Utoaji chanjo ya Uviko-19 bado kitendawili Afrika

September 3, 2021 8:24 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Lengo hilo linatakiwa kufikiwa mwezi Septemba 2021.
  • Mataifa 42 kati ya 54 ya Afrika yatashindwa kufikia lengo hilo.
  • WHO kuongeza kasi ya usambazaji chanjo.

Dar es Salaam. Bara la Afrika litashindwa kufikia lengo la dharura la ulimwengu la kutoa chanjo ya COVID-19 kwa asilimia 10 ya watu wake ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba 2021, limeeleza Shirika la Afya Duniani (WHO).

WHO kanda ya Afrika imesema mataifa 42 kati ya 54 ya Afrika karibu asilimia 80 yatashindwa kufikia lengo hilo ikiwa kasi ya sasa ya utoaji wa chanjo haitaongezeka.

Mpaka sasa nchi tisa za Afrika ikiwemo Afrika Kusini, Morocco na Tunisia zimeshafikia lengo hilo la ulimwengu lililowekwa mwezi Mei, katika mkutano mkuu wa nchi wanachama wa WHO. 

Kwa kasi ya sasa inategemewa nchi nyingine tatu huenda zikafikia lengo ifikapo mwishoni mwa mwezi Septemba 2021. 

“Suala la uhifadhi wa chanjo umeirudisha nyuma Afrika, na tunahitaji chanjo zaidi kwa haraka, lakini kadri dozi nyingi zinavyofika, nchi za Kiafrika lazima zifanye haraka ili kuweza kusonga mbele na mipango sahihi ya kutoa chanjo kwa haraka kwa mamilioni ya watu ambao bado wanakabiliwa na tishio kubwa kutoka kwa Uviko-19, “amesema Dk Matshidiso Moeti, Mkurugenzi WHO Kanda wa Afrika.

Mwezi Agosti, 2021 jumla ya chanjo zilizofikishwa bara la Afrika kupitia mfumo wa utoaji chanjo wa pamoja wa COVAX zilikuwa milioni 21, hili ni ongezeko kubwa ikiwa ni sawa na chanjo zote zilizotolewa katika kipindi cha miezi 4 iliyopita. 

Chanjo nyingi zaidi zinategemewa kuwasili barani Afrika kutokea mfuko wa COVAX na Umoja wa Afrika (EU) kufikia mwishoni mwa Septemba, chanjo za kuweza kutosha kufikia lengo la asilimia 10. 

Takwimu za utoaji chanjo

Chanjo milioni 143 zimewasili barani Afrika na jumla ya watu waliochanjwa ni milioni 39 sawa na kusema asilimia 3 ya idadi ya watu wa bara hilo ndio wamepata chanjo. 

Ikilinganishwa na nchini Marekani ambapo asilimia 52 ya watu wake wamepata chanjo na bara la Ulaya takwimu zikionyesha asilimia 57 ya watu wameshapata chanjo. 

“Ukosefu huu wa usawa unasumbua sana. Asilimia 2 tu ya dozi zaidi ya bilioni tano zilizotolewa ulimwenguni zimetolewa barani Afrika. Lakini kuongezeka kwa hivi karibuni kwa usafirishaji wa chanjo na ahadi zinazoendelea kutolewa kunaonyesha kuwa utoaji chanjo kwa haki zaidi, usambazaji kimataifa wa chanjo unawezekana,” amesema Dk Moeti.

Hata hivyo mkuu huyo wa WHO Afrika amehimiza nchi za bara hilo lazima zishughulikia mapungufu ya utendaji na kuendelea kuboresha na kurekebisha kampeni zao za chanjo ya Uviko-19. 

Kati ya nchi 30 ambazo zimewasilisha takwimu zao WHO juu ya utayari wa utendaji kazi wao, ni nchi moja kati ya mbili haijafanya mapitio ya hatua, ambazo ni muhimu kwa kutathmini na kupanga vizuri maendeleo ya utendaji wao. 

Pia ni nchi mmoja kati ya nchi tatu hawajawasilisha mipango yao ya Kitaifa ya kusambaza chanjo, ambayo inaonyesha  masuala yote ya kampeni ya utoaji chanjo ya Yviko-19 katika kila nchi.

Kwa mujibu wa WHO, wagonjwa wa Uviko-19 wamepungua kidogo barani Afrika lakini bado wagonjwa wanaendelea kuteseka na janga hilo.

Takwimu zinaonesha idadi inayoongezeka ya kesi mpya ni katika Afrika ya Kati, Mashariki na Magharibi ambapo wamefanya idadi kuongezeka hadi kukaribia 215,000 katika wiki inayoishia 29 Agosti huku zaidi ya vifo 5,500 viliripotiwa.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW