Simulizi ya mwanafunzi ‘babu’ wa miaka 53 aliye hatarini kuacha shule ya msingi – 3

July 19, 2020 5:31 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Ugumu wa maisha unazidi kuhatarisha safari ya kielimu ya Mzee Mabindo, shule anaitaka na familia inamtegemea, je anafanya nini kutatua mtanziko huo? 
  • Mkewe hataki kusikia habari za mumewe kusoma. 

Katika sehemu zilizopita za makala hii, tuliangazia namna Mabindo alivyojiunga shule na changamoto zilizomfanya atoweke shule hadi sasa. Je, ataendelea na shule? Endelea. 

Mabindo, huku akiongea kwa sauti ya chini inayoonekana kuwa na huzuni, anasema toka mfadhili huyo afariki dunia miaka miwili iliyopita, kwa sasa utawala haumsaidii kwa chochote na ndio maana yuko sokoni kuangalia namna atakavyoihudumia familia yake.

Biashara kubwa iliyompeleka hapo ni kununua na kuuza fulana. Kila siku asubuhi hutafuta fulana za mtumba na baadaye huzichambua na kuzipunguza kiwango kwenye cherehani kisha kuziuza kwenye mnada.


Aomba kupigwa jeki

“Bado ninatamani kurudi shule hivyo endapo nitapata mtu wa kunifadhili naweza kuendelea na masomo yangu,”anasema Mabindo huku akionesha kukata tamaa.

Ombi hilo lilizungumzwa pia na mwalimu mkuu msaidizi wa shule anayosoma, ambaye anaiomba jamii ione umuhimu wa kumsaidia mwanafunzi huyo ili aendelee na shule.

Mwalimu huyo anasema sababu kubwa inayomfanya asihudhurie shule na huenda inahusiana kwa kiwango kikubwa na masuala ya kiuchumi na kwamba hata awali mahudhurio yake yalikuwa hafifu. 

“Alikuwa na utoro wa rejareja,” anasema Gwihava akielezea kuwa sababu ilikuwa ni masuala ya kutafuta fedha. 

Abdallah Mabindo akiwa na wanafunzi wenzake shuleni hapo. Mwanafunzi huyo mwenye miaka 53 aliamua kwenda shule ili kujifunza kusoma na kuandika na kuondoa ujinga. Picha| Mariam John. 

Ndugu, jamii na marafiki wanamzungumziaje

Uamuzi wa Mabindo kurudi shule katika umri mkubwa ili akasome na watoto wadogo sawa na wajukuu wake, umepokelewa kwa hisia mseto miongoni mwa wanajamii. 

Familia yake imegawanyika. Mwanaye anakubali baba aendelee kusoma lakini mkewe anaona hatua hiyo ni kama “upuuzi” tu. 

Mariam Abdalah (26), mtoto pekee wa Mabindo, anasema anafurahishwa na kitendo alichokifanya baba yake kwa kuwa anaamini elimu haina mwisho.

Mariam ambaye ana Stashahada ya (Diploma) ya Jiolojia anasema jamii inaweza kumtazama vibaya baba yake lakini kiuhalisia anachokifanya kinabadilisha historia ya maisha yake.

“Amebadilisha mtizamo kuwa siwezi kupata elimu tena, na hii imemjengea uimara na uthubutu wa kufanya mambo yake na si hivyo tu lakini ametoa ushawishi kwa watu wengine wenye umri kama wa kwake kuona bado wanaweza kupata elimu ya darasani,” anasema Mariam anayefanya kazi katika moja ya migodi ya madini wilayani Kahama. 

Kuhusu kumsaidia baba yake ili atimize ndoto zake anasema anafanya hivyo japokuwa jukumu kubwa la kuhudumia ni mzazi wake na kwamba wakati wote baba yake anajiona kama hawajibiki ipasavyo. 

“Nafanya kwa nafasi yangu lakini huenda kwa kuwa yeye ni baba na wajibu wa baba ni kuhudumia familia ndio maana anaona aibu kuiacha kama ilivyo na kuendelea na masomo yake,” anasema.

Mkewe hataki kusikia habari za mumewe na hata hakutaka kabisa kuzungumza nami mtazamo wake juu ya elimu ya Mabindo. 

Masanja Mussa, mmoja wa majirani wa Mzee Mabindo, anasema anamfahamu kwa muda mrefu na alikuwa hajui kusoma na kuandika jambo lililomkosesha fursa mbalimbali mtaani kwakwe.

Jambo hilo pia lilimfanya ashindwe kutumia simu, kusoma magazeti na hata fursa za kiuongozi zinapokuja mtaani kwake alishindwa kuchaguliwa kutokana na tatizo hilo.

“Hata alipojaribu kufanya biashara wakati mwingine alikuwa akiwazidia chenji wateja wake,”anasema Bakari Elias, jirani mwingine wa Mabindo. 

Hata hivyo, wengi wanamuunga mkono kwa kuwa ni hatua muhimu katika maisha. 

Shamsa Abdallah anasema kitendo alichokifanya ni kizuri kwa kuwa kinamsaidia kuondoa giza lililokuwa mbele yake.


Zinazohusiana:


Wataalamu wa masuala ya elimu wanaeleza kuwa alichokifanya Mabindo ni sahihi na kitu cha kuigwa na wengine waliokosa elimu kipindi cha nyuma. 

Dk Benard Kapaya, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania tawi la Mwanza (OUT) anasema ubongo wa mtu hauna kizuizi na unakuzwa kwa kutegemea na mazingira uliyokulia aidha darasani au nje ya darasani. 

Kuhusu matokeo ya wastani ya Mabindo darasani hasa kushika nafasi za chini tofauti na inavyodhaniwa na watu wengine, Dk Kapaya anasema mtoto mdogo ana uwezo mkubwa wa kushika na kuyahifadhi mambo mengi kuliko mtu mkubwa ambaye anaweza kushika mambo mawili ama matatu.

“Suala la kushika nafasi si la muhimu bali ni kujua huyo anayefundishwa ana uwezo wa kushika na kuelewa kile anachofundishwa, mfano aliyekaa darasanI na asiyekaa wote ni wasomi na wanaweza kutekeleza majukumu yao kikamilifu,” Dk Kapaya ameiambia Nukta. 

Anasema wapo watu walioenda shule lakini hawawezi kufanya biashara vizuri na wapo ambao hawajapata elimu ya darasani lakini wanafanya biashara vizuri.

Dk Kapaya anasema wanapotoa elimu wanawapima kwa kuangalia kile kinachofundishwa kinaeleweka ama hamna.

Hali ya elimu nchini Tanzania

Ripoti ya Takwimu Muhimu Tanzania (Tanzania in Figures 2019) iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu inaeleza kuwa hadi kufikia mwaka 2012 asilimia 71.8 ya Watanzania walikuwa wanajua kusoma na kuandika. 

Hiyo ni sawa kusema zaidi theluthi moja ya Watanzania hawajui kusoma na kuandika kama ilivyokuwa kwa mzee Mabindo ambaye sasa ameamua kuondoa ujinga kwa kurudi shuleni. 

Hata hivyo, hadi kipindi hicho Zanzibar ndiyo ilikuwa na watu wengi zaidi wanaojua kusoma na kuandika kwa asilimia 80 ukilinganisha Tanzania Bara (asilimia 71.5). 


Bado ana ndoto

Umri mkubwa bado haunekani kumzuia Mabindo kuishi ndoto zake. Hadi sasa bado anasisitiza kuwa ndoto yake kuu ni kuhitimu elimu ya chuo kikuu ili atimize lengo la kuwa mwanaharakati wa kuhamasisha watu wasiojua kusoma na kaundika kurudi shule.

“Ninaamini kuna Watanzania wengi tu hususan watu wazima wengi wao hawajui kusoma na kuandika na kwa mantiki hiyo nitatumia hata baiskeli kuzunguka nchi nzima kuhamasisha watu wasiojua kusoma na kuandika warudi shule,” anasema huku akitabasamu. 

Mzee Abdalah anasema pamoja na changamoto hizo lakini bado anapata muda wa kujisomea awapo nyumbani usiku na wakati mwingine mtoto wa jirani yake humfundisha kwa kuwa hana mtoto mdogo nyumbani na mkewe hamuungi mkono.


‘Mabindo atumie fursa kikamilifu’

Serikali inaeleza kuwa Mabindo kama wanafunzi wengine wana nafasi ya kusoma elimu bila malipo kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne hivyo naye anapaswa kuitumia.

“Kwa sasa Serikali imetangaza elimu bure kuanzia darasa la awali mpaka kidato cha nne na imetoa mwanya huo kwa wanafunzi wote, hivyo ni vema mwanafunzi huyo akaendelea kupata elimu,” anasema Afisa Elimu jiji la Mwanza Efrahim Majinge. 

Takwimu za Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) za mwaka 2020 zinaeleza kuwa wanafunzi wa darasa la kwanza walioandikishwa hadi Machi, 2020 ni milioni 1.55 sawa na asilimia 97.5 ikilinganishwa na lengo la kuandikisha wanafunzi milioni 1.59.  

“Uandikishaji wa rika lengwa la watoto wa darasa la kwanza umeongezeka kutoka asilimia 95 mwaka 2015 hadi asilimia 97.5 mwezi Machi, 2020,” amesema Waziri wa Tamisemi Seleman Jafo katika hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2020/21. 

Hata hivyo, watu ambao hakukwenda shule bado wana nafasi ya kusoma elimu ya watu wazima au kwa walioikosa (MEMKWA) ambayo inasaidia kupunguza idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika.

Jafo katika hotuba hiyo amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya utoaji elimu ili kuhakikisha kila mwanafunzi anapata elimu bora. 

/
No matches found for this filter
31 May, 2026 · TZS
No forex gainers today
No forex losers today
Forex rates unavailable
31 May, 2026 · TZS
No gainers today
No losers today
31 May, 2026
No active movers today

Inaendeshwa na Nukta AI

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
AKILI UNDE INAVYOIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA KINYWA NA MENO

AKILI UNDE INAVYOIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA KINYWA NA MENO

Nukta TV

WAFAHAMU 'THE BIG FIVE' WA AFRIKA

WAFAHAMU 'THE BIG FIVE' WA AFRIKA

Nukta TV

HIVI NDIVYO UNAWEZA KUSAFISHA MENO YAKO

HIVI NDIVYO UNAWEZA KUSAFISHA MENO YAKO

Nukta TV