Serikali ya Tanzania yakamilisha malipo ya ndege tatu, kuimarisha ATCL

April 13, 2021 11:54 am · Nuzulack Dausen
Share
Tweet
Copy Link
  • Ununuzi wa ndege hizo utaifanya Serikali sasa kumiliki ndege 12.
  • Ndege hizo zinatarajiwa kuingia nchini mwaka wa fedha wa 2021/22.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema imeshakamilisha malipo ya ununuzi wa ndege mpya tatu, hatua ambayo itaongeza idadi ya ndege inazozimiliki kufikia 12.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaambia wabunge jijini Dodoma leo (Aprili 13, 2021) kuwa kati ya ndege hizo tatu, mbili ni Airbus A220-300 wakati iliyosalia ikiwa ni De Havilland Dash 8 Q400 ambazo zamani zilikuwa zinaitwa Bombardier.

“Ndege hizo zinatarajiwa kuwasili mwaka 2021/22 na hivyo kuiwezesha Serikali kuwa na ndege zake 12,” amesema Majaliwa bila kutaja bei iliyotumika kuzinunua ndege hizo. 

Kiongozi huyo amesema Serikali inaimarisha miundombinu ya anga ili kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi ikiwemo utalii huku akilisifu Shirika la ndege Tanzania (ATCL) kwa kupanua safari zake za ndege za ndani na kimataifa.

Hivi karibuni ATCL ama maarufu kama Air Tanzania ilitangaza kurejesha safari zake za kwenda Guangzhou, China.

“Safari hizo zitakuwa chachu ya kuimarisha utalii, biashara na ajira,” amesema Majaliwa.

Ununuzi wa ndege hizo tatu utaisadia ATCL kuongeza idadi ya ndege na kufikia maeneo mengine zaidi. De Havilland wanaeleza kuwa Dash 8 Q400 zina uwezo wa kubeba abiria hadi 90 wakati Airbus A220-300 zina uwezo wa kubeba abiria hadi 150 kwa wakati mmoja.


Soma zaidi: 


Hata hivyo, ATCL itahitajika kufanya mabadiliko makubwa ya kibiashara ili iweze kufikia uwezo wa kupata faida baada ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kubainisha kuwa mwaka 2019/20 ilipata hasara ya Sh60 bilioni. Mwenendo huo wa hasara umeliandama shirika hilo kwa miaka mitano iliyopita.

ATCL, inayoendesha biashara zake kwa ndege nane hadi sasa, imekua kwa kasi katika miaka mitano iliyopita baada ya mwenendo wake wa biashara kuzorota.

Kwa sasa Air Tanzania inachuana vikali na Shirika la ndege la Precision Air baada ya kampuni ya ndege ya FastJet kumwaga manyanga miaka miwili iliyopita.

Kumekuwepo na mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii na bungeni kwa baadhi ya watu wakieleza kuwa ununuzi wa ndege hauna tija kwa kuwa unailetea hasara Serikali wakati wengine wakisema ni bora biashara hiyo iendelee ili kusaidia kukuza shughuli nyingine za kiuchumi hususan utalii.

Enable Notifications OK No thanks