Tanzania kununua ndege nyingine tano
- Malipo ya awali yamekwishafanyika.
- Zitawasili mwaka 2023.
- Kwa sasa, Tanzania ina ndege tisa na mbili ziko njiani.
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema tayari imefanya malipo ya awali ya ununuzi wa ndege nyingine tano ambazo zitawasili nchini mwaka 2023 ili kuimarisha sekta ya anga, utalii na biashara.
Kwa sasa, Serikali ya Tanzania ina ndege tisa na nyingine mbili aina ya Airbus A220-300 za masafa ya kati ambazo tayari Serikali ilikwisha kufanya malipo zinatarajiwa kuwasili mwaka huu.
Ndege hizo mbili zina uwezo wa kubeba abiria 160 mpaka 170 zitasaidia kuongeza wigo wa kutoa huduma za usafiri wa anga kati ya Tanzania na nchi za jirani.
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Gerson Msigwa amesema Serikali ina mpango wa kuongeza ndege nyingine tano na tayari Serikali imefanya malipo ya awali ya ndege hizo na “matarajio yetu ndege hizi zitafika mwaka 2023.”
“Hivi tunavyozungumza wataalam wetu wameshakaa na wazalishaji wa ndege kwa ajili ya kuangalia muonekano wa ndege hizo, vitu gani wanataka viwemo,” amesema Msigwa leo Agosti 28, 2021 wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dodoma.
Kati ya ndege hizo tano, mbili zitakuwa kubwa aina ya Dreamliner ambapo moja ni kwa ajili ya kubeba mizigo na nyingine ya abiria.
“Inapanga kununua ndege mbili za masafa ya kati zile za abiria 160 mpaka 170 lakini inapanga kununua ndege moja aina ya Bombardier na hizi zote zinatarajia kuwasili mwaka 2023,” amesema Msigwa.
Ikiwa ndege hizo zitanunuliwa kama ilivyopangwa, ifikapo mwaka 2023, Serikali ya Tanzania itakuwa na ndege 16.
Rais Samia Suluhu Hassan, akiwa pamoja na Viongozi mbalimbali akikata utepe kuashiria kupokea ndege mpya aina ya Bombadier DASH 8-Q400 iliyonunuliwa na Serikali katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Julai 30, 2021. Picha| Michuzi Blog.
Kwa sasa, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lnachuana vikali na Shirika la ndege la Precision Air baada ya kampuni ya ndege ya FastJet kumwaga manyanga miaka miwili iliyopita.
Kumekuwepo na mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii na bungeni kwa baadhi ya watu wakieleza kuwa ununuzi wa ndege hauna tija kwa kuwa unailetea hasara Serikali wakati wengine wakisema ni bora biashara hiyo iendelee ili kusaidia kukuza shughuli nyingine za kiuchumi hususan utalii.
Hata hivyo, katika hotuba zake Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisema kuwa Serikali yake itaendelea kuilea ATCL kimkakati ii liweze kujiendesha kwa ufanisi ikiwemo kulitua mzigo wa madeni makubwa na kulipa ahueni ya baadhi ya tozo na kodi.
ATCL ina vituo 23 ambavyo ndege zake zinatua ndani na nje ya nchi ambapo inatarajia kufufua safari ambazo zilisitishwa hasa wakati wa janga la Uviko-19 ikiwemo za kwenda India.
Pia itarejesha safari za Nairobi, Kenya na Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Congo DRC).
Latest
