Serikali yasitisha tena mikutano ya siasa Tanzania
- Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi asema lengo la uamuzi huo ni kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi
- Hii ni mara ya pili Serikali inazuia mikutano ya siasa ndani ya miaka 10, baada ya Magufuli kufanya hivyo mwaka 2016.
Arusha. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amesitisha utoaji wa vibali vya mikutano ya siasa kutokana na hofu za kiusalama, ikiwa ni mara ya pili kwa Serikali kuchukua hatua hiyo ndani ya miaka 10.
Katambi amemuagiza Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Camilius Wambura, kusitisha utoaji wa vibali hivyo kwa kwa vyama vyote vya siasa, ili kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi.
Katambi ametoa agizo hilo leo Juni 26, 2026, bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Dodoma Mjini, Paschal Kinyere aliyetaka kujua mipango ya Serikali kudhibiti mandamano yalipangwa kufanyika nchini.
“Kupitia Bunge lako tukufu ninamwelekeza IGP Wambura kusitisha utoaji wa vibali vya mikutano ya hadhara kwa kipindi hiki kwa vyama vyote vya siasa, iwe Chama Cha Mapinduzi au chama kingine chochote,” amesema Katambi.
Hata hivyo, Katambi hakuweka bayana ni muda zuio hilo litadumu ili kuvipa fursa vyama vya siasa kukutana na wafuasi wao nchini.
Hii ni mara ya pili Serikali ya Tanzania inazuia mikutano ya hadhara ya kisiasa ndani ya miaka 10.
Ni kama mwaka 2016?
Katikati mwa mwaka 2016 aliyekuwa Rais wa Tanzania, hayati John Magufuli alipiga marufuku mikutano hadhara ya siasa na kuruhusu ile ya wanasiasa waliochaguliwa kwenye maeneo ya utawala, hatua iliyokosolewa vikali na vyama vya siasa na watetezi wa haki za binadamu.
Hata hivyo, Mwaka 2023 Rais Samia Suluhu Hassan aliondoa zuio hilo lililokuwa limedumu kwa miaka 6.
Wiki za hivi karibuni kumekuwa na maudhui mtandao yanayohamasisha maandamano kufanyika siku ya Sabasaba ikiwa ni mwendelezo wa kudai mabadiliko ya kidemokrasia na uwajibikaji kwa Serikali.
Baada ya kusambaa taarifa kuhusu maandamano hayo, Jeshi la Polisi lilitoa tahadhari dhidi ya maandamano hayo, likisema hayajapata kibali na kwamba hatua za kisheria zitachukuliwa kwa mtu yeyote atakayeshiriki au kuyaratibu kinyume cha sheria.
Katambi amesema Serikali imebaini kuwepo kwa viashiria vya matishio ya kiusalama katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mikutano ya hadhara pamoja na mitandao ya kijamii kuchochea uvunjifu wa amani.
Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kukusanya ushahidi dhidi ya watu wanaodaiwa kuhusika na vitendo hivyo, huku akisisitiza kuwa wale watakaobainika kuvunja sheria watahojiwa na kufikishwa mahakamani.
Baadhi ya wachambuzi na wadau wa demokrasia nchini wamekosoa hatua hiyo wakieleza kuwa itanyima demokrasia na kuirudisha nyuma nchi katika mazingira ya vyama vya siasa kutokutana na wafuasi wao.
‘Demokrasia inaminywa’
Efron Mkungilwa, mchambuzi wa masuala ya siasa kutoka jijini Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari kuwa uamuzi huo unarudisha nyuma hatua za kidemokasia ambazo tayari Tanzania ilikuwa imeanza kuzipiga za watu kusikilizwa.
“Mwelekeo kama huu unawanyima watu uhuru wa kutoa maoni yao, na athari inayoweza kujitokeza na huenda watu wakaja na mbinu nyingine zaidi ya kutaka kusikilizwa,” amesema Mkungilwa huku akishauri mbinu nyingine ingetumika kudhibiti tishio la maandamano.
Chama cha ACT Wazalendo, ambacho ni cha pili kwa ukubwa nchini, katika taarifa yake kwa umma kimeelani hatua hiyo na kwamba kinapinga maelekezo hayo kilichoyaita ni haramu.
“Inashangaza kuona Serikali kwa makusudi inaleta taharuki kwa wananchi, kuwajaza hofu na vitisho katika wakati ambao Serikali inatakiwa kuwajibika katika kusimamia haki za wananchi na kuwaleta pamoja baada ya mauaji ya Oktoba 29,” amesema Rashid Habib Ali, Waziri Kivuli wa Wizara ya Ulinzi, Mambo ya Ndani na Usalama wa Raia wa ACT-Wazalendo.
Rais wa TLS akosoa
Kwa Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) Boniface Mwabukusi uamuzi huo ni kinyume na Katiba ya Tanzania akisisitiza kwamba chama chake kitachukua hatua kwa atakayetekeleza agizo hilo.
Amesema Waziri wa Mambo ya Ndani hana mamlaka yeyote ya kuzuia au kutozuia mikutano iliyoruhusiwa kisheria na kwamba TLS imepokea kwa mshtuko taarifa hizo.
“Tutakaa na kuona namna ambayo tutachukua hatua za kisheria za ndani ya nchi na nje ya nchi dhidi ya yeyote atakaye jaribu kutekeleza agizo hili haramu na batili kwa kukiuka katiba na sheria za nchi,” amesema Mwabukusi katika mtandao wa X.
Nyongeza na Nuzulack Dausen, Dar es Salaam.