BoT yasitisha huduma za Yetu Microfinance, yaiweka chini ya uangalizi

December 12, 2022 9:42 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Huduma za beki hiyo zimesitishwa kwa siku 90. 
  • Bodi ya Wakurugenzi na uongozi wa benki wasimamishwa.
  • Ni kutokana na upungufu mkubwa wa ukwasi na mtaji. 

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeiweka chini ya uangalizi benki ya Yetu Microfinance Bank Plc na kusitisha huduma za kifedha ndani ya siku 90 kutokana na upungufu mkubwa wa ukwasi na mtaji.

“Napenda kuwataarifu kuwa, kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu namba 56(1)(g)(i) &(iii) cha sheria ya Benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006, Benki Kuu ya Tanzania imeiweka Yetu Microfinance Bank Plc chini ya usimamizi wake kuanzia leo,” amesema Gavana wa BoT, Professa Florens Luoga katika taarifa yake iliyotolewa leo Novemba 12, 2022.

Sambamba na kuiweka chini ya uangalizi, BoT imesitisha shughuli za kibenki za taasisi hiyo ya fedha kwa siku 90. 

“Katika kipindi kisichozidi siku tisini (90) kuanzia siku ya taarifa hii, shughuli za utoaji wa huduma za kibenki za Yetu Microfinance Bank Plc zitasimama ili kuipa nafasi Benki Kuu kutathmini hatua za kuchukua ili kupata ufumbuzi wa suala hili,” amesema Prof Luoga. 

Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, inaipa BoT mamlaka ya kusimamia shughuli zote za kibenki na taasisi za fedha nchini kwa lengo la kuhakikisha uimara na ustahimilivu wa sekta ya benki na ya fedha kwa ujumla.


Soma zaidi


Kutokana na ukwasi na mtaji mdogo wa benki hiyo unaoweza  kuhatarisha usalama wa sekta ya fedha, BoT imeisimamisha Bodi ya Wakurugenzi na Uongozi wa Yetu Microfinance Bank Plc kuanzia leo Disemba 12, 2022.

Aidha, BoT imemteua Meneja Msimamizi ambaye atakuwa na jukumu la kusimamia shughuli za Yetu Microfinance Bank Plc kwa kipindi ambacho itakuwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania. 

Licha ya benki hiyo kuwekwa chini ya uangalizi BoT itaendelea kulinda maslahi ya wenye amana katika mabenki kwa lengo la kuleta ustahimilivu katika sekta ya fedha.

Huenda hatua za kusitisha huduma za benki hiyo za bahati mbaya kwa sababu uendeshaji wa benki hiyo umekuwa ukisua sua katika miaka ya hivi karibuni. 

Mathalan, mwaka 2021 benki hiyo ilipata hasara ya Sh1.12 bilioni ikilinganishwa na hasara ya Sh54.9 milioni ya mwaka juzi, kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2021 ya benki hiyo.

Hasara hiyo ya mwaka 2021 ni ongezeko la Sh1.07 bilioni ndani ya kipindi cha mwaka mmoja au sawa na asilimia 1,948.

Yetu microfinance Bank ilianzishwa Disemba 23, 2013 na mpaka sasa ina matawi sita ikiwemo tawi la Mzizima na  Mbagala (Dares Salaam), tawi la  Ifakara na Mngeta (Morogoro),  tawi la Zanzibar and Kilwa mkoani Lindi.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW