Dk. Mpango atoa maagizo mazito kwa ATCL akipokea ndege mpya
- Ni Boeing 737-Max 9 ndege mpya ya kisasa
- Ndege hiyo inafanya Tanzania iwe na jumla ya ndege 14
- Aitaka Wizara ya Uchukuzi na ATCL kukuza sekta ya anga.
Dar es Salaam. Makamu wa Rais Dk. Philip Mpango ameongoza maelfu ya Watanzania kupokea ndege mpya ya kisasa aina ya Boeing 737-Max 9 iliyonunuliwa na Serikali huku akiagiza kusimamiwa vyema kwa sekta ya usafiri wa anga ili kuongeza mchango wake katika pato la Taifa.
Dk. Mpango aliyemuwakilisha Rais Samia katika tukio hilo, amesema ujio wa ndege hiyo ni sehemu ya mipango ya Serikali kukuza sekta ya usafiri wa anga nchini.
“Kuwasili kwa ndege hii ya kisasa ni sehemu ya mkakati wa Serikali kuiwezesha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoa huduma bora na ya ushindani…Ufanisi katika huduma za uchukuzi utaliweka Taifa letu kwenye nafasi nzuri ya ushindani wa kibiashara lakini pia kutuongezea mapato ya fedha za kigeni na kukuza mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa,” amesema Makamu wa Rais Dk. Mpango.
Ndege hiyo iliyowasili majira ya saa nane mchana leo Oktoba 3, 2023 imenakshiwa kwa rangi ya bluu na nyeupe ikiwa na mchoro wa bendera ya Tanzania pamoja na maandishi yanayosomeka ‘Olduvai George Kazi Iendelee’ katika kichwa cha ndege na mnyama twiga katika mkia.
Zinazohusiana : Air Tanzania yapokea ndege ya mizigo kupunguza maumivu kwa wafanyabiashara
Atoa maagizo mazito
Aidha, Dk.Mpango amemuagiza Wazari wa Uchukuzi profesa Makambe Mbarawa, kuhakikisha wizara yake inasimamia utoaji wa huduma bora za usafiri wa anga ili kuongeza kasi ya ukuaji wa pato la Taifa.
“Simamieni vizuri utoaji wa huduma za usafiri wa anga ili kuongeza mchango katika pato la Taifa, fanyeni kazi kibiashara kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia sekta hii,” amesisitiza Mpango.
Mpango ametoa maagizo kwa bodi ya Shirika la Ndege Tanzania, (ATCL ) kujiendesha kwa faida ili kulinda mtaji unaotokana na fedha za zilizotolewa na kuwa Serikali haitavumilia uzembe wowote utakaojitokeza.
“Niseme wazi Serikali haitavumilia uzembe wowote utakaojitokeza tena ndani ya ATCL kama ilivyowahi kuwa miaka ya nyuma,” ameongeza Dk. Mpango.
Itakumbukwa kuwa ATCL ni miongoni mwa mashirika yaliyotajwa na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kujiendesha kwa hasara kwa kipindi cha miaka mitano mfululizo.
Katika ripoti ya mashirika ya umma ya mwaka 2021/22 CAG Charles Kichere alibainisha kuwa ATCL iliripoti hasara ya Sh35.23 bilioni ambayo ingeongezeka kama Serikali isingetoa ruzuku.
“Serikali isingetoa ruzuku hiyo, kampuni ingepata hasara ya Sh65.86 bilioni. Hii inaonesha changamoto ambazo kampuni ya ndege Tanzania inakabiliana nazo katika soko kwa sasa,” alisema CAG Kichere March 29, 2023 akiwasilisha ripoti hiyo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Hivyo huenda kuwasili kwa ndege hiyo kunakolifanya ATCL kuwa na na jumla ya ndege 14 zinazofanya safari zake ndani na nje ya nchi kutaliokoa shirika hilo kutoka kwenye rekodi za kuingiza hasara katika miaka mitano mfululizo.
Siku 14 kutatua changamoto za watumiaji
Katika hatua nyingine Mpango ametoa siku 14 kwa Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Fedha na ATCL kutatua changamoto zote zilizopo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) uliopo jijini Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume uliopo Zanzibar.
Changamoto hizo ni pamoja na kuahirishwa mara kwa mara kwa safari za ndege na gharama kubwa ya kusafirisha mizigo iliyopo katika baadhi ya viwanja vya ndege.
“Napenda kuilekeza Wizara ya Uchukuzi pamoja na Wizara ya Fedha washirikiane na wenzao wa Zanzibar ili kuchambua na kubaini kiini cha changamoto hii na kubaini hatua zinazopaswa kuchukuliwa.,” amesema Mpango.
Kwa wafanyabiashara na wauzaji wa bidhaa za chakula nchini huenda ujio wa ndege hii ukafungua fursa kwao mara baada ya Mpango kuagiza ATCL kuanza kutumia bidhaa za chakula zinazozalishwa nchini katika ndege zote zinazomilikiwa na Serikali ya Tanzania.
Latest