Mawakili wa Serikali waomba kuzungumza na Kabendera
Mwandishi wa habari, Erick Kabendera akizungumza na Wakili wake, Jebra Kambole alipofika mahakani leo kusikiliza kesi yake ya uhujumu uchumi inayomkabili. Picha|Nuzulack Dausen.
- Waiomba mahakama kuzungumza na mtuhumiwa huyo leo ili kumaliza majadiliano ya makubaliano ya kukiri na kuomba msamaha.
- Upande wa utetezi wa kesi hiyo, ulioongozwa na Jebra Kambole, umesema hauna kipingamizi katika maombi hayo ya Serikali.
- Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega ameahirisha kesi hadi Februari 17 mwaka huu.
Dar es Salaam. Mawakili wa Serikali katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mwandishi wa habari, Erick Kabendera wameiomba mahakama kuzungumza na mtuhumiwa huyo leo ikiwa ni moja za hatua za mwisho za kumaliza majadiliano ya makubaliano ya kukiri na kuomba msamaha (plea-bargaining).
Kabendera, ambaye anaandikia vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi anakabiliwa na mashtaka matatu ya kuongoza kundi la uhalifu kwa lengo la kupata faida au manufaa mengine, kutokulipa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya zaidi ya Sh173.24 milioni na utakatishaji wa fedha kiasi cha zaidi ya Sh173.24 milioni.
Wakili Mkuu wa Serikali, Faraja Nchimbi ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam leo (Februari 11, 2020) kuwa wapo kwenye hatua za mwisho za kumaliza majadiliano na mtuhumiwa baada ya kuandika barua ya kuomba kufanya makubaliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili aweze kuachiwa.
“Kwa muda mrefu tumekuwa kwenye majadiliano na mshtakiwa na sasa tupo kwenye hatua za mwisho za kuandaa documentation (nyaraka). Mbali ya kupata mwakilishi katika majadiliano hayo tunaiomba mahakama tupate muda wa kuongea na mtuhumiwa in person (binafsi) siku ya leo ili tupate nafasi ya kukaa na kukamilisha jambo hili. Pia, tunaomba shauri hilo liahirishwe hadi Jumatatu Februari 17, 2020,” amesema Nchimbi mahakamani hapo.
Nchimbi amesema wamefikia hatua ya kuomba kuongea na Kabendera kwa kuwa muda wote wa majadiliano hayo walikuwa wakiongea na wakili wake.
Upande wa utetezi wa kesi hiyo, ulioongozwa na Jebra Kambole, umesema hauna kipingamizi katika maombi hayo ya Serikali.
Hakimu Mkazi Mkuu, Janeth Mtega alikubaliana na pande zote mbili na kumruhusu Kabendera azungumze na mawakili wa Serikali.
Mtega ameahirisha shauri hilo hadi Februari 17 mwaka huu.
Soma zaidi:
- Polisi Tanznaia yakiri kumshikilia Mwanahabari Kabendera
- Uhamiaji waeleza sababu za kuendelea kumshikilia Mwanahabari Kabendera
- Mwanahabari Erick Kabendera ashtakiwa kwa utakatishaji fedha, uhujumu uchumi
Oktoba 1, 2019, Wakili Kambole aliwaeleza wanahabari katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Kabdendera amewaagiza kumuomba msamaha Rais John Magufuli iwapo kuna kosa lolote alilifanya katika kutekeleza majukumu yake ya uandishi wa habari.
Licha ya Kabendera kutopata dhamana kutokana na mashtaka yanayomkabili, aliendelea kusaka haki yake ili aachiwe huru na kurudi uraiani.
Oktoba 11 alipopanda kizimbani tena, alieleza mbele ya Hakimu Mwandamizi Mkazi, Augustino Rwezile kuwa wameomba kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kumaliza kesi inayomkabili.
“Lakini la msingi ni nia yake Erick ya kuwa nje na kuendelea kuisaidia familia ili maisha mengine yaendelee,” alinukuliwa Kambole na wanahabari.
Tangu wakati huo, Mawakili wa Kabendera wamekuwa wakiendelea na mazungumzo na DPP ili mshtakiwa huyo aachiwe huru.
Kabendera alichukuliwa kwa nguvu nyumbani kwake Mbweni Jijini Dar es Salaam Julai 29, 2019 na watu waliojitambulisha kuwa ni polisi na tangu wakati huo amekuwa akishikiliwa polisi na kuhudhuria mahakamani kuzikiliza shauri lake.