Ijue mbinu iliyochochea mabadiliko makubwa Mbogwe

July 28, 2021 6:24 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni uraghabishi ulioshawishi watu kuwabana viongozi wao vijijini.
  • Yasaidia wananchi kujua wajibu wao, kuchangia maendeleo.

Mbogwe. Kwa anayefika Mbogwe kwa mara ya kwanza, basi neno uraghabishi litakuwa ni sehemu ya maneno ambayo atayafahamu kwa haraka. 

Huenda kwa baadhi ni neno jipya ila kwa wakazi wengi wa halmashauri hii iliyopo mkoani Geita, uraghabishi imekuwa ni chachu ya maendeleo ya jamii.

Kwa lugha nyepesi, uragabhishi ni mfumo wa mawasiliano unaolenga kubadilisha tabia ndani ya jamii ili kufikia malengo yaliyowekwa na ni moja ya mbinu ambayo Ofisi ya Rais-Tamisemi inatumia kufanikisha maendeleo katika ngazi za chini. 

Dhana ya uraghabishi inahususisha mfumo wa kijamii ambao unawawezesha wananchi wa eneo fulani kutambua na kuzipigania haki zao, kutatua changamoto za kijamii na kushiriki kikamilifu katika kujiletea maendeleo bila kuisubiri Serikali.

Kwa mujibu wa Katibu wa Mtandao wa Waraghabishi Wilaya ya Mbogwe (MBODANETI) Leonard Mbigule, uraghabishi uliingia wilayani humo mwaka 2011/12 kupitia mafunzo yaliyotolewa na shirika la Tamasha kwa ufadhili wa shirika la Oxfam kwa wananchi katika kata 10.

Mafunzo ya kuwajengea uwezo wananchi yaliyofanyika katika makundi ya wanawake, vijana, wazee na walemavu yalilenga zaidi kuwajengea uwezo wananchi kujitambua na kusimamia maendeleo katika maeneo yao. 

“Uraghabishi ni mfumo wa kufanya kazi za jamii, ndani ya jamii kupitia wanajamii wenyewe,” anasema Mbigule.

Baada ya mafunzo hayo kuzaa matunda waliyatanua na kuzifikia kata saba zilizobaki mwaka 2018/19 ili kuhakikisha maeneo yote wilayani humo wananchi wake wanahamasika kuanzisha miradi yao wenyewe na kuikamilisha.

Mafanikio hayo yamezidi kuwavuta zaidi wadau wa maendeleo ambapo safari hii mafunzo hayo yaliwezeshwa na Shirika la Twaweza na kuendeshwa na Tamasha.  

Kazi kubwa iliyofanywa miaka ya hivi karibuni ilikuwa ni kutoa mafunzo, kufanya tafiti shirikishi, kuchagua kamati za wananchi na kubaini vipaumbele vya makundi yote kwenye jamii na kisha kuanza kutafuta suluhu za changamoto zote zilizoibuliwa. 

Miongoni mwa changamoto zilizojitokeza zaidi ni ukosefu wa huduma za kijamii; maji, shule, vituo vya afya na wananchi hasa wanawake kutoshiriki kikamilifu katika mikutano na shughuli za maendeleo.

“Tangu hapo kazi zimekuwa zikifanywa kwa ushirikiano wa pamoja, hiyo ilileta hamasa kubwa kwa jamii kuona kumbe maendeleo yanahusu wote na ndiyo maana sasa kazi zimekuwa zikifanyika kwa uratibu huo,” anasema mraghabishi huyo. 

                 Jengo la ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe mkoani Geita. Picha| Gift Mijoe.

Uraghabishi ulivyobadili mambo

Licha ya kuwa mapokeo ya dhana ya uraghabishi kutofautiana miongoni mwa wananchi wa Mbogwe, imejenga jamii inayojitambua yenye kuzifahamu changamoto na kuzitafutia suluhu za kudumu. 

Kabla ya uraghabishi kuingia wilayani humo, ilikuwa ni vigumu kwa wananchi hasa wanawake kushiriki katika mikutano ya vijiji na shughuli za maendeleo. 

“Zamani tulikuwa tunavutana sana na wananchi kuhudhuria mikutano ya vijiji kwa sababu baadhi ya mambo hayakukaa sawa, kwa sasa muamko ni mkubwa sana mpaka viongozi inabidi tuwe makini na usimamizi wa rasilimali,” anasema Mwenyekiti wa Kijiji cha Shenda, Kata ya Masumbwe wilayani humo, Justini Mkali. 

Hamasa hiyo ya kujitoa kwenye shughuli za maendeleo imewezesha wananchi kujenga maboma ya zahanati katika vijiji 85 kati ya 87, shule za msingi na sekondari na kuanzisha miradi ya maji. 

Baadhi ya shule za sekondari zilizojengwa na nguvu ya wananchi ni pamoja na Isebya, Bunigonzi, Nyakafuru, Isangijo na Nyakasuluma ambazo zimesaidia kuinua elimu ya watoto wa wilaya hiyo.

                     

Wapiga ‘spana’ wizi mapato

Kutokana na wananchi kuwa sehemu ya utekekelezaji wa miradi ya kijamii, tabia za baadhi ya viongozi kutumia vibaya fedha za wananchi zimepungua kwa sababu kila mwananchi anafahamu kinachoendelea.

“Zamani hela zilikuwa zikipigwa na hapakuwa na maendeleo kama haya,” anasema Saila Macheku (28), mkazi wa Kijiji cha Shenda, Kata ya Masumbwe. 

Wakazi wa mbogwe wanasema kwa sasa, viongozi hawasukumwi kusoma mapato na matumizi kila baada ya miezi mitatu na kila hatua ya utekelezaji wa miradi ya kijamii katika maeneo yao wanawashirikisha wananchi.

Wanawake na watoto hawalazimiki kutembea umbali mrefu kutafuta maji kwa sababu wananchi wamejenga miradi ya visima katika vijiji vyao ili kupata maji safi  na salama. Picha| Gift Mijoe.


Sauti za wanawake zasikika  

Mkazi wa kata ya Nyasato, Kabelela Augustine anasema  ushiriki wa wanawake kwenye mikutano umeongezeka na kufanya sauti zao ziwe na nguvu hasa wanapotoa hoja zinazolenga kuboresha huduma za kijamii kama ujenzi wa zahanati na uchimbaji wa visima vya maji.

“Wakina mama wamekuwa ni wahamasishaji wakubwa wa maendeleo hususani uchangiaji wa huduma za afya,” anasema Augustine ambaye pia ni Katibu wa Siasa na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbogwe.

Muamko huo umesaidia kuingia katika vikao muhimu vya maamuzi zikiwemo kamati za vijiji za maendeleo, kugombea nafasi za uongozi katika serikali za mitaa na ndani ya vyama vya siasa.

Lucy Mganga, mraghabishi wa kata ya Nyasato amefanikiwa kuwa Diwani wa Viti Maalum wilayani humo kwa sababu ya ujasiri na kujiamini aliojengewa katika mafunzo ya uraghabishi. 

Kuboreshwa kwa huduma za kijamii, kumerahisisha wananchi wa Mbogwe kuinuka kiuchumi kwa kujishughulisha katika miradi mbalimbali ya kuwaingizia kipato hasa kilimo na uchimbaji madini.

Jengo la Shule Mpya ya Msingi ya Muungano iliyopo kata ya Masumbwe ambayo inajengwa kwa nguvu za wananchi ili kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani katika shule ya Masumbwe. Picha| Gift Mijoe

Nini siri ya mafanikio hayo?

Mwenyekiti wa MBODANET, Petro Hyera anasema kilichosaidia Mbogwe kupiga hatua kubwa ya maendeleo ni mfumo wa uraghabishi uliowaleta pamoja wananchi na Serikali kufanya kazi kwa kushirikiana na kuyapa kipaumbele makundi yote kwenye jamii bila kumuacha mtu nyuma.

“Ukienda vijijini kwa sasa, ukaangalia miradi ambayo wananchi wameibua na wanatekeleza ni mingi sana,” anasema Petro na kubainisha kuwa wana matarajio kuwa maeneo mengine ya Tanzania yatajifunza kutoka Mbogwe.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mbogwe, Pastory Mukaruka anasema uraghabishi umekuwa nyenzo muhimu kwa wananchi kujiletea maendeleo na Serikali kuwawezesha pale wanapopata changamoto.

Anasema muitikio wa wananchi katika kushiriki katika miradi ya maendeleo ni mzuri lakini inategemea na mazingira ya watu wa eneo husika, hivyo Serikali na wadau wataendelea kutoa elimu ili wananchi watambua kuwa wana wajibu wa kujiletea maendeleo.

“Suala la maendeleo linatofautiana kata moja na nyingine. Unaweza kukutana kata moja muamko ni mkubwa katika kuchangia miradi ya maendeleo lakini kata zingine wananchi wanatakiwa kuendelea kuelimishwa waone kwamba shughuli hizo ni kwa ajili ya maendeleo yao,” anasema mkurugenzi huyo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW