Erick Kabendera aitaarifu mahakama kuanza majadiliano na DPP
Mwanahabari wa habari za uchunguzi Erick Kabendera (Aliyekaa) akizungumza na Wakili wake, Jebra Kambole katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu leo. Picha|Nuzulack Dausen.
- Wakili wake asema wamefikia hatua hiyo ili mwanahabari aweze kuwa huru na ajumuike na familia yake.
- Erick ameiambia mahakama kuwa alishirikishwa kwenye majadiliano hayo na ameridhia.
- Kesi imeahirishwa hadi Oktoba 24 lakini iwapo watamalizana mapema itaitwa kabla ya muda huo.
Dar es Salaam. Mwanahabari wa habari za uchunguzi Erick Kabendera ameingia kwenye orodha ya watuhumiwa wa makosa ya uhujumu nchini ambao wameomba kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ili kumaliza kesi inayomkabili.
Erick anatuhumiwa kwa makosa matatu ikiwemo kuongoza genge la uhalifu, utakatishaji fedha wa zaidi ya Sh173 milioni na kukwepa kodi kiasi hicho hicho cha pesa.
Wakili wa mwanahabari huyo, Jebra Kambole ameijulisha mahakama kuwa wameshaanza mchakato wa kufanya makubaliano na upande wa Serikali ili mteja wao aweze kuwa huru.
Awali Wakili Mwandamizi wa Serikali, Wankyo Simon aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo bada haujakamilika ila wanafahamu kuwa Erick tayari ameshaanza mchakato wa majadiliano hayo.
“Barua ameshaandika ipo kwenye mchakato. Tutakapokuwa tumeshakamilisha majadiliano tutainotify (tutaijulisha) mahakama yako,” amesema Simon mahakamani leo (Oktoba 11, 2019).
Kabendera naye alipopewa nafasi na mahakama kuzungumza amesema uamuzi wa kuingia majadiliano hayo ni wake na umeshirikishwa kikamilifu na mawakili wake.
Soma zaidi:
- Mwanahabari Erick Kabendera ashtakiwa kwa utakatishaji fedha, uhujumu uchumi
- Mawakili wa Kabendera wamwangukia Rais Magufuli
Hakimu Mwandamizi Mkazi, Augustino Rwezile ameiahirisha kesi hiyo mpaka Oktoba 24 ila ameeleza kuwa iwapo pande hizo mbili zitamaliza mapema majadiliano yao waijulishe mahakama ili iweze kuendelea.
Nje ya mahakama, Kambole amewaambia wanahabari kuwa wameamua kufanya hivyo kwa sababu sheria iliyofanyiwa marekebisho hivi karibuni inaruhusu kufanya hivyo na kuijulisha mahakama.
“Mchakato unaruhusu kupunguziwa pesa siyo kiasi kile kile, unaruhusu kulipa kwa ‘instalment’ (kwa awamu), unaruhusu kupata adhabu ndogo zaidi, vyote hivyo tuliviconsider (tulivizingatia).
“Lakini la msingi ni nia yake Erick ya kuwa nje na kuendelea kuisaidia familia ili maisha mengine yaendelee,” amesema Kambole ambaye hakuta kueleza undani baadhi ya masuala watakayoenda kujadiliana na Serikali.
Hata wakati pande hizo mbili zikiendelea na mchakato wa majadilino, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRC) umesema “unaamini mchakato wa makubaliano (pre-bargaining arrangement) utakaoanzishwa kati ya mshtakiwa na mwendesha mashtaka mkuu wa Serikali utaenda kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa kisheria na kwamba matokeo ya makubaliano hayo yatakuwa na manufaa kwa pande zote mbili.”