Corona: Serikali ya Tanzania haijaamuru wafanyakazi, wanafunzi kukaa nyumbani
- Serikali haijatoa tamko lolote kuhusu wanafunzi na wafanyakazi kukaa nyumbani kipindi hiki cha Corona.
- Habari zinazosambaa kuhusu jambo hilo ni uongo.
Dar es Salaam. Kama umeshakutana na taarifa inayosambaa kwenye mtandao wa Whatsapp juu Serikali ya Tanzania kuamuru wafanyakazi na wanafunzi kukaa nyumbani ili kujikinga na Corona, fahamu kuwa huo ni uzushi.
Serikali haijatoa tamko lolote kuhusu wanafunzi na wafanyakazi kukaa nyumbani kipindi hiki ambacho dunia inapambana na janga la COVID-19.
Habari hiyo inayosambaa mitandaoni hasa Whatsapp kwa mfumo wa maandishi iliyoambatanishwa na kiunganishi inasema Serikali imetangaza ofisi zilizo na wafanyakazi zaidi ya 10 kuchukua likizo za lazima kuanzia Februari 17, 2021 kwa wiki mbili na shule zote kufungwa kwa muda wa wiki mbili kuanzia tarehe hiyo.
Sehemu ya habari hiyo inasema “The Tanzania Government have announced measures that all workplaces with 10 employees or more are to have paid mandatory leave to avoid the spread of the COVID-19 coronavirus starting from February 17, 2021. All schools are to close for 2 weeks also from February 17th,”
Ujumbe huo unamaanisha kuwa “Serikali ya Tanzania imetangaza njia za kujikinga na Corona kwa ofisi zilizo na wafanyakazi zaidi ya 10 kwenda likizo ya lazima kuanzia Februari 17, 2021. Shule zote kufungwa kwa wiki mbili kwanzia Februari 17.”
Hata hivyo, habari hiyo haina ukweli wowote kwasababu Serikali haikutoa tamko lolote kama hilo siku za hivi karibuni.
Zinazohusiana:
- Ni uzushi: Kidato cha sita hawajaagizwa kubeba tangawizi, malimao shuleni
- Serikali ya Tanzania yazungumzia uvaaji wa barakoa
Pia kiunganishi cha habari hiyo ambacho kinamuelekeza mtu kwenda kwenye tovuti nyingine ili kusoma zaidi, lakini hakuna habari kama hiyo. Kiunganishi hicho kina maudhui ambayo hayafai kuonyeshwa kwa umma.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii wanapaswa kutumia taarifa sahihi kutoka vyanzo sahihi vya Serikali ikiwemo Wizara ya Afya na Shirika la Afya Duniani (WHO) ili kujikinga na COVID-19.
Latest
