Tanzania ina wagonjwa wa Corona zaidi ya 100, kuagiza chanjo
- Rais Samia amesema kati ya hao, 70 wanatumia mitungi ya gesi.
- Awataka Watanzania kuchukua tahadhari.
- Serikali imeridhia kuagiza chanjo kupambana na ugonjwa huo.
Mwanza. Hatimaye, Serikali ya Tanzania imetoa tena hadharani takwimu za wagonjwa Corona tangu ilipositisha Mei mwaka jana huku Rais Samia Suluhu Hassan akisema tayari wameridhia kuagiza chanjo ambayo itakuwa inatolewa kwa hiari kwa wananchi kujikinga na ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Rais Samia, kwa sasa Tanzania ina wagonjwa wa Corona zaidi ya 100 ambao wanaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali nchini.
Rais Samia amesema kati ya wagonjwa hao, 70 wanaendelea kupatiwa matibabu ya kupumua kwa kutumia mitungi ya gesi huku idadi iliyobaki wakipatiwa matibabu ya kawaida.
“Kuhusu ugonjwa wa corona maamuzi yetu ni kuwa tutaendana na dunia inavyokwenda na kwamba naomba niwe mkweli, Tanzania tuna wagonjwa kama 100 na kitu na kati yao 70 wapo kwenye mitungi ya gesi,” amesema Samia.
Rais Samia ametoa takwimu hizo leo Juni 28, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari baada ya kuulizwa swali na Mhariri wa Shirika la Habari la Tanzania (TBC) Lulu Sanga aliyetaka kufahamu ni lini Tanzania itaanza kutoa takwimu za wagonjwa wa Corona.
Tanzania iliacha kutoa takwimu za Corona Mei 2020 katika Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Hayati Rais John Magufuli ambapo mara ya mwisho takwimu zilizotolewa hadharani zilirekodi jumla ya visa 509 vya Corona na vifo 21.
Rais Samia ametoa takwimu hizo leo Juni 28, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari. Picha| Mtandao.
Tanzania iliacha kutoa takwimu za Corona Mei 2020 katika Serikali iliyokuwa ikiongozwa na Haya
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo kama wataalam wa afya wanavyoelekeza.
“Ninaomba tuendelee kuchukua tahadhari zote za kujinga na ugonjwa wa Corona kama unaona ukipiga nyungu itakusaidia fanya hivyo na kama unaona utatumia dawa zingine tumia ila Serikali tunasisitiza kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo kama zinavyotolewa na wataalam,” amesema Samia
Amesema kwa sasa hali ni mbaya kwa nchi jirani na kwamba wazazi walinde familia zao hususani kuwakinga watoto.
Chanjo inakuja Tanzania
Rais amesema tayari Serikali yake imeridhia kuwa chanjo ya Corona itakuja nchi kwa muda ukaopangwa na itakuwa inatolewa kwa hiari kwa wananchi licha ya kuwa baadhi ya watu wakiwemo wafanyabiashara wamepata nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Samia, tayari Tanzania imejiunga katika mpango wa Umoja wa Mataifa wa utoaji chanjo wa COVAX tangu Juni 15 mwaka huu.
Kinachosubiriwa kwa sasa ni kutathmini ni aina gani ya chanjo italetwa na mifumo itayotumwia kuileta, kuisambaza na kuihifadhi itakapoanza kutumika.
Amesema zaidi ya Dola za Marekani milioni 470 (zaidi ya Sh1 trilioni) zimetengwa kwa ajili kupambana na ugonjwa huo ambapo nusu ya hela itaenda kushughulikia chanjo ya corona huku nyingine itaenda kwa mashirika yaliyoathirika.
Latest
