Uholanzi yaelemewa na idadi kubwa ya watalii
Makumbusho ya Rijksmuseum katika jiji la Amsterdam ni miongoni mwa maeneo yanayopata wageni duniani, ambapo Serikali inaangalia uwezekano wa kudhibiti idadi ya watu wanaotembelea eneo hilo. Picha|Mtandao.
- Yajipanga kudhibiti watalii wanaoingia nchini humo ili kukabiliana na msongamano mkubwa wa watu kwenye vituo vya utalii vilivyopo katika miji mikubwa hasa Amsterdam.
- Idadi ya watalii inaongezeka kwa kasi ambapo mwaka huu imefikia 19 milioni na miaka 10 ijayo itafikia 29 milioni kwa mwaka.
- Itatumia kodi maalum ya watalii na kuwaelekeza wageni watembelee vivutio vilivyoko pembezoni mwa nchi.
Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea na mikakati ya kuongeza idadi ya watalii, Bodi ya Utalii nchini Uholanzi (NBTC) imesema inajipanga kuzuia matangazo ya utalii na kuongeza kodi kwa wageni wanaoingia nchini humo ili kudhibiti msongamano mkubwa wa wageni katika miji unaotishia uharibifu wa vituo vya utalii vya nchi hiyo.
Hatua hiyo inakuja baada ya vituo vya utalii katika miji mbalimbali kuelemewa na idadi kubwa ya watu na wakati mwingine kuzua tafrani na kutatiza utoaji wa huduma za kijamii.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari nchini humo, idadi ya watalii wanaotembelea Uholanzi inatarajiwa kuongezeka kutoka watalii 19 milioni mwaka huu hadi 29 milioni kwa mwaka katika miaka 10 ijayo ambapo mamlaka nchini humo zinaona hiyo siyo ishara nzuri.
Msongamano mkubwa wa watalii unashuhudiwa zaidi katika majiji makubwa likiwemo Amsterdam na maeneo mengine kama bustani ya Keukenhof na makumbusho ya mashine za upepo (Windmill) zilizopo katika wilaya ya Kinderdijk.
Mashine za upepo (Windmill) zilizopo katika wilaya ya Kinderdijk nchini Uholanzi ambazo zimekuwa kivutio kikubwa cha watalii kutoka maeneo mbalimbali duniani. Picha|Mtandao.
Athari za ongezeko la watalii wanaotembelea nchi hiyo iliyopo bara la Ulaya zimejidhihirisha zaidi katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ambapo zimeongeza gharama za nyumba, kukosekana kwa mpangilio wa jamii na kupungua kwa ujirani na undugu katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
“Idadi ya wageni iliongezeka kutoka 11 milioni mwaka 2005 hadi 18 milioni mwaka 2016,” inaeleza sehemu ya mpango mkakati wa NTBC na kuongeza kuwa, “Kudhibiti idadi ya wageni na kuweka usawa wa fursa za utalii zinazoambatana nazo, tunatakiwa kama nchi tuchukue hatua.”
Zinazohusiana:
- Serikali kuwabana wanaopangisha nyumba kwa watalii bila leseni.
- Tamasha la Urithi Festival kufanyika mikoani kila mwaka.
- Tanzania yaangazia masoko 18 duniani kukuza utalii
- Tanzania yang’ara tena tuzo za eneo bora la utalii duniani
Hata hivyo, NTBC imeanza kuchukua hatua za kuwahamasisha watalii wanaoingia nchini humo kutembelea maeneo ya pembezoni ya nchi hiyo zilizo mbali na Amsterdam.
Pia mwaka jana, Serikali ilianzisha kodi ya watalii ili kupunguza idadi ya wageni lakini walizimudu na kuendelea kuingia katika nchi hiyo. Serikali nchini humo imesema itaongeza tena kodi hiyo mwaka huu lakini haijasema kwa kiasi gani.
Hadi sasa nchi hiyo ambayo inategemea sekta ya utalii kuendesha uchumi wake ina watu 17.12 milioni kwa takwimu zilizotolewa May 10, 2019 na taasisi ya Worldmeters
Bustani ya Keukenhof iliyopo Uholanzi nayo imekuwa kivutio kikubwa cha watalii duniani. Picha|Mtandao.