BoT yahamisha mali, madeni ya China Commercial Bank kwenda NMB
- Ni baada ya kukaa chini ya usimamizi wa BoT kwa siku 90.
- Ilishindwa kutimiza masharti ya ukwasi na mtaji wa kujiendesha.
- Kwa sasa, shughuli za benki hiyo zitakuwa zinatolewa na benki ya NMB.
Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania imehamisha mali na madeni ya benki ya biashara ya China (China Commercial Bank) kwenda kwa benki ya NMB Plc baada ya kukaa chini ya uangalizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa siku 90 kutokana na kutokidhi matakwa ya ukwasi.
Novemba 19 mwaka jana, BoT iliiweka benki ya China Commercial Bank chini ya usimamizi wake kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya ukwasi.
Kwa mujibu wa kanuni za mabenki na taasisi za fedha zinazosimamia masuala ya mitaji za mwaka 2015 (The Banking and Financial Institutions Capital Adequacy (Amendment) Regulations, 2015) benki inatakiwa kuwa na mtaji usiopungua Sh15 bilioni ili kutoa huduma.
Katika kipindi ambacho benki hiyo iliwekwa chini ya BoT ilikuwa ikitafutwa njia itakayoisaidia kurejesha uwezo wa kuendesha shughuli za kibenki ama kwa kujiendesha yenyewe au chini ya usimamizi wa benki nyingine ya biashara.
Hata hivyo, BoT katika taarifa yake iliyotolewa leo Machi 4, 2021 imesema tayari imefanya uamuzi wa kuhamisha mali na shughuli zote za benki hiyo kwenda kwa benki ya NMB.
“Benki Kuu ya Tanzania inautaarifu umma kuwa kwa mamlaka iliyopewa na Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, mchakato wa kutafuta njia ya kuirejeshea China Commercial Bank uwezo wa kuendesha shughuli za kibenki umekamilika na uhamishaji wa mali na shughuli za benki hiyo tayari umefikiwa kuanzia Machi 4, 2021,” imeeleza taarifa iliyotolewa na BoT.
Aidha, BoT imeeleza kuwa wateja wa benki hiyo watajulishwa muda muafaka wa kuanza na jinsi ya kupata huduma za kibenki katika benki ya NMB.
“Kwa sasa, wadaiwa wote wanatakiwa kuendelea kulipa madeni yao kulingana na masharti na makubaliano waliyofikia na benki hiyo wakati wakichukua mikopo,” imesema taarifa ya BoT.
Katika hatua nyingine, BoT imesema itaendelea kusimamia na kuimarisha sekta ya benki na fedha nchini ili iweze kutoa mchango katika ukuaji wa uchumi Tanzania.
Zinazohusiana:
Siku 90 zilivyokuwa kwa China Commercial Bank
Kutokana na uamuzi huo wa kiudhibiti, BoT iliisimamisha bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya benki hiyo na kuteua msimamizi aliyeisimamia kwa siku zisizozidi 90.
Katika kipindi hicho, benki hiyo ilifungwa na haikuruhusiwa kutoa huduma yeyote kwa wateja wake
“Tunatoa taarifa hii ili kusije kuwa na taharuki. Hizi ni taratibu za kawaida ili kuhakikisha tunalinda maslahi ya wateja wa benki hii,” alieleza Gavana wa BoT, Florens Luoga wakati akitoa tamko la kuchukua usimamizi wa benki hiyo mwaka jana.
Alisema lengo la uamuzi huo siyo kuifilisi benki hiyo yenye makazi yake makuu katika makutano ya Mtaa wa Ohio na Garden jijini Dar es Salaam.
China Commercial Bank inaingia katika orodha ya benki ambazo zilishawahi kuwekwa chini ya uangalizi wa BoT baada ya kushindwa matakwa ya kimtaji.
Katikati mwa mwaka 2018 BoT iliiweka Bank M katika usimamizi wake baada ya kubaini kuwa taasisi hiyo ya kifedha ilikuwa na mapungufu makubwa ya kimtaji.