Serikali kuimarisha miundombinu ya usafiri kuboresha huduma za uchumi na utalii
- Ni pamoja na kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga, reli, bandari na barabara.
Dar es Salaam. Serikali imesema inaendelea kuchukua hatua kuboresha miundombinu ya usafiri ikiwemo anga, reli, bandari na barabara, kwa lengo la kupanua wigo wa utoaji huduma na kukuza sekta za uchumi hususan utalii na usafirishaji.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 26, 2026, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amesema maboresho hayo ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafirishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Kufikia mwaka 2050 tunategemea nchi yetu itakuwa na watu zaidi ya milioni 120…kwa kutambua hili Serikali imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya usafiri na usafirishaji,” amebainisha Msigwa.
Kwa upande wa usafiri wa anga, Msigwa amesema Serikali imepanga kuongeza ndege nane katika Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) ifikapo mwaka 2030, hatua itakayoongeza idadi ya ndege kufikia 24 na kuongeza ufanisi wa huduma kwa abiria.
Amefafanua kuwa mwaka 2026 Serikali itanunua ndege nne aina ya Bombardier Q400, huku nyingine zikitarajiwa kununuliwa katika awamu zinazofuata.
“Tutaongeza zaidi ndege aina ya Bombardier Q400 ili kupanua vituo vya safari za ndani na kurahisisha usafiri kwa wananchi,” amesema Msigwa.
Katika sekta ya reli, Msigwa amesema Serikali kwa kushirikiana na Zambia imesaini makubaliano na Serikali ya China kwa ajili ya kuanza ukarabati wa reli ya Tanzania-Zambia Railway Authority (TAZARA) ili kuongeza ufanisi wa usafirishaji wa mizigo na abiria katika reli hiyo.

“Tunakarabati reli hii kwa mkataba wa Dola za Marekani bilioni 1.4 sawa na Sh3.5 trilioni,” amebainisha Msigwa.
Akizungumza kuhusu badari amesema upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam unaendelea, ukihusisha ujenzi wa magati 10 na matenki 15 ya kuhifadhi mafuta yenye ujazo wa mita za ujazo 378,000.
Aidha, amesema ujenzi wa magati mawili ya awali yenye urefu wa mita 500 unatarajiwa kuanza Juni 2026.
“Hii itatuongezea sana biashara katika huu ukanda na kupunduza sana gharama za usafiri,” amesema Msigwa.
Aidha , Msigwa ameongeza kuwa ili kupunguza msongamano wa makasha bandarini, Serikali inaendelea na mipango ya kuendeleza bandari nyingine ikiwemo Bandari ya Bagamoyo pamoja na miradi ya bandari katika ukanda wa Ziwa Victoria. Kwa mujibu wa Msigwa, hatua hizo zitasaidia kuongeza biashara katika ukanda huo na kupunguza gharama za usafirishaji.
Hata hivyo, ufafanuzi wa Msigwa kuhusu miundombinu ya usafirishaji unakuja katika kipindi ambacho baadhi ya wananchi wamekuwa wakilalamikia changamoto za ucheleweshwaji wa safari na ufanisi wa huduma, hususan katika reli ya kisasa (SGR) na safari za ATCL licha ya kila mara kutolea ufafanuzi malalamiko hayo.
Latest