BoT yahimiza matumizi ya malipo ya kidijitali
- Yasema malipo ya kidigitali ni muhimu kwa mabadiliko ya uchumi na kupunguza utegemezi wa pesa taslimu.
Dar Es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imehamasisha Wananchi kufanya malipo ya bidhaa na huduma kwa kutumia njia za kidigitali ikiwemo mashine za malipo (POS) hatua inayotajwa kuchangia ukuaji wa uchumi.
Mashine za POS (Point of Sale) ni vifaa vya kielektroniki vinavyotumiwa na wafanyabiashara kupokea malipo kutoka kwa wateja wao kwa njia ya kidigitali badala ya mteja kulipa pesa taslimu anatumia kadi ya benki kulipia bidhaa au huduma alizonunua.
Taarifa ya Emmanuel Tutuba, Gavana wa benki hiyo iliyotolewa leo Disemba 23, 2024 imesistiza kuwa matumizi ya huduma za kifedha kwa njia hiyo ni rahisi zaidi kwani hayatozwi ada zozote.
“Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuwakumbusha wananchi kwamba malipo yanayofanywa kwa kutumia kadi za benki (debit, credit, au prepaid) kwenye mashine yoyote ya POS hayatozwi ada yoyote…
…Wafanyabiashara wote wamekatazwa kutoza ada au gharama za ziada kwa miamala inayofanywa kwa mashine za POS,” imesema taarifa ya Tutuba.
Taarifa ya BoT inakuja wakati ambao Watanzania wanatarajiwa kufanya manunuzi mengi ya bidhaa za vyakula, vinywaji, mavazi yanayotokana na sikukuu za mwisho wa mwaka.
Licha ya hamasa hiyo kujitokeza msimu huu bado takwimu zinaonesha kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kigitali nchini hususani za kibenki.
Ripoti ya Mifumo ya Malipo kwa mwaka 2023 iliyotolewa na BoT inaonesha kuongezeka kwa idadi ya mashine za POS kwa asilimia 18.25.
Mwaka 2023 Tanzania ilikuwa na mashine 8,652 ikilinganishwa na mashine 7,317 zilizokuwepo mwaka 2022 hukuidadi ya miamala ya ndani inayofanywa kwa mashine hizo ikiongezeka kwa asilimia 46.95 na miamala ya fedha za kigeni ikiongezeka kwa asilimia 43.72.
Thamani ya miamala ya ndani iliyofanyika kupitia mashine za POS imeongezeka kwa asilimia 43.04 na kufikia Sh1.92 bilioni kwa mwaka 2023. ikilinganishwa na Sh1.34 bilioni kwa 2022. Vilevile, thamani ya miamala ya fedha za kigeni imeongezeka kwa asilimia 23.22, kufikia Sh662.28 bilioni, 2023 kutoka Sh537.5 bilioni, 2022.
Kufuatia kuongezeka huko Bot imesema kuwa malipo ya kidigitali ni muhimu kwa mabadiliko ya uchumi yakitarajiwa kupunguza utegemezi wa pesa taslimu, gharama za miamala na kuboresha ufanisi wa shughuli za biashara.
Kupitia taarifa hiyo wananchi wamehimizwa kutumia fursa ya faida zinazotokana na malipo ya kidijitali na kuripoti ukiukwaji wowote wa sera ya kutotoza ada kwa miamala inayofanywa kwa kadi kupitia dawati la malalamiko la benki hiyo.