Uzushi: WHO haijathibitisha dawa ya “Ziverdokit” kutibu Corona
- Wazushi wamedai kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) limeithibitisha dawa kutibu Corona.
- Mankind Pharma wamesema dawa ya Ziverdokit haijathibitishwa na WHO licha ya kuwa inatibu Corona.
Dar es Salaam. Habari za uzushi kuhusu tiba ya Corona zimeendelea kusambaa kwa kasi duniani mpaka kufikia hatua ya watu kusambaza uzushi kuwa Shirika la Afya Duniani (WHO) limethibitisha dawa aina ya “Ziverdokit” kutibu ugonjwa wa Corona.
Hata hivyo, habari hiyo haina ukweli wowote kwa sababu WHO haijatoa maelekezo kuhusu dawa hiyo.
Tangazo hilo linalosambaa katika mfumo wa picha kwenye mitandao ya kijamii hasa Whatsapp, linaonesha nembo ya WHO ikiwa na picha ya dawa na familia, ikiambatana na maneno yanayosema “Treat & Prevent COVID-19, COVID-19 is not a death sentence. Treat easily with ZIVERDOKIT”
Maneno hayo yanamaanisha kuwa “Tibu na jikinge na COVID-19, COVID-19 siyo hukumu ya kifo. Jitibu na ZIVERDOKIT”.

Kampuni ya Mankind Pharma wakanusha
Timu ya Nukta Fakti imewasiliana na kampuni ya Mankind Pharma iliyopo India inayotengeneza dawa ya Ziverdokit, ambapo imesema haijatoa tangazo hilo na siyo la kweli kuwa WHO imeithibitisha bidhaa hiyo.
“Hilo sio tangazo letu. WHO hawajathibitisha bidhaa hiyo kuwa inatibu COVID-19,” amesema huduma kwa wateja wa Mankind Pharma aliyekuwa akiongea na Nukta Habari.
Hata hivyo, kampuni hiyo inadai Ziverdokit ni dawa inayotibu ugonjwa wa Corona na imethibitishwa na Serikali ya India kwa matumizi.
“Dawa hizi zimetengenezwa kutibu Corona, zinasaidia mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Corona,” amesema huduma kwa wateja wa Mankind Pharma aliyekuwa akiongea na Nukta Habari.
Hii ni mara ya tatu Shirika hilo kuzushiwa taarifa ya uzushi baada ya Januari 2, 2021 kuzushiwa kwamba imetoa fedha za ufadhili kwa watu kujikinga na Corona.
Kama umekutana na taarifa hiyo, usiwe mwepesi wa kuisambaza kwa watu wengine kabla ya kujiridhisha kama ni kweli ili kupunguza madhara ya habari za uzushi kwenye jamii.