Mawakili wa Kabendera wamwangukia Rais Magufuli
- Wamuomba Rais amsamehe “iwapo aliteleza katika utekelezaji wa majukumu yake ya uandishi wa habari.”
- Erick ameiambia mahakama leo kuwa anaendelea na matibabu na ameanza kutumia dawa.
- Kesi ya mwanahabari huo imeahirishwa hadi Oktoba 11 mwaka huu.
Dar es Salaam. Mawakili wa mwanahabari Erick Kabendera wamemuomba Rais John Magufuli amsamehe mteja wao ili aweze kurejea uraiani.
Kabendera alishtakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam mapema Agosti mwaka huu kwa makosa matatu ya uhujumu uchumi, ukwepaji kodi na utakatishaji fedha. Hadi sasa ameshakaa rumande kwa miezi miwili baada ya kukamatwa na polisi mwishoni mwa Julai mwaka huu.
Kesi ya mwanahabari huyo imeahirishwa tena leo mahakamani hapo hadi Oktoba 11 baada ya Wakili wa Serikali Wankyo Simon kueleza kuwa upelelezi wa shauri hilo haujakamilika katika maeneo machache.
Wakili Jebra Kambole amewaeleza wanahabari nje ya mahakama hiyo kuwa Erick amewaagiza kumuomba msamaha Rais Magufuli iwapo kuna kosa lolote alilifanya katika kutekeleza majukumu yake ya uandishi wa habari.
“Kama (Rais Magufuli) ataupata ujumbe huu tunaomba aweze kulifanyia kazi hilo jambo… na kama ataona Erick kuna somewhere (mahali fulani) anatakiwa afanye jambo lolote sisi tupo tayari kulifanya ili kuweza kusecure uhuru wake na kuwa nje kama raia wa kawaida,” amesema Kambole.
Hata hivyo, alipoulizwa iwapo watatumia fursa ya kuomba msamaha uliyootolewa na Rais Magufuli kwa watuhumiwa wa uhujumu uchumi, Kambole amesema kwa sasa Erick hana uwezo wa kulipa fedha anazotuhumiwa nazo.
“Ili uweze kusamehewa katika maeneo kama hayo (uhujumu uchumi) lazima uwe na fedha za kulipa, fedha ambazo unatuhumiwa kuzitakatisha ama kuziiba. Sasa huwezi ukaomba msamaha kama pesa zenyewe huna…au huwezi kuandika barua kwa DPP. DPP ameshatoa msimamo kwamba kama una pesa andika.
“Sisi tunasema kwamba kwa kuwa bado tunafanya utafiti wa namna gani lakini kwa sasa Erick hana pesa za kuzilipa kama mwandishi wa habari wa kawaida lakini tunaomba kama somewhere, somehow aliteleza aweze kusamehewa na yeye kwa nafasi hiyo,” amesema Kambole.
Awali akiwa ndani ya mahakama, Kambole ameiomba Serikali kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo inayomkabili Erick kwa kuwa shauri hilo halina dhamana na afya ya mteja wake bado haijaimarika.
Erick leo pia ameiambia mahakama kuwa anaendelea vyema kupatiwa matibabu kutokana na maradhi yanayomsumbua.
“Nimeanza kutumia dawa na madaktari wanaendelea kunitibu,” amesema Erick aliyeingia mahakamani hapo Saa 3:08 asubuhi huku akichechemea mguu mmoja.