa Makalla kuhudumu katika nafasi ya ukuu wa mkoa, kwa nafasi tofauti amekuwa Mkuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Katavi pamoja na Mbeya.

Kwa sasa nafasi ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM inashikiliwa na Kenani Kihongosi ambaye uteuzi wake pia  ulienda sambamba na uteuzi wa Dk. Asha-Rose Migiro kwenye nafasi ya Katibu Mkuu CCM akichukua mikoba ya Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye kwa sasa chama kimempendekeza kusimama na Rais Samia kama mgombea mwenza kwenye nafasi ya Makamu wa Rais.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW