Wagonjwa wa Corona wazidi kuongezeka Tanzania

April 13, 2020 8:09 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Wagonjwa wengine 14 watangazwa leo na kufanya idadi ya walioambukizwa ugonjwa huo kufikia 46.
  • Kati yao waliogundulika leo, 13 wapo Dar es Salaam na mmoja yupo jijini Arusha. 

Dar es Salaam. Idadi ya wagonjwa wa virusi vya corona (COVID-19) nchini Tanzania imeendelea kuongezeka baada ya Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kutangaza ongezeko la wagonjwa wapya 14 na kufanya idadi ya walioambukizwa ugonjwa huo kufika 46 hadi sasa. 

Wagonjwa hao wapya, ambao ni wengi kuwahi kuripotiwa kwa siku moja tangu mgonjwa wa kwanza agundulike Machi 16,  wameongeza idadi ya waliokutwa na madhira ya COVID-19 kutoka watu 32 walioripotiwa awali Aprili 10, 2020. 

Waziri Ummy katika taarifa yake iliyotolewa leo (Aprili 13, 2020) amesema wagonjwa wote 14 ni Watanzania ambapo 13 wanatoka katika Mkoa wa Dar es Salaam na mmoja yupo katika Mkoa wa Arusha. 

Idadi hiyo mpya ya wagonjwa wa COVID-19 inafanya Dar es Salaam kuendelea kuwa kitovu cha ugonjwa huo ambao umeshaua watu watatu hadi sasa. 

Hadi leo Dar es Salaam imeripotiwa kuwa na wagonjwa 32 kati ya 46 waliotangazwa nchini. 

Hii ni sawa na kusema kuwa wagonjwa saba kwa kila 10 walioripotiwa Tanzania wapo Dar es Salaam. 


Zinazohusiana:


 “Wagonjwa wote wanaendelea na matibabu chini ya uangalizi wa wataalam wa afya. Ufuatiliaji wa watu waliokuwa karibu na wagonjwa unaendelea,” amesema Ummy katika taarifa hiyo.  

Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kuzingatia miongozo ya kujikinga na ugonjwa huo ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara, kutokugusa pua, mdomo au macho, kutumia tishu wakati wa kukohoa au kupiga chafya.

Pia kuepuka mikusanyiko isiyo ya lazima na ikiwezekana kutulia nyumbani. 

Enable Notifications OK No thanks