Fahamu: Dawa hii siyo chanjo ya Corona
- Ni dawa aina ya Covifor inayotumika kutuliza dalili za wagonjwa wa COVID-19.
- Baadhi ya watu wanazusha kuwa ni chanjo ya Corona maalum kwa watu wa Afrika.
- Ukweli ni kuwa dawa hiyo imeidhinishwa kutumika Marekani na nchi za Umoja wa Ulaya.
Dar es Salaam. Tangu mwezi Septemba mwaka huu, watumiaji wa mitandao ya kijamii barani Afrika wamekuwa wakishirikishana bandiko (posts) linaloonyesha dawa inayojulika kama ‘Covifor’ ambayo ni muendelezo wa dawa ya ‘Remdisivir’.
Kifungashio cha dawa hiyo kimembatana na maandishi yaliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza yanayoyosema “Not for distribution in the United States, Canada and the European Union”. Maandishi hayo yanamaanisha, “Siyo kwa ajili ya usambazaji katika nchi za Marekani, Canada and Umoja wa Ulaya”.
Watu waliofikiwa na ujumbe huo, wanadai kuwa nchi za magharibi zinafanya majaribio ya chanjo dhidi ya Corona katika nchi zinazoendelea duniani ikiwemo Afrika.
Pia picha ya dawa hiyo zinazosambaa mtandaoni hasa WhatsApp zimeambatana na maneno yanayosema “Wake up Africa, this is not a cure but a trap to kill you or use you as ‘laboratory rat’,” ikimaanisha kuwa “Amkeni Afrika, hiyo siyo dawa bali ni mtego wa kuwaua au kuwatumia nyie kama “panya wa maabala”.
Hata hivyo, taarifa hiyo haina ukweli wowote na inalenga kupotosha. Dawa ya Covifor siyo chanjo dhidi ya Corona na imekuwa ikisambazwa na kutumika katika nchi mbalimbali za Umoja wa Ulaya.
Covifor inatibu nini?
Covifor ni dawa halisi inayotengenezwa na kampuni ya famasia ya Hetero Drugs ya nchini India, kama ilivyoonyeshwa kwenye kifungashio chake.
Kwa mujibu wa Hetero Drugs, Covifor inatumika kuwatibu wagonjwa wa COVID-19 waliolazwa hospitali wenye dalili mbalimbali za ugonjwa huo.
Dawa hiyo ina ujazo wa miligramu 100 na inaingizwa mwilini kwa njia ya sindano chini ya usimamizi wa madaktari na mazingira salama ya utoaji huduma za afya.
Dawa hiyo ilianza kuuzwa nchini India tangu mwezi Juni, 2020 na gharama yake ni kati ya Euro 57 na 68 (Kati ya Sh160,494 na Sh191,467).
Zinazohusiana:
Dawa hiyo siyo chanzo ya COVID-19
Kampuni ya Hetero Drugs imesema dawa hiyo siyo chanjo dhidi ya Corona kama inavyovumishwa na baadhi ya watu, bali ni dawa ya kutuliza maambukizi ya virusi hivyo.
“Hii siyo dawa ya kuzuia au chanjo, bali ni tiba inayokusudia kutuliza dalili za COVID-19 kwa wagonjwa ambao wanaumwa sana wakati wakiwa hospitali,” amesema mwakilishi wa kampuni hiyo wakati akihojiwa na shirika la habari la FRANCE 24.
Maneno yaliyoandikwa kwenye kifungashio cha dawa hiyo ya “Siyo kwa ajili ya usambazaji nchini Marekani, Canada and Umoja wa Ulaya”, kampuni hiyo imesema yanalenga kuzuia usambazaji holela na soko lisilo rasmi la dawa hiyo.
Kwa mujibu wa mkataba wa usambazaji wa dawa hiyo uliosainiwa kati ya Hetero Drugs na shirika la kimataifa la Gilead Sciences Inc, unaonyesha kuwa dawa hiyo inaweza kusambazwa katika nchi 127 duniani, ikiwa itapata kibali cha mamlaka za nchi husika.
Hata hivyo, nchi za Marekani na Canada hazipo kwenye orodha hiyo, ingawa dawa hiyo imethibitishwa kutumika.
Ili kujiweka salama, sehemu sahihi ya kupata taarifa kuhusu chanjo ya Corona ni kupitia tovuti na mitandao ya kijamii ya wizara za afya za nchi mbalimbali, mashirika ya afya kama Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Africa-CDC) na Shirika la Afya Duniani (WHO).
Latest