Ni uzushi: Kidato cha sita hawajaagizwa kubeba tangawizi, malimao shuleni

Mwandishi Wetu 1012Hrs   Mei 27, 2020 NuktaFakti
  • Baadhi ya shule zimezushiwa kuchangisha wazazi pesa ya kununua tangawizi na malimao ili kujikinga na Corona.
  • Shule ya St Mary’s Mazinde Juu imesema haijatoa masharti hayo.
  • Kidato cha sita watakiwa kurudi shuleni wakifuata tahadhari zote za afya.

Dar es Salaam. Shule zenye wanafunzi wa kidato cha sita nchini Tanzania ni miongoni mwa taasisi zilizoingia kwenye mikono ya wazushi safari hii baada ya kuzushizwa kuwa zimeagiza wazazi kutoa fedha kwa ajili kununua tangawizi na malimao ili kuwezesha watoto wao kujikinga na ugonjwa huo. 

Habari hiyo inayosambaa mitandaoni inadai kuwa baadhi ya shule zimeagiza wanafunzi wa kidato cha sita ambao wanarudi shuleni Mei mosi kubeba malimao, tangawizi na wengine wakiambiwa kubeba fedha zitakazotumika kununua bidhaa hizo. 

Katika habari hiyo ambayo inasambaa kwenye mitandao ya kijamii imezitaja baadhi ya shule ikiwemo ya St. Mary’s Mazinde Juu ya mkoani Tanga kuwa zimeagiza wanafunzi kutekeleza maagizo hayo. 


Zinazohusiana: 



Ukweli uko wapi?

Habari ya wazazi wa St. Mary’s Mazinde Juu kuwalipia watoto wa kidato cha sita wanaosoma shuleni hapo Sh750,000 kwa ajili ya malimao na tangawizi, siyo ya kweli na ni uzushi mtupu. 

Uongozi wa shule hiyo katika taarifa yake ya Mei 26 umeeleza kuwa haijatoa masharti yoyote kwa wanafunzi kurudi shuleni hapo huku ikibainisha kuwa wazazi hawajalalamikia suala hilo kwa sababu shule haijatoa maagizo kama hayo. 

Imesema inaendelea na maandalizi ya kuwapokea wanafunzi Juni mosi na itazingatia miongozo iliyotolewa na Wizara ya Afya juu ya kujikinga na ugonjwa huo na si vinginevyo. 

Serikali ya Tanzania ilitangaza kuwa wanafunzi wa kidato cha sita wanatakiwa kurudi shuleni Juni mosi ili kujiandaa na mitihani inayotarajia kuanza Juni 29. 

Pia ilizitaka shule kuweka mazingira sawa kuhakikisha wanafunzi wanakuwa salama dhidi ya Corona wawapo shuleni. 

Related Post