Wafahamu ‘mashujaa’ wa maendeleo Kigoma

August 23, 2021 12:27 pm · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link

                             


  • Mashujaa hao ni waraghabishi ambao wanashawishi wananchi kuibua kero na kutatua matatizo yao.

Kigoma. Kwa mwaka wa nne sasa Mwamvua Kechegwa amekuwa moja ya watu ambao ni kimbilio kwa wakazi wengi hasa wanawake katika Manispaa ya Kigoma Ujiji. 

Kila siku hutenga muda wake kufuatilia masuala aliyoletewa hususan yanayohusu ukatili wa kijinsia na ushiriki wa wanawake katika shughuli za maendeleo katika mitaa ya manispaa hiyo iliyopo Magharibi mwa Tanzania. 

Wakati nakutana naye kwa mara ya kwanza, Mwamvua alikuwa akiingia katika ofisi ya mtendaji wa kata ya Kasimbu akiwa na mgeni aliyekuwa akitaka kujitolea kumtibu mmoja ya watoto wawili waliotekelezwa na wazazi wao katika moja ya mitaa ya kata hiyo. 

Kwa mujibu wa Mwamvua, mtoto huyo alikuwa akisumbuliwa na funza miguuni na mikononi. 

“Tumekuja kuona namna bora ambayo tunaweza kuwasaidia watoto hao,” anasema huku akitikisa kichwa taratibu kushoto na kulia, akionyesha kusikitishwa na jambo. “Nimeshawajulisha ustawi wa jamii,” anaongeza. 

Kwa wageni, wanaweza kudhani Mwamvua (30) ni moja ya viongozi wa juu wa masuala ya maendeleo ya jamii katika manispaa hii, la hasha. 

Dada huyo ni miongoni mwa wanachama 21 wa chama cha waraghabishi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji ambao wanajitolea kuwaelimisha wakazi wa maeneo hayo kushiriki kikamilifu katika kuibua kero na kutafuta suluhu kwa matatizo wanayoweza kuyamudu badala ya kusubiria Serikali kwa kila jambo. 

Mwamvua na wenzie wamekuwa wakifanya kazi kwa karibu na sehemu kubwa ya viongozi wa Serikali za mitaa katika kuhamasisha wananchi kushiriki katika mikutano, kuchangia hoja, nguvukazi au michango ya kifedha katika kutatua sehemu kubwa ya matatizo yao yakiwemo ya ulinzi na usalama. 

Waraghabishi hao ambao wanaitwa na baadhi ya wakazi wa manispaa hii kama “mashujaa” walipatiwa mafunzo ya uraghabishi mwaka 2017 wilayani Mbogwe, Geita na taasisi ya kiraia ya Tamasha inayotumia njia ya uraghabishi katika kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo. 

“Tumefanikiwa kupata uelewa wa kushawishi wenzetu kuanza kujitegemea…tunaiwezesha jamii kujitambua kutokana na elimu tunayowapatia,” anasema John Edward, Mwenyekiti wa chama cha waraghabishi Manispaa ya Kigoma-Ujiji. 

“Hii ni kazi ya kujitolea tu,” anaongeza.

John Edward (Kulia), mwenyekiti wa waraghabishi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji akiwaongoza wenzake katika mipango yao ya utendaji ikiwemo kutoa elimu kwa jamii kuhusu ushiriki katika shughuli za maendeleo. Picha| Gift Mijoe.

Ili kuwafikia wakazi wengi zaidi na kufanya kazi ipasavyo na viongozi wa Serikali za mitaa, Edward anasema walikuwa na waraghabishi katika kata zote 19 za manispaa hii lakini kadri siku zinavyokwenda idadi yao inapungua. 

Kwa sasa, anasema, wana waraghabishi imara katika kata 14 baada ya wengine kushindwa kujitolea kwa kuwa kazi hiyo haiwaingizii kipato licha ya kutumia muda mwingi kutoa elimu au kushiriki mikutano ya mitaa kuchangia kuibua kero na kutoa utatuzi. 

Tangu mwaka 2017 wakazi hao walikuwa wakifanya shughuli hizo kwa kujitolea kama chachu ya mabadiliko bila kuwa na taasisi yeyote ambayo ingewasaidia kufikia malengo yao kwa haraka. 

Kutosajili chama chao kama asasi ya kiraia inayoshughulikia masuala ya kijamii (CBO) kulifanya kutotambuliwa na baadhi ya maofisa wa mitaa na kata na kuzifanya kazi zao kutokuwa halali. 

Hamza Selemani, Katibu wa chama hicho cha waraghabishi anasema kukua kwao kulitokana na utekelezaji wa Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali kwa Uwazi (OGP) na baada ya Tanzania kujitoa sehemu kubwa watendaji walihitaji utambulisho mpya ambao hawakuwa nao. 

Hata hivyo, waliendelea na shughuli zao japo kwa changamoto lukuki za kiutambulisho na fedha. 

Pamoja na kupata vikwazo vya kiutambuzi, baadhi ya viongozi wa Serikali za mitaa wanaeleza kuwa waraghabishi wamechangia sana wananchi kuamka katika kushiriki shughuli za maendeleo. 

Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Buzebazeba kata ya Buzebazeba Shaban Ibrahim anasema waraghabishi wamewasaidia sana katika kuhamasisha watu kuhudhuria mikutano kwa kuwa baadhi yao walijitolea kuzunguka na ofisa huyo. 

“Wakati nahamia hapa mwaka 2017 walikuwa wamepamba moto sana, kila mkutano wapo, baadhi waliwachukua vijana, wanawake na wengineo kwenda kuwafundisha na namna ya kuibua kero na kutatua matatizo yao ila miaka ya hivi karibuni walipoa kidogo,” anasema. 

“Kazi zao zimezaa matunda sana na kuongeza ushiriki wa wananchi katika mtaa wetu kwenye masuala ya maendeleo,” anasema Ibrahim. Waraghabishi katika Manispaa ya Kigoma Ujiji wamekuwa chachu ya uanzishwaji wa miradi ya kijamii ikiwemo ujenzi wa shule kwa ajili ya kuinua elimu ya watoto katika manispaa hiyo iliyopo mkoani Kigoma. Picha| Gift Mijoe.

Tangu wameanza shughuli za uraghabishi, wameshawapoteza wenzao wengi ambao hawakuvumilia kazi hiyo kutokana na kutokuwa na posho kwa wanachofanya. 

Waraghabishi hao, akiwemo Mwamvua ambaye ni Mhasibu msaidizi wa chama, wanafurahia mafanikio waliyoyapata kutokana na kazi yao ikiwemo kuongeza ushirika wa wakazi wa mitaa mbalimbali kushiriki mikutano, ujenzi wa madarasa na kufanya ulinzi shirikishi kuongeza ulinzi na usalama mitaani.  

“Mwanga Kusini wakati tunawaelimisha wananchi kuibua na kutatua kero zao tuliambiwa kuna tatizo la teleza ambalo baadhi ya wanaume wahalifu walikuwa wanapaka oili mwilini, wanaingia kwenye nyumba wanazoishi wanawake na kuwabaka, kuwaibia na hata kuwajeruhi pale wanapokabiliana nao. 

“Baada ya kulifuatilia hili suala, ulianzishwa ulinzi shirikishi na sasa teleza ni historia,” anasema Selemani. 

Waraghabishi hao, wanaojumuisha vijana, wanawake na wazee, walifanikiwa kusajili chama chao Machi mwaka huu na sasa wanatafuta wafadhili ambao watasaidia kuwapatia mafunzo zaidi katika shughuli zao kuchangia katika kuendesha ofisi yao.

Kwa sasa, kwa mujibu wa Edward, kila mwanachama anachangia Sh2,000 kwa mwezi ambayo inasaidia kulipia ofisi iliyopo katika soko la Buzebazeba pembezo mwa barabara ya Lumumba.

Hata hivyo, kutokana na ukata, siyo wanachama wote wanaweza kuchangia jambo linalopunguza ufanisi wa kundi hilo.

“Kwa sasa tunatafuta wadau ambao watakuwa tayari kutufundisha na kutuwezesha kutoa elimu kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na Corona,” anasema mwenyekiti huyo. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW