Namna ya kubaini “Breaking news” inayopotosha kuhusu Corona
- “Breaking News” (Habari Mpasuko) hutoa taarifa muhimu na fupi ambayo imetokea ndani ya muda mfupi.
- Kubaini aina hiyo ya bahari inayopotosha tazama kwa makini picha, kichwa cha habari kwa sababu mara nyingi hukosa uhalisia.
Dar es Salaam. Kila linapotokea tukio au jambo muhimu ambalo watu au jamii inatakiwa ifahamu kwa haraka, vyombo vya habari hasa vilivyopo mtandaoni huchuana ili kushika nafasi ya kwanza kutoa habari husika.
Habari hizo hujulikana kama “Breaking News” (Habari Mpasuko) ambazo hutoa taarifa muhimu na fupi ambayo imetokea ndani ya muda mfupi ili watu wapate taarifa wakati uchakataji wa habari kamili ukiendelea.
Mathalan, taarifa ya kifo cha waziri kufariki kwa ugonjwa wa Corona itakuwa na umuhimu mkubwa kwenye jamii na hivyo utoaji wake nao pia unatakiwa ufanyike haraka.
Siyo jambo geni kusikia #BreakingNews: Waziri apata maambukizi ya Corona au #MPYA: Watu 2,000 wafariki kwa Corona. Aina hii ya habari utaipata zaidi kwenye mitandao ya kijamii kama Twitter au Facebook ya watu binafsi na vyombo vya habari.
Hata hivyo, aina hiyo ya habari imekuwa ni nyenzo kwa baadhi ya watu kupotosha na kuzua taharuki kwenye jamii kwa kutumia janga la Corona linaloitesa dunia kwa sasa.
Tumia mbinu hizi kubaini habari mpasuko inayopotosha au isiyo ya kweli kuhusu ugonjwa wa Corona.
Matumizi ya picha zisizo na uhalisia
Hii ni alama muhimu sana kuitambua “Breaking News” ya uongo kwa sababu hutumia picha isiyoendana na tukio au jambo linazungumzwa (Doctored or out-of-context imagery).
Watengezaji wa habari hizi za uzushi hufanya hivyo kwa sababu wanajua habari picha husambaa kwa haraka na kwa urahisi kuliko habari isiyo na picha.
Ili kuepuka mtego wa kutumia au kusambaza habari kama hizo mtandaoni, jipe muda wa kujiridhisha kama picha iliyotumika ni sahihi na inaendana na tukio lenyewe. Zana kama Google Image, RevEye Search zinaweza kukusaidia kubaini ukweli wa picha iliyotumika.
Kichwa cha habari za uongo
Habari nyingi “Breaking News” (Habari Mpasuko) ambazo ni za uzushi huwa na vichwa vya habari ambavyo hutumia maneno ambayo kwa kiasi kikubwa huweza kuzua taharuki au kutoa vitisho kwa lengo la kutimiza makusudi fulani kwenye jamii.
Mara nyingi vichwa vya habari hivyo vya mpasuko wakati wingi hutumia tukio kubwa, majanga makubwa au watu maarufu. Mfano, kabla ya Tanzania kutangaza mgonjwa wa kwanza Machi 16, 2020 kulisambaa habari feki katika mfumo wa Break News ikisema “BREAKING NEWS: Tanzania confirms first case of Coronavirus”.
Hivyo kabla ya kusambaza habari za mtindo huo unatakiwa kuwa makini sana ili kuzuia kusambaza habari za uongo.
Zinazohusiana:
Wahusika wa uongo
Mbinu ya tatu ya kubaini habari za uongo kwenye habari za “breaking news” ni matumizi ya wahusika wa uongo au wakutungwa. Mara nyingi watengezaji hao wa habari za uzushi hutumia majina ya watu maarufu au wenye nyazifa kubwa serikalini wakiwa na lengo la kuzua taharuki.
Mathalan, Waziri wa Afya wa Tanzania wakati huo, Ummy Mwalimu alizushiwa kuwa alipata Corona na habari hiyo ilisambaa kwa haraka lakini baadaye ikagundulika siyo kweli.
Hivyo wakati huu wa ambao dunia bado inapambana na janga la corona, hatuna budi kila mmoja wetu kuendelea kuwa makini katika kusambaza habari ambazo hatuna uhakika nazo.
Latest
