Ahueni: Kasi ya kupeleka chanjo za Uviko-19 barani Afrika yaongezeka
- Wiki iliyopita Afrika imepokea takribani dozi milioni 4 ikilinganishwa na dozi 245,000 za mwezi Juni.
- Hadi sasa takribani chanjo milioni 79 zimewasilishwa Afrika na watu milioni 21 wamepatiwa chanjo.
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) limesema kumekuwa na kasi kubwa ya bara la Afrika kupelekewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona, jambo linaoweza kusaidia kupunguza madhara ya ugonjwa huo ikiwemo vifo.
WHO imebaini ndani ya wiki mbili zilizopita kumekuwepo na ongezeko kubwa la maambukizi ya ugonjwa huo.
Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Dk Matshidiso Moeti amesema wiki iliyopita Afrika imepokea takribani dozi milioni 4 za chanjo dhidi Uviko-19 ikilinganishwa na dozi 245,000 zilizosafirishwa kupitia mpango wa COVAX katika kipindi chote cha mwezi uliopita wa Juni.
Miongoni mwa nchi zilizopokea chanjo hivi karibuni ni Tanzania ambayo kupitia COVAX na kwa msaada wa Marekani imepokea dozi zaidi ya milioni 1 za chanjo aina ya Johnson & Johnson.
Lengo la COVAX ni kusambaza dozi milioni 520 kwa Afrika ifikapo mwisho wa mwaka huu wa 2021, chanzo zinazosambazwa kupitia mfuko wa wadhamini wa Muungano wa Afrika AU wa upataji wa chanjo, AVAT.
Inakadiriwa kuwa ifikapo mwezi Septemba, kila mwezi chanzo milioni 10 zitakuwa zinasambazwa Afrika.
Waziri wa Afya nchini Tanzania Dk Dorothy Gwajima akizungumza baada ya kuwasili kwa chanjo za COVID-19 jijini Dar es salaam tarehe 24 Julai 2021. Picha| UNICEF/Daniel Msirikale.
Hadi sasa takribani chanjo milioni 79 zimewasilishwa Afrika na watu milioni 21 wamepatiwa chanjo sawa na asilimia 1.6 ya idadi ya watu barani humo wenye umri wa kupatiwa chanjo.
Nchi za kipato cha juu zimetoa mara 61 ya kiwango hicho cha chanjo ikilinganishwa na nchi maskini.
Ili kuwapatia chanjo wakazi wa Afrika kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2021, bara hilo linahitaji dozi milioni 820 kwa chanzo za dozi mbili mbili.
Chanjo ya Johnson & Johnson ndiyo inayotolewa mara moja lakini Prifzer, Moderna na AstraZenaca zinatolewa dozi mbili mbili.
“Tunaona mwanga sasa katika upelekaji chanjo Afrika, lakini nasihi nchi zenye ziada zipeleka chanjo kwa Afrika. Nasihi nchi za Afrika nazo zichangamke na ziwe tayari kwa kuwa naona ukame wa chanjo sasa unakaribia kumalizika,” amesema Dk Moeti jana Julai 28, 2021.
Latest
